Yohane wa Parma

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Yohane Buralli wa Parma (Parma, Emilia-Romagna, 1209 hivi - Camerino, Marche, 19 Machi 1289) alikuwa padri wa Kanisa Katoliki kutoka Italia ambaye aliongoza utawa wa Ndugu Wadogo (1247-1257).

Papa Pius VI alimtangaza mwenye heri mwaka 1777. Anaheshimiwa hasa tarehe 19 Machi.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Kisha kujiunga na shirika na kupata upadrisho, alifundisha teolojia Bologna na Napoli.

Alishiriki Mtaguso wa kwanza wa Lyon (1245) kama mtaalamu.

Mwaka 1247 katika mkutano mkuu wa shirika ulioagizwa na Papa walimuondoa madarakani Kreshensi wa Iesi wakamchagua Yohane wa Parma mtu wa kufaa sana kwa elimu na utakatifu, aliyeongoza hasa kwa mfano wa maisha yake bora.

Kitu cha kwanza alifuta lawama na adhabu zote dhidi ya ndugu wenye ari. Halafu akatembelea kwa miguu kanda zote akiwa na kanzu moja tu tena kuukuu na kuamsha nia ya kushika kanuni na wasia wa Fransisko wa Asizi.

Ingawa aliwahi kufundisha katika vyuo vikuu vitatu, alikusudia hasa kurudisha shirika katika hali ya mwanzoni, kwa kukataa fadhili za Papa na kwa kuheshimu Maaskofu na mapadri. Hivyo mkutano mkuu (1254) ulisimamisha utumiaji wa fadhili kadhaa.

Lakini, alivyosema Egidi wa Asizi (+1262), juhudi hizo nzuri zilikuwa zimechelewa zisiweze kurekebisha shirika lote. Wapinzani walimshtaki Yohane kwa Papa, akalazimika kujiuzulu. Mkutano mkuu ulitaka aendelee, lakini mwenyewe hakurudi nyuma. Hatimaye aliombwa amchague mwandamizi wake, naye akamtaja Bonaventura wa Bagnoregio akaenda kuishi upwekeni kwa miaka 30, akikataa mara mbili ukardinali.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Rosalind B. Brooke, Early Franciscan Government: Ellias to Bonaventure, Cambridge University Press, 2004.