Mkoa wa Kilwa (DOA)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mkoa wa kihistoria wa Kilwa mnamo 1913 (na. VIII)
Boma la Kierumani Kilwa Kivinje ilikuwa makao makuu ya mkoa huu wa kihistoria

Mkoa wa Kilwa ilikuwa mkoa mmoja kati ya mikoa 21 ya koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (DOA, Deutsch Ostafrika) iliyokuwa mtangulizi wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi wa leo.

Mkoa huu ulikuwa na eneo la kilomita za mraba 56,900 pamoja na visiwa vya Mafia, Kilwa Kisiwani na Songo Mnara. Makao makuu (jer. Bezirksamt) yalikuwepo Kilwa Kivinje. Ofisi ndogo za mkoa (jer. Bezirksnebenstelle) zilikuwepo Kibata, Liwale na Chole (Mafia)

Mkoa huu ulipakana na

  • Mkoa wa Rufiji (VI kwenye ramani) upande wa kaskazini (mpaka ulikuwa mto Rufiji)
  • Mikoa ya Morogoro (VII), Mahenge (XXI) na Songea (XXII) upande wa magharibi (mpaka ulifuata mito ya Mbaragandu, Luwegu na Rufiji)
  • Mkoa wa Lindi (IX) upande wa kusini (mpaka ulifuata mto Mbemkuru)

Mwaka 1913 kulikuwa na wakazi 98,000. 96,200 walihesabiwa kama wazalendo, Wazungu 49, na wengine waliotazamiwa kuwa Waarabu au Wahindi. Mifugo ilikadiriwa kuwa ng'ombe 3090, mbuzi 5190 na kondoo 390.

Kabla ya 1914 yalikuwepo makampuni 6 ya kizungu na walowezi 7 walioanzisha mashamba ya kibiashara ya pamba, miti ya mpira, minazi, misufi na mikonge. Mashamba haya ya kizungu yalikuwa na eneo la 87.9 km² na 13.7 km² pekee zililimwa hali halisi hadi wakati ule.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]