Papa Gregori I

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Papa Gregori I.
Gregori akishughulikia muziki mtakatifu.
Mchoro wa Andrea Mantegna juu ya Gregori akiwa na Yohane Mbatizaji, Benedikto wa Nursia na Jeromu.
Papa Gregori I.
Kaburi la Gregori I, ndani ya Basilika la Mt. Petro huko Vatikano.

Papa Gregori I (Roma, Italia, takriban 540 – Roma, 12 Machi 604) alikuwa papa kuanzia 3 Septemba 590 hadi kifo chake.

Alimfuata Papa Pelagio II akafuatwa na Papa Sabinian.

Jina lake la kuzaliwa pia lilikuwa Gregorius. Kutokana na umuhimu wake katika historia, hasa ya Kanisa na Italia, aliongezewa lile la Magnus, yaani "Mkuu".

Lakini mwenyewe, aliposikia kuwa Patriarki wa Konstantinopoli alijiita "Patriarki wa ekumene", aliitikia kwa kujiita "Servus servorum Dei" (yaani "Mtumishi wa watumishi wa Mungu"), jina linalotumiwa hata leo na kila Papa.

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Septemba.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Utoto na ujana[hariri | hariri chanzo]

Gregori alizaliwa mwaka 540 hivi katika familia ya ukoo maarufu ya Anici, akiwa mtoto wa seneta Gordianus na wa Silvia. Kati ya mababu wake kulikuwa na Papa Felisi II na Papa Agapito I.

Alipokuwa na umri wa miaka 25 tu alichaguliwa kuwa mkuu wa jiji la Roma.

Mmonaki na balozi wa papa[hariri | hariri chanzo]

Akivutiwa na mfano wa Benedikto wa Nursia, aligeuza nyumba yake mjini kuwa monasteri na kujifanya mmonaki, halafu akajitahidi katika maisha ya sala na kutafakari Biblia. Pia alianzisha monasteri 6 katika kisiwa cha Sicilia.

Lakini mapema papa Pelagio II alimfanya shemasi akamtuma kama balozi kwenye ikulu ya Konstantinopoli, alipobaki miaka sita akiendelea kuishi kimonaki kati ya fahari za mazingira ya Kikaisari.

Upapa[hariri | hariri chanzo]

Aliporudi Roma, mwaka 586, akarejea monasterini, lakini tarehe 3 Septemba 590 alishangiliwa na umati wa watu awe Papa wa 64. Ndiye mmonaki wa kwanza kufikia upapa, ingawa hakutaka.

Mapema alijitokeza kama mtendaji bora hata upande wa jamii na siasa (kwa sababu hiyo aliitwa "Mrumi wa mwisho"), ingawa alikuwa na afya mbovu.

Aliwasiliana na viongozi wa nchi mbalimbali za Ulaya, na hasa wa kabila la Wafranki ambalo lilikuwa la kwanza kati ya yale ya Kijerumani kuingia Ukatoliki moja kwa moja pamoja na kujitokeza kama lenye nguvu kuliko yote.

Tena alifanikisha uongofu wa makabila ya aina hiyo yaliyoteka Uingereza, alipomtuma kama mmisionari Augustino wa Canterbury, priori wa monasteri yake ya Mt. Andrea.

Alilinda pia Roma dhidi ya uvamizi wa Agilulf, mfalme wa Walombardi, ambao alijenga nao uhusiano mpya ili kuwaleta kwenye Kanisa Katoliki kutoka uzushi wa Ario, kama alivyofanya pia na walioendelea kufuata dini za jadi.

Lakini mafanikio yake hayo yalimfanya achukiwe na watu wa Konstantinopoli.

Alipambana na matatizo mengine ya Italia, kama vile mafuriko, njaa, tauni, akisimamia kwa usawa masuala ya kijamii yaliyopuuziwa na wawakilishi wa kaisari.

Alishughulikia hata huduma ya maji.

Alirekebisha liturujia ya Kiroma, akipanga matini ya zamani na kutunga mengine mapya, pamoja na kushughulikia muziki wa ibada za Kilatini ambao kwa heshima yake unaitwa wa Kigregori.

Vitabu vyake, barua 848 zilizotufikia pamoja na hotuba mbalimbali vinashuhudia kazi zake nyingi na ujuzi wake wa Biblia.

Pia aliandika maisha ya watakatifu kadhaa wa Italia, kama vile Benedikto wa Nursia ambaye tunamfahamu kwa njia hiyo tu.

Kitabu kingine kilichoacha athari kubwa ni Mwongozo wa Kichungaji kwa ajili ya maaskofu.

Alieneza mafundisho ya Augustino wa Hippo, akisisitiza kama yeye hali ya dhambi ya binadamu, nafasi ya kwanza ya neema katika wokovu pamoja na imani katika uteuzi wa watakaookoka uliofanywa na Mungu.

Pia alichangia ustawi wa fundisho la uwepo wa toharani.

Mtu huyo alikuwa wa ajabu kuliko kazi zake, akivutia kwa nguvu na upendevu wa tabia. Ndani mwake upana wa moyo na roho ya Kikristo vilitegemeza yote.

Inawezekana kusema ndiye papa wa kwanza kutumia mamlaka upande wa siasa pia, lakini bila kuweka pembeni majukumu yake ya kiroho.

Alifariki Roma tarehe 12 Machi 604.

Maandishi yake[hariri | hariri chanzo]

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]

  • Cantor, Norman F. (1993). The Civilization of the Middle Ages. New York: Harper. 
  • Cavadini, John, ed. (1995). Gregory the Great: A Symposium. Notre Dame: University of Notre Dame Press. 
  • Dudden, Frederick H. (1905). Gregory the Great. London: Longmans, Green, and Co. 
  • Ekonomou, Andrew J. 2007. Byzantine Rome and the Greek Popes: Eastern influences on Rome and the papacy from Gregory the Great to Zacharias, A.D. 590-752. Lexington Books.
  • Richards, Jeffrey (1980). Consul of God. London: Routelege & Keatland Paul. 
  • Straw, Carole E. (1988). Gregory the Great: Perfection in Imperfection. Berkeley: University of California Press. 
  • Leyser, Conrad (2000). Authority and Asceticism from Augustine to Gregory the Great. Oxford: Clarendon Press. 
  • Markus, R.A. (1997). Gregory the Great and His World. Cambridge: University Press. 
  • Ricci, Cristina (2002). Mysterium dispensationis. Tracce di una teologia della storia in Gregorio Magno. Rome: Centro Studi S. Anselmo. . Studia Anselmiana, volume 135.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]