Panji (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Panji (Dorado) katika sehemu yao ya angani

Panji (kwa Kilatini na Kiingereza Dorado) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu.

Mahali pake[hariri | hariri chanzo]

Panji lipo kwenye mstari wa ekliptiki karibu na nyota angavu ya Suheli (Canopus). Kundinyota jirani ni Meza (Mensa), Nyoka Maji (Hydrus), Nyavu ( Reticulum), Saa (Horologium), Patasi (Caelum), Mchoraji (Pictor) na Panzimaji (Volans).

Jina[hariri | hariri chanzo]

Panji inapatikana kati ya kundinyota zilizobuniwa tangu mabaharia, Wazungu walipozunguka Dunia yote katika karne ya 16 na kuona mara ya kwanza nyota za kusini. Hazikutajwa katika vitabu vya Wagiriki wa Kale au Waarabu. Kundinyota hii ilielezwa mara ya kwanza na mabaharia Waholanzi Pieter Dirkszoon Keyser na Frederick de Houtman katika safari yao ya kuelekea Indonesia zikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1598 katika globu ya nyota ya Petrus Plancius.

Keyser alitumia jina la Kihispania “Dorado” linalomaanisha “ya dhahabu” na hii ni rangi ya samaki ya Panji. [2]

Leo Dorado – Panji iko kati ya kundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3]. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Dor'.[4]

Nyota[hariri | hariri chanzo]

Nyota angavu zaidi ni α Alfa Doradus ambayo ni nyota maradufu ambayo ni badilifu yenye mwangaza unaoonekana wa 3.3 mag ikiwa umbali wa Dunia wa miakanuru 176[5]

Wingu Kubwa la Magellan ambayo ni galaksi kibete jirani yenye nyota bilioni 15 iko mpakani kati ya Panji na Meza (Mensa). Umbali wake na Dunia ni miakanuru 170,000.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Dorado" katika lugha ya Kilatini ni "Doradus" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Doradus, nk.
  2. Panji inaitwa pia “Fulusi” katika maeneo kadhaa ya pwani la Afrika ya Mashariki. Jina la kitaalamu ni Coryphaena hippurus.
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. Alpha APS (Alpha Doradus), tovuti ya Prof. Jim Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]