Mara (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Kundinyota ya Mara

Mara ni kundinyota inayojulikana pia kwa jina lake la kimagharibi la Andromeda[1]. Ni moja ya kundinyota zinazotambuliwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [2] Jinsi ilivyo kwenye kundinyota zote, nyota za Mara hazikai pamoja hali halisi lakini zinaonekana vile tu kutoka duniani. Hali halisi kuna umbali mkubwa kati yao. Kwa hiyo "Mara" inataja eneo la angani jinsi inavyoonekana kutoka dunia.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Mara ilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili walioitumia kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[3]

Jina la Kiswahili ni Mara latokana na kifupi cha Kiarabu المرأة المسلسلة al-mara al-musalsalah ambalo linamaanisha "mwanamke aliyefungwa kwa nyororo ". Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa mitholojia ya Wagiriki wa Kale walioita nyota hizi Ανδρομέδα ("Andromeda") kufuatana na masimulizi ya binti wa mfalme aliyefungwa kwa nyororo kwenye ufuko wa bahari ili aliwe na dubwana wa baharini lakini aliokolewa na Perseus. Hadithi hii ina mizizi tayari katika mitholojia ya Babeli. [4].

Mahali pake[hariri | hariri chanzo]

Mara inaonekana pande zote mbili za ikweta ya Dunia; katika Afrika ya Mashariki Mara inaonekana kuanzia Septemba hadi Februari. Inapatikana juu ya „M“ ya Mke wa Kurusi (Cassiopeia) na karibu na Farasi (Pegasus) na upande wa magharibi na Farisi (Perseus) upande wa mashariki.

Magimba ya angani[hariri | hariri chanzo]

Sehemu ya Mara inayotambuliwa kirahisi ni safu ya nyota nne zinazotoka kwenye pembenne ya Farasi. Nyota tatu angavu zaidi zinaitwa γ Andromedae au Alamak, β Andromedae au Mirach na α Andromedae au Sirrah zikiwa kweye mstari usionyoka.

Upande wa kusini kati ya δ Andromedae na β Andromedae doa jeupe inaonekana ambayo ni galaksi M31 inayojulikana pia kama galaksi ya Andromeda. Hii ni galaksi ya karibu zaidi na Njia Nyeupe na Dunia.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Andromeda" katika lugha ya Kilatini ni "Andromedae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Andromedae, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. ling. Knappert 1993
  4. Allen, uk 31-32

Marejeo[hariri | hariri chanzo]