Ufufuko

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa Leonhard Kern, Njozi ya Ezekieli, kwenye Schwäbisch Hall.

Ufufuko (kutoka kitenzi "kufufua") ni hali ya mwili kurudi kuishi baada ya kufa, kwa mfano wa kuamka kutoka usingizini.

Dini mbalimbali zinasadiki uwezekano wake, ingawa kwa misingi na mitazamo tofauti.

Kuna visasili kuhusu miungu kufa na kufufuka mara kwa mara, kwa mfano wa uhai wa uasilia katika mzunguko wa majira, hasa katika majira ya kuchipua baada ya majira ya baridi.

Tofauti na hadithi hizo, Biblia inafundisha uwezo wa Mungu juu ya kifo cha binadamu, kwamba kupitia manabii kama Elia na Elisha, yeye aliwarudishia uhai watu waliokufa tangu muda mfupi.

Baada ya nabii Ezekieli kupata njozi kuhusu ufufuko wa mifupa mikavu iliyozagaa bondeni, Wayahudi walizidi kukubali kwamba Mungu atafufua wafu wote.

Injili zinasimulia jinsi Yesu Kristo alivyofufua vijana watatu kwa nyakati tofauti: binti Yairo, mvulana wa Nain na Lazaro wa Bethania.

Lakini jambo kuu la vitabu hivyo ni kwamba mwenyewe aliweza kufufuka siku ya tatu baada ya kufa msalabani, tena si kwa kurudia maisha ya duniani, bali kwa kuingia uzima wa milele akiwa na mwili mtukufu.

Yesu alitabiri kwamba atarudi kutoka huko siku ya mwisho ili afufue wafu wote na kuwahukumu. “Ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi” (Lk 21:27). “Saa yaja ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuko wa uzima, na waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu” (Yoh 5:28-29). “Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele” (Math 25:46).

Mwili utakaofufuliwa ni huuhuu tulionao sasa, lakini katika hali tofauti, alivyoeleza Mtume Paulo: “hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika” (1Kor 15:42).

Uislamu pia unafundisha kwamba mwishoni kutakuwa na ufufuo wa wafu wote (Yawm al-Qiyāmah, kwa Kiarabu: يوم القيامة‎‎). Siku hiyo imepangwa na Mungu lakini haijafunuliwa kwa binadamu.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.