Pembetatu ya Kusini (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Pembetatu ya Kusini (Triangulum Australe ) katika sehemu yao ya angani

Pembetatu ya Kusini (kwa Kilatini na Kiingereza Triangulum Australe) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia yetu.

Mahali pake[hariri | hariri chanzo]

Pembetatu ya Kusini inaonekana vema katika kanda ya Njia Nyeupe, karibu na nyota mashuhuri za Alfa Centauri (Rijili Kantori) na Beta Centauri kwenye kundinyota ya Salibu. Lipo jirani na makundinyota Kipimapembe (Norma) upande wa kaskazini, Bikari (Circinus) upande wa magharibi, Ndege wa Peponi (Apus) upande wa kusini na Madhabahu (Ara) upande wa mashariki.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Pembetatu ya Kusini ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kutoka nusutufe ya kusini pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu kwa hiyo wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nazo. Inawezekana ya kwamba mbaharia Mwitalia Amerigo Vespucci aliiona na kueleza katika taarifa moja iliyopotea baadaye. Pembetatu ya Kusini ilionyeshwa mara ya kwanza mnamo 1589 kwenye globu ya nyota ya Petrus Plancius. Ilichorwa kikamilifu zaidi katika atlasi ya nyota ya Johann Bayer iliyoitwa Uranometria mnamo 1603 na hapa kutajwa kwa jina lake la sasa yaani Triangulum Australe. [2]

Pembetatu ya Kusini ipo kati ya makundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] kwa jina la Triangulum Australe. Kifupi chake rasmi kufuatana ni 'TrA'.[4]

Nyota[hariri | hariri chanzo]

Kundinyota hili lilipokea jina lake kutokana na nyota zake tatu angavu zaidi zinazoonekana kwa umbo la pembetatu. Hizi ni α Alfa Trianguli Australis (pia: Atria) pamoja na β Beta na γ Gamma Trianguli Australis. α Alfa Trianguli Australis ni nyota jitu yenye mwangaza unaoonekana wa mag 1.91 ikiwa na umbali wa miakanuru 424 kutoka Dunia.[5]

β Beta Trianguli Australis ni nyotamaradufu yenye mwangaza wa mag2.85 ikiwa umbali wa miakanuru 40.

Karibu na mpaka na Kipimapemba kuna fungunyota NGC 6025 linaloweza kutazamiwa kwa darubini ya kawaida.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Triangulum Australe " katika lugha ya Kilatini ni "Trianguli Australis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Trianguli Australis, nk.
  2. linganisha Moore, Patrick; Tirion, Wil (1997), Cambridge Guide to Stars and Planets, Cambridge, United Kingdom: Cambridge University Press, ISBN 978-0-521-58582-8, uk 120
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. Schaaf, Fred (2008), The Brightest Stars: Discovering the Universe Through the Sky's Most Brilliant Stars, Hoboken, New Jersey: John Wiley and Sons, ISBN 0-471-70410-5, uk. 263–65.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pembetatu ya Kusini (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.