Nenda kwa yaliyomo

Twiga (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sehemu ya nyota za kundinyota Twiga (Camelopardalis) katika sehemu yao ya angani, jinsi inavyoonekana Tanzania
Ramani ya Twiga (Camelopardalis)

Twiga (kwa Kilatini na Kiingereza Camelopardalis) [1] ni jina la kundinyota kubwa lenye nyota hafifu kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia yetu.

Mahali pake

Twiga iko karibu na ncha ya anga ya kaskazini. Kwa sababu hiyo inaonekana kisehemu tu kutoka Tanzania.

Inapakana na kundinyota Farisi (Perseus), Hudhi (Auriga) na Washaki (Lynx) upande wa kusini, Dubu Mkubwa (Ursa Maior) na Tinini (Draco) upande wa magharibi, Dubu Mdogo (Ursa Minor), Kifausi (Cepheus) upande wa kaskazini na Mke wa Kurusi (Cassiopeia úpande wa mashariki.

Jina

Twiga ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa tangu mabaharia Wazungu walizunguka dunia yote yaani karne ya 16 na hapo wanaastronomia wa Ulaya walilenga kuchora ramani ya nyota zote. Wagiriki wa Kale hawakujaribu kupanga nyota zake hafifu kati ya makundinyota waliyojua. Mholanzi Petrus Plancius aliwahi kupokea taarifa ya mabaharia waliochora nyota za kusini halafu akajitahidi kujaza eneo lote la angani kwa kupanga nyota zote kwa makundinyota kwenye globu ya nyota yake. Hapo alitambua pengo kaskazini akaunda makundinyota ya Twiga na Munukero (Monoceros).

Plancius alitumia jina la Camelopardalis kwa mnyama wa twiga maana Wazungu hawakujua mnyama huyu na kutokana na maelezo waliona ana shingo ndefu kama ngamia (camel) halafu madoa kama chui (pardalis kwa Kigiriki).

Leo Camelopardalis - Twiga iko pia kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [2]. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Cam'.[3]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni β Alfa Camelopardalis yenye uangavu unaoonekana wa mag 4.03 ikiwa na umbali wa Dunia wa miaka nuru 1,000 [4]

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Camelopardalis" katika lugha ya Kilatini ni pia "Camelopardalis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Phoenicis, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  4. Alpha Cam (Alpha Camelopardalis), tovuti ya Prof. Jim Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje