Sikio

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Muundo wa sikio
Picha ya sikio la nje
Ngoma ya sikio.

Sikio ni sehemu ya mwili inayowezesha kusikia sauti. Wanadamu na wanyama mamalia wana masikio mawili kichwani. Wanyama wengine husikia sauti kupitia viungo vingine kama vile buibui kupitia nywele za miguu au samaki kupitia neva ndefu iliyopo chini ya ngozi kando ya mwili.

Sikio la binadamu huwa na sehemu ya nje inayoonekana na sehemu isiyoonekana iliyopo ndani ya fuvu. Usikivu wenyewe hutokea kwenye sehemu ya ndani.

Sehemu ya nje yenye kazi ya kupokea na kukusanya mawimbi ya sauti na kuyaelekeza ndani ya njia ya sikio inayoishia kwenye kiwambo cha sikio ambacho ni ngozi inayotikisishwa na sauti.

Kucheza kwa kiwambo kunasikitisha mifupa sikivu ambayo ni mifupa mitatu midogo inayoungwa nacho na mwendo wa mifupa sikivu unapokelewa na mishipa ya fahamu ya sikio la ndani ukibadilishwa kwa mishtuko ya umeme inayopita kwenye neva hadi ubongo. Chumba cha sikio la kati kimeunganishwa na koromeo kwa njia ya neli ya koromeo.

Sehemu ya kiwambo cha sikio pamoja na chumba nyuma yake penye mifupa sikivu huitwa sikio la kati. Nyuma yake kuna sehemu ya sikio la ndani. Kiungo cha mwili kinachobadilisha mwendo wa mishipa sikivu kuwa alama za neva huitwa komboli.

Kazi nyingine za masikio[hariri | hariri chanzo]

Pamoja na kupokea sauti, sikio la ndani lina pia kazi ya kutunza uwiano wa mwili likiweza kutofautisha kati ya juu, chini, kulia na kushoto.

Uchomekaji wa hereni na mapambo mbalimbali penye sikio.

Wanyama mbalimbali hutumia masikio pia kwa kupoza mwili. Hivyo tembo anatumia masikio yake kama feni.

Matatizo na magonjwa ya sikio[hariri | hariri chanzo]

Sehemu zote tatu za sikio zinaweza kuathiriwa na magonjwa na maumivu.

  • Sikio la nje huwa na ngozi laini ambayo inaweza kuumizwa na vidonda na kuambukizwa. Njia ya sauti inaumizwa kama watu wanajikuna ndani yake kwa kidole kichafu au kwa kutumia vijiti. Mara nyingi inajazwa hasa na nta ya mwilini inayokusanyika hapa na kuzuia sauti kupita vema. Daktari anaweza kusaidia kwa kuondoa nta au uchafu mwingine uliokusanyika akitumia mpira mdogo na maji ya vuguvugu.
  • Sikio la kati linapata matatizo yafuatayo: kiwambo cha sikio kinaweza kuumizwa, kwa mfano kwa kuingiza kitu ndani ya sikio, kutokana na mlio mkubwa mno kama mtu yuko karibu na mlipuko na pia kutokana na magonjwa. Magonjwa inayotokea mara yingi ni mchonyoto wa chumba cha mifupa sikivu kwa sababu bakteria zinaweza kupitia neli ya koromeo na kuingia ndani; wakati wa magonjwa ya shingoni neli hii inaweza kuvimba na kufunga bakteria ndani ya sikio la kati ambako zinasababisha mchonyoto. Mchonyoto katika sehemu hii inaleta maumivu makali. Isipotibiwa ambukizo linaweza kuathiri hata kuharibu mifupa sikivu.
  • Sikio la ndani huumia kama makelele yanazidi. Kuzidi kwa makelele au pia kupokea mlio mkubwa wa mlipuko wa karibu unaweza kuharibu neva ndogo zinazobadilisha mwendo wa mishipa fahamu kuwa alama za neva. Sehemu hii inaweza kushambuliwa pia na maambukizi ya virusi mbalimbali.

Kuna pia matatizo ambayo hayajaelewka vema na wataalamu kama tinnitus ambako mtu anasikia sauti ya kudumu ndani ya sikio hata kama wengine hawawezi kusikia kitu. Tatizo lingine ni upotevu wa usikivu upande mmoja unaotokea hasa kwa watu wanaobanwa na matatizo na shughuli nyingi. Matatizo haya yana upande wa nafsi na majaribio ya tiba huenda sambamba na kumpatia mgonjwa kipindi cha raha na mapumziko pamoja na athari nyingine za kutuliza moyo.

Pia watumiaji wa earphones ni rahisi kuumia sikio ukitumia sauti kubwa.

Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Sikio kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.