Mbuzi (kundinyota)
Mbuzi (pia: Jadi) ni kundinyota la zodiaki inayojulikana kimataifa kwa jina lake la kimagharibi la Capricornus[1]. Ni moja ya makundinyota yanayotambuliwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2]
Nyota za Mbuzi huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Mbuzi" linaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Duniani.
Jina
Mabaharia Waswahili wamejua nyota hizi kwa jina la Jadi linalotokana na Kiarabu جدي jadi ambalo linamaanisha "mbuzi dume wa mlimani". Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa Wagiriki wa Kale waliosema Αιγόκερως ("Aigokeros") na majina yenye maana hiyohiyo yalitumiwa pia na mataifa mengi ya kale.
Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Jadi" limesahauliwa badala yake "Mbuzi“ limekuwa jina la kawaida.
Mahali pake
Mbuzi lipo angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Mshale (pia Kausi, lat. Sagittarius) upande wa magharibi na Ndoo (pia Dalu, lat. Aquarius) upande wa mashariki.
Magimba ya angani
Mbuzi ni kundinyota dogo katika Zodiaki ina nyota chache hakuna ambayo ni angavu sana. Nyota angavu zaidi ni en:Delta Capricorni au Deneb Algedi (« mkia wa mbuzi ») yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3 ikiwa umbali wa miakanuru 39.
Jina la (Bayer) |
Namba ya Flamsteed |
Jina (Ukia) |
Mwangaza unaoonekana |
Umbali (miakanuru) |
Aina ya spektra |
---|---|---|---|---|---|
δ | 49 | Deneb Algedi | 2,81–3,05 | 39 | kA5hF0mF2 III |
β | 9 | 3,21 | 330 | K0 II + A5:n | |
α | 6 | 3,74 | 106 | G8,5 III-IV | |
γ | 40 | 3,77 | 157 | kF0hF1mF2 V | |
ζ | 34 | 3,92 | 385 | ||
Tanbihi
- ↑ Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Capricornus" katika lugha ya Kilatini ni "Capricorni" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Capricorni, nk.
- ↑ The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
Marejeo
- Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 135 ff (online kwenye archive.org)
- Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
- Constellation Guide:Capricornus
- Capricornus, the sea goat, kwenye tovuti ya Ian Ridpath, Star Tales, iliangaliwa Oktoba 2017
- Capricornus, kwenye tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
Makundinyota ya Zodiaki Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa) |
||
---|---|---|
Kaa (Saratani – Cancer ) • Kondoo (Hamali – Aries ) • Mapacha (Jauza – Gemini ) • Mashuke (Nadhifa – Virgo ) • Mbuzi (Jadi – Capricornus ) • Mizani – Libra ) • Mshale (Kausi – Sagittarius ) • Ndoo (Dalu – Aquarius ) • Nge (Akarabu – Scorpius ) • Ng'ombe (Tauri – Taurus ) • Samaki (Hutu – Pisces ) • Simba (Asadi – Leo ) |