Divai
Divai nyekundu na nyeupe |
Divai (kutoka Kifaransa du vin) ni kileo kinachotengenezwa kwa majimaji ya zabibu.
Pengine inaitwa pia: mvinyo (kutoka Kireno vinho), ingawa jina hilo linaweza kutumika kwa vileo vikali zaidi.
Inawezekana kutumia pia majimaji ya matunda mengine ili kupata kinywaji cha kufanana ingawa watu wengine hawapendi kukiita "divai".
Zabibu na divai
[hariri | hariri chanzo]Kimsingi maji ya zabibu huwa divai kwa kuchachuka kwa sukari iliyomo ndani yake.
Zabibu hupondwa zikiachwa katika chombo kikubwa kwa kuchachua. Maji ya mizabibu huwa na sukari nyingi pamoja na asidi ndani yake inayohitajika kwa ladha inayolengwa.
Divai safi haitakiwi kutiwa nyongeza yoyote. Nyongeza zinazotokea ni hasa sukari kama kiwango chake ndani ya zabibu hakitoshi.
Kazi ya kuchachua inaendelea kwa kawaida kutokana na hamira asilia zinazokaa kwenye maganda; lakini inawezekana pia kuongeza hamira za pekee.
Aina za divai
[hariri | hariri chanzo]Aina mbili zinazotengenezwa hasa ni divai nyekundu na divai nyeupe.
Divai nyeupe hupatikana kama maji ya zabibu pekee huchachua. Divai nyekundu inapatikana kama tunda lote yaani maji pamoja na maganda huchachua.
Kuna aina za divai za kuchemka yaani zinatoa viputo vya gesi vidogovidogo. Maarufu kati ya divai hizo ni shempeni kutoka mkoa wa Champagne katika Ufaransa.
Divai katika historia
[hariri | hariri chanzo]Divai imejulikana tangu miaka mingi; kuna dalili za kiakiolojia ya kwamba imepatikana katika sehemu za Uajemi na Kaukazi tangu miaka 5000 KK.
Imekuwa sehemu ya utamaduni ya nchi nyingi hasa katika mashariki ya kati na nchi za kandokando ya Mediteranea.
Waroma wa Kale waliipeleka katika sehemu zote za dola lao.
Lakini upatikanaji umetegemea na hali ya hewa; divai inahitaji kiwango chake cha jua na mvua, kwa hiyo kwenye tabianchi za kaskazini ya Ulaya mizabibu haistawi.
Divai katika dini
[hariri | hariri chanzo]Iliingia pia katika dini za Misri, Babeli na Ugiriki ya Kale. Osiris (Misri), Dionisi (Ugiriki) na Gilgamesh (Babeli) walikuwa miungu iliyohusika na divai ama kwa kuileta kwa binadamu au kwa kulinda kilimo chake.
Katika Biblia
[hariri | hariri chanzo]Katika Biblia Nuhu anatajwa kama mnywaji wa kwanza wa divai. Katika kitabu cha Zaburi divai ni ishara ya furaha, kwa kitabu cha Mithali ni dawa la mwenye huzuni lakini kuna pia maonyo dhidi ya hatari za ulevi.
Kitabu cha Yoshua bin Sira (31:27-29) kinasema: ”Kwa wanadamu mvinyo ni kama maji ya uzima, ukinywa kwa kiasi. Je, anao uzima gani mtu asiye na mvinyo? Nayo imeumbwa ili kuwafurahisha wanadamu. Mvinyo ni furaha ya moyo na changamko ya roho, ikinywewa kwa wakati wake na ya kutosha. Lakini kunywa mno ni uchungu wa roho, na fedheha, na ugomvi.”
Katika Agano Jipya Yesu anatumia divai na mzabibu kama ishara za uzima wa milele na pia kwa umoja wa watakatifu. Jinsi ilivyo katika Uyahudi kwenye ibada ya jioni ya Sabato, divai ni sehemu za ibada ya Ekaristi au chakula cha Bwana.
Katika Uislamu
[hariri | hariri chanzo]Uislamu ni dini ambamo wafuasi wengi hupinga divai pamoja na vinywaji vya kileo.
Qurani yenyewe ina matamko mbalimbali juu ya divai. Mizabibu ni sehemu ya uumbaji wa Allah (sura 16, 10-11), kwenye Paradiso waumini watakuwa na maji, maziwa, divai na asali tele (sura 47,15). Sura 2,119 inaona pande mbili kwenye divai: "Wanakuuliza juu ya divai (Kar. khamar)[1] na kamari. Sema: Katika hivyo mna madhara makuu na manufaa kwa watu. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake." Katika sura 5, 90-91 divai hutajwa kama uchafu na kazi ya shetani.
Aya hizi zinachukuliwa na wataalamu wengi kama kupiga marufuku divai na kileo kwa jumla; wataalamu wachache huona ya kwamba Qurani haitumii neno "haramu" kwa hiyo wanataka kupiga marufuku si divai yenyewe lakini kiasi kile kinacholeta ulevi. Hoja la kupiga ulevi wote marufuku limekuwa hoja kuu kati ya Waislamu; inaonekana pia katika hadithi kadhaa za mtume Muhammad.
Nchi zinazovuna divai kwa wingi
[hariri | hariri chanzo]Zabibu zinazofaa kwa divai zinastawi vizuri duniani kati ya latitudo ya 30 na 50 upande wa kusini na kaskazini ya ikweta.
Nafasi | Nchi |
Zao (tani) |
---|---|---|
1 | Ufaransa | 5,349,333 |
2 | Italia | 4,711,665 |
3 | Hispania | 3,643,666 |
4 | Marekani | 2,232,000 |
5 | Argentina | 1,539,600 |
6 | Australia | 1,410,483 |
7 | China | 1,400,000 |
8 | Afrika Kusini | 1,012,980 |
9 | Chile | 977,087 |
10 | Ujerumani | 891,600 |
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ tafsir ya Sheikh Al-Farsy hutumia neno "ulevi" kwa "khamr" الخمور
- ↑ FAO Ilihifadhiwa 19 Juni 2012 kwenye Wayback Machine. production statistics
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- The Wine Institute Ilihifadhiwa 3 Julai 2008 kwenye Wayback Machine.
- 'www.guidale.com' Wine of France, directory of French producers
- 3000 word report - Comprehensive overview importance of various wine stemware, wine glasses Ilihifadhiwa 8 Aprili 2008 kwenye Wayback Machine.
- Varieties of red wines - (Kiingereza) (Kifaransa)
- Wine storage - (Kiingereza) (Kifaransa)
- Wine vintages, vintage charts - (Kiingereza) (Kifaransa)
- GWF (Georgian Wine Family) Ilihifadhiwa 27 Septemba 2007 kwenye Wayback Machine. - (Kiingereza) (Kirusi)
Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Divai kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |