Egidi wa Asizi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mwenye heri Egidi alivyochorwa, Deruta.

Egidi wa Asizi (1190 hivi - 1262), alikuwa wa tatu kati ya wenzi wa kwanza wa Fransisko wa Asizi, mwanzilishi wa Ndugu Wadogo.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Hakuna habari za hakika kuhusu maisha yake kabla ya kujiunga na Fransisko mnamo Aprili 1209.

Muda mfupi baadaye aliongozana naye kuelekea mkoa wa Marche kwa mahubiri. Halafu alifuata naye na wenzao kwenda Roma ili kukubaliwa na Papa Inosenti III.

Mwaka 1212 alihiji Compostella, huko Hispania, halafu Yerusalemu, akipitia patakatifu pengine.

Baadaye alikuwa Roma, tena Tunisi, akijitahidi kupata riziki zake kwa kazi mbalimbali za mikono kama vile kutengeneza vikapu huko Ancona au kuuza maji na kuzika wafu huko Brindisi.

Baada ya kushika maisha ya upwekeni huko Fabriano, alizidi kuzama katika maisha ya sala.

Ingawa hakuwa msomi, katika sala, safari na mang'amuzi yake alijipatia hekima aliyowashirikisha wengine kwa semi zake zenye ari.

Ndiyo sababu watu wengi, wakiwa pamoja na Papa, walimkimbilia ili kusikia anasema nini kuhusu masuala mbalimbali.

Ndiyo asili ya kitabu maarufu cha Dicta (Semi zake), ambacho kiliandikwa kwa Kilatini, kilitafsiriwa katika lugha mbalimbali na kilitumika kwa madondoo katika vitabu vya watu wengine.

Alifariki mwaka 1262, akiheshimiwa kama mtakatifu. Uhalali wa heshima yake ulithibitishwa na Papa Pius VI. Sikukuu yake ni tarehe 23 Aprili.

Semi[hariri | hariri chanzo]

Toleo bora la "Dicta" ni lile la Quaracchi la mwaka 1905. Tafsiri ya Kiingereza ni:

  • "The Golden Words of the Blessed Brother Giles", together with a sketch of his life, by the writer of this article (Philadelphia, 1906).