Nenda kwa yaliyomo

Ambrosi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ambrosi wa Milano)
Mt. Ambrosi alivyochorwa kwa nakshi za mawe katika kanisa lake huko Milano

Aureli Ambrosi (Trier, leo nchini Ujerumani, 340 hivi - Milano, Italia, 4 Aprili 397), alikuwa askofu wa Milano kuanzia mwaka 374 hadi kifo chake.

Ndiye aliyemuongoa na kumbatiza Agostino wa Hippo

Kati ya mambo ya pekee aliyoacha ni urithi wa tenzi na liturujia ya pekee inayoendelea kutumika Milano na sehemu nyingine kadhaa za Italia kaskazini na Uswisi ("liturujia ya Kiambrosi").

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 7 Desemba[1].

Mwanasiasa

[hariri | hariri chanzo]

Ambrosi alizaliwa mwaka 340 hivi katika familia ya Kikristo ya Dola la Roma mjini Trier, akakulia huko.

Baba yake, aliyeitwa Ambrosius Aurelianus, alikuwa liwali wa Gallia (leo Ufaransa); mama yake alijulikana kwa akili na imani yake. Ndugu zake, Satiro na Marselina wanaheshimiwa pia kama watakatifu.

Alipofiwa baba, Ambrosi alihamia Roma pamoja na mama aliyemuandaa kufuata nyayo za baba yake katika siasa. Alisomea huko, hasa fasihi, sheria na hotuba.

Liwali Anicius Probus kwanza alimpa nafasi katika halmashauri halafu (370) akamfanya gavana wa Liguria na Emilia, akiwa na makao makuu huko Milano, mji wa pili wa Italia.

Ambrosi aliendelea na ugavana hadi mwaka 374 alipochaguliwa askofu wa Milano.

Ni kwamba, baada ya kifo cha askofu Ausensi aliyefuata uzushi wa Ario, Ambrosi alikuwa amefika kanisani ili kutuliza ghasia kati ya Waario na Wakatoliki. Kumbe alipohutubia umati, akashangiliwa na pande zote mbili, "Ambrosi askofu! Ambrosi askofu!". Alitaka kukataa, kwa kuwa hata hajabatizwa, lakini hatimaye alikubali.

Alipewa mara ubatizo, kipaimara na ekaristi, halafu baada ya wiki moja daraja takatifu ya uaskofu (tarehe 7 Desemba, ambayo imekuwa sikukuu yake hadi leo) akatoa kwa Kanisa na mafukara dhahabu na fedha zake zote.

Mt. Ambrose, alivyochorwa na Francisco de Zurbarán

Kama askofu, zaidi ya useja wake, alishika juhudi za kitawa, alisaidia mafukara kwa mali zake karibu zote, akajitahidi kupata elimu ya Biblia na teolojia hasa kutoka vitabu vya Origene akaitumia vema katika kuhubiri, akifafanua kwa upana na udhati maandiko matakatifu aliyoyatafakari kwanza. Hivyo alieneza magharibi mtindo wa Lectio Divina ulioanzishwa na mtaalamu huyo wa Misri.

Augustino aliandika kwamba kila alipokwenda kumuona Ambrosi alimkuta amefikiwa na umati wa watu wenye shida mbalimbali, ambao alijitahidi kwa kila namna kuwasaidia. Kila mara kulikuwa na foleni ndefu ikisubiri kuongea naye ili kupata faraja na tumaini. Akibaki kidogo peke yake, alilisha au mwili kwa kula au roho kwa kusoma.

Mwenye nguvu na udumifu, pamoja na kipawa cha kuhisi nini inawezekanika, aliweza kuongoza jimbo vizuri ajabu kama mchungaji halisi, mwenye msimamo na busara, na hasa wema na upendo. Hivyo hakufukuza wakleri waliofuata mafundisho ya Ario.

Mwaka 378 alikutana na Kaisari Grasyano, aliyemuomba amfundishe imani sahihi kinyume na mafundisho ya Ario. Baadaye Kaisari huyo alizidi kusimama upande wa Wakatoliki akatoa hati dhidi ya wazushi (22 Aprili 380), halafu akaieneza kwa Wapagani, akiwaondolea fadhili zao za awali.

Mwaka uliofuata wote wawili walishiriki Mtaguso wa Aquileia ili kuimarisha imani sahihi katika dola.

Baada ya Grasyano kuuawa (383), ilimbidi Ambrosi azidi kupambana na wafuasi wa Ario, mmojawao akiwa Kaisari Masimo aliyedai (386) awaachie makanisa mawili ya Milano. Ambrosi alikataa katakata, akisema, "Ukinitaka mwenyewe, niko tayari kutii: unipeleke gerezani au kifoni, sitapinga; lakini sitasaliti kamwe Kanisa la Yesu Kristo. Sitaita watu kunisaidia; nitakufa kwenye altare lakini si kuikimbia. Sitahimiza watu kupiga kelele lakini Mungu tu anaweza kuwatuliza". Hivyo alihamia pamoja na wafuasi wake basilika lililogombaniwa wakaendelea kulitumia usiku na mchana.

Kadiri ya Augustino, aliyeguswa sana na umoja huo, ndiyo mwanzo wa nyimbo za Ambrosi: “Umati wenye imani ulikesha, ukiwa tayari kufa pamoja na askofu wao… Sisi pia, ingawa vuguvugu kiroho, tulishiriki katika mhemko wa wote”..

Mt. Ambrosi na kaisari Theodosius walivyochorwa na Anthony van Dyck.
Kikanisa chini ya basilika lake.

Ikulu haikupendezwa na msimamo wa Ambrosi, lakini ilimuogopa na kumhitaji katika mapambano ya siasa. Mahusiano yaliendelea kuwa magumu.

Hatimaye Theodosius I, Kaisari wa Mashariki, alipoangamiza (390) watu 7,000 huko Thesalonike (Ugiriki), Ambrosi alitisha kumtenga na Kanisa asipofanya toba kama mfalme Daudi, akamruhusu kupokea tena ekaristi baada tu ya miezi kadhaa ya malipizi.

Mtetezi wa wale wote walionyanyaswa, alipambana vilevile na seneti ya Roma na malkia ili kutetea siasa ya Kikristo kweli.

Msimamo wake ulibaki kielelezo kwa Kanisa la Magharibi hata likaendelea kudai uhuru na mara nyingi kushindana na mamlaka za serikali zisizotenda haki.

Ambrosi alipaswa pia kupambana na Wapagani waliotaka kufanya tena dini ya jadi kuwa dini rasmi ya Dola la Roma badala ya Ukristo. Alifaulu kumfanya Theodosius I atoe hati zake maarufu za mwaka 391.

Mtume wa upendo, alisaidia yeyote aliyemkimbilia, hata akauza vyombo vya ibada ili kukomboa watumwa, akisema, “Ikiwa Kanisa lina dhahabu, si kwa ajili ya kuitunza, bali ili liwape wanaohitaji”.

Tarehe 4 Aprili, siku ya Ijumaa Kuu, Ambrosi alifariki huku amenyosha mikono yake kama Yesu msalabani, akaheshimika mara kama mtakatifu.

Masalia yake, ambayo ni kati ya maiti za zamani zaidi zilizopo nje ya Misri, yanatunzwa katika kanisa lake mjini Milano.

Maandishi na teolojia yake

[hariri | hariri chanzo]

Ambrosi aliandika sana, ila si vitabu vyake vyote vimetufikia: vilikuwepo ishirini hivi vya ufafanuzi wa Biblia na vingine juu ya mafumbo ya imani na juu ya maadili. Tunazo pia hotuba za mazishi, barua, mashairi na tenzi hasa kwa ajili ya liturujia.

Kwa jumla maandishi yake ni ya kichungaji kuliko ya kinadharia, pia kutokana na jinsi alivyopata uaskofu ghafla. Alijaribu kuziba pengo la ujuzi wa kiteolojia, lakini bila mafanikio makubwa. Ndiyo sababu anategemea sana mababu waliomtangulia.

Kuhusu Kristo, anatofautisha ndani yake hali mbili (umungu na utu) na vilevile utashi wa Kimungu na ule wa kibinadamu. Alikuwa hachoki kusema, “Kwetu Kristo ni kila kitu!” akifafanua, “Ukiwa na donda linalohitaji kuponywa, yeye ndiye mganga; ukiwa na joto la homa, yeye ndiye burudisho; ukilemewa na dhuluma, yeye ndiye haki; ukihitaji msaada, yeye ndiye nguvu; ukiogopa kifo, yeye ndiye uzima; ukitamani mbingu, yeye ndiye njia; ukiwa gizani, yeye ndiye mwanga… Onja na kuona jinsi Bwana alivyo mwema: heri mtu anayemtumainia!”

Kuhusu ukombozi, alidhani kifo cha Yesu kilikuwa gharama iliyolipwa kwa shetani ili kuokoa watu.

Kuhusu Bikira Maria, alimuona hakuwa na dhambi maisha yake yote.

Kuhusu kitubio, alionelea kwamba kwa dhambi kubwa sana kitolewe mara moja tu, tena hadharani.

Sala yake

[hariri | hariri chanzo]

Ee Bwana, mwenye huruma kwa wote, uniondolee dhambi zangu, na kwa huruma washa ndani mwangu moto wa Roho wako Mtakatifu.

Uniondolee moyo wa jiwe na kunipa moyo wa nyama, moyo wa kukupenda na kukuabudu wewe, moyo wa kupata raha ndani yako, kukufuata na kukufurahia kwa ajili ya Kristo.

Orodha ya maandishi

[hariri | hariri chanzo]
Divi Ambrosii Episcopi Mediolanensis Omnia Opera, 1527

Ufafanuzi wa Biblia

[hariri | hariri chanzo]
  • Hexameron
  • De Paradiso
  • De Cain et Abel
  • De Noe
  • De Abraham
  • De Isaac et Anima
  • De Bono Mortis
  • De Fuga Saeculi
  • De Jacob et Vita Beata
  • De Joseph
  • De Patriarchis
  • De Helia e Jejunio
  • De Nabuthae Historia
  • De Tobia
  • De Interpellatione Job et David
  • De Apologia Profhetae David
  • Ennarrationes in XII Psalmos Davidicos
  • Expositio Psalmi CXVIII
  • Esposizione Evangelii Lucae
  • Expositio Isaiae Prophetae
  • De Fide ad Gratianum
  • De Spiritu Sancto
  • De Incarnationis Dominicae Sacramento
  • Explanatio Symboli ad Initiandos (imetafsiriwa kwa Kiswahili)
  • Expositio Fidei
  • De Mysteriis (imetafsiriwa kwa Kiswahili)
  • De Sacramentis (imetafsiriwa kwa Kiswahili)
  • De Poenitentia
  • De Sacramento regenerationis vel de Philosophia
  • De Officiis Ministrorum
  • De Virginibus
  • De Viduis
  • De Virginitate
  • De Instituitione Virginis
  • Exhortatio Virginitatis

Mengineyo

[hariri | hariri chanzo]
  • De obitu Theodosii
  • Epistulae, hymni, etc.

Tafsiri ya Kiswahili

[hariri | hariri chanzo]
  • MT. AMBROSI WA MILANO, Juu ya Sakramenti za kikristo (Explanatio Simboli – De Sacramentis – De Mysteriis) – tafsiri ya G. M. Brandolini na Tommaso Serra – ed. Ndanda Mission Press – Ndanda 2004 – ISBN 9976-63-664-4

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]