Pembemraba (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Pembemraba (Norma ) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Pembemraba - Norma jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini

Pembemraba (kwa Kilatini na Kiingereza Norma) [1] ni jina la kundinyota dogo kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia yetu.

Mahali pake

Pembemraba lipo jirani na makundinyota ya Akarabu (Nge) (Scorpius) upande wa kaskazini, Dhibu (Lupus) upande wa kaskazini magharibi, Bikari (Circinus) upande wa magharibi, Pembetatu ya Kusini (Triangulum Australe) upande wa kusini halafu Madhbahu (Ara) upande wa mashariki.

Njia Nyeupe inapita eneo lake.

Jina

Pembemraba ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kutoka nusutufe ya kusini pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu kwa hiyo wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nazo. Kundinyota hili lilielezwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “ l’Equerre et la Regle“ lililomaanisha “mraba na rula“ yaani kifaa kilichotumiwa na wajenzi, kwa namna tofauti pia na wanabaharia.

Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) alipotazama nyota za anga ya kusini ambazo wakati ule zilianza tu kujulikana kati ya wanaastronomia wa Ulaya. Alipima nyota 10,000 akazipanga katika makundinyota na kutunga majina kwa makundinyota mapya 14[2]. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kwa Kilatini na kufupishwa kama "Norma“.

Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale. Pembemraba au Norma ipo kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] kwa jina la Norma. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Nor'.[4]

Nyota

Nyota za Pembemraba ni chache na dhaifu; hakuna inayozidi mag 3. Nyota zilizorekodiwa na Lacaille kama angavu zaidi yaani Alfa na Beta baadaye zilihamishwa kwenda kundinyota la Akarabu (Nge – Scorpius). Kwa hiyo leo hii nyota kuu ni Gamma Normae yenye mwangaza unaoonekana wa mag 4.0 ikiwa umbali wa miakanuru 129 kutoka Dunia[5].

Nyota angavu zaidi nne ambazo ni Gamma, Delta, Epsilon na Eta, zinaonyesha umbo la pembenne.

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Norma " katika lugha ya Kilatini ni "Normae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Normae, nk.
  2. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. van Leeuwen, F. (2007). "Validation of the New Hipparcos Reduction". Astronomy and Astrophysics 474 (2): 653–64. Bibcode:2007A&A...474..653V. arXiv:0708.1752. doi:10.1051/0004-6361:20078357. 

Viungo vya Nje

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pembemraba (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.