Mbweha (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa mnyama angalia hapa Mbweha

Nyota za kundinyota Mbweha (Vulpecula ) katika sehemu yao ya angani
Mbweha (Vulpecula) akimshika Bata bukini (Anser) kwenye atlasi ya nyota ya Hevelius ya mwaka 1690

Mbweha (kwa Kilatini na Kiingereza Vulpecula) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye angakaskazi.

Mahali pake

Mbweha lipo kwenye Njia Nyeupe likipakana na kundinyota la Farasi (Pegasus), Dalufnin (Delphinus), Sagita (Sagitta), Rakisi (Hercules), Kinubi (Lyra) na Dajaja (Cygnus).

Mbweha – Vulpecula lipo katikati ya nyota angavu za Vega, Dhanabu ya Ukabu (ing. Deneb) na Tairi (Altair) ambazo zinajulikana pia kama Pembetatu ya Kianganzi kwenye angakaskazi ya Dunia.

Jina

Kundinyota hili halikujulikana kwa mabaharia Waswahili wa Kale wala kwa Waarabu au Wagiriki kwa sababu nyota zake ni hafifu sana. Katika enzi ya kale nyota hizi hazikupangwa kuwa sehemu ya makundinyota maalumu. Mbweha ni kati ya makundinyota yaliyoanzishwa na mwanaastronomia Johannes Hevelius wa Danzig (Gdansk) mnamo mwaka 1690 BK. Akiwa mpika pombe na mfanyabiashara tajiri aliyeshika kwa muda pia umeya wa mji wake alikuwa hasa maarufu kwa kuangalia, kupima na kuorodhesha nyota pamoja na mke wake Elisabeth Hevelius.

Hevelius aliyelenga kujaza mapengo kati ya kundinyota akiandika kwa Kilatini alichagua jina “Anser et Vulpecula” (bata bukini na mbweha akimaanisha mbweha mwekundu (Vulpes vulpes) wa Ulaya; wimbo maarufu wa Kijerumani unaimbia mbweha aliyeiba bata).

Vulpecula - Mbweha iko kati ya makundinyota 88 yaliyoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kwa jina la Vulpecula. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Vul'.[2]

Nyota

Mbweha –Vulpecula ina nyota hafifu tu. Nyota angavu zaidi ni Alfa Vulpeculae au Anser (bata bukini) ambayo ni nyota yenye mag 4.4 ikiwa umbali wa miakanuru 497 kutoka Dunia.[3].

23 Vulpeculae ni nyota angavu ya pili ikiwa na mag 4.52 na umbali wa miaka nuru 339. Jina lake linafuata namba za Flamsteed.

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Vulpecula " katika lugha ya Kilatini ni "Vulpeculae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Vulpeculae, nk.
  2. The constellations, tovuti ya Ukia, iliangaliwa Oktoba 2017
  3. ANSER (Alpha Vulpeculae), tovuti ya prof Jim Kaler wa Chuo Kikuu cha Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje