Hadubini (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa kifaa cha utafiti angalia Hadubini

Nyota za kundinyota Hadubini (Microscopium ) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya kundinyota Hadubini - Microscopium

Hadubini (kwa Kilatini na Kiingereza Microscopium) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye angakusi ya Dunia yetu.

Mahali pake

Hadubini lipo jirani na makundinyota ya Mhindi (Indus) upande wa kusini, Mshale (pia Kausi au lat. Sagittarius) upande wa mashariki, Mbuzi (zamani Jadi au lat. Capricornus) upande wa kaskazini halafu Hutu Junubi (Piscis Austrinus) na Kuruki (Grus) upande wa magharibi.

Jina

Hadubini ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kwenye angakusi pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale. Waarabu waliijua lakini walizihesabu nyota zale kama miguu ya Mshale. Kundinyota hili lilielezwa kama pekee mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “ le Microscope” lililomaanisha “hadubini“ [2].

Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) alipotazama nyota za angakusi ambazo wakati ule zilianza tu kujulikana kati ya wanaastronomia wa Ulaya. Alipima nyota 10,000 akazipanga katika makundinyota na kutunga majina kwa makundinyota mpya 14. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kuwa lat. "Microscopium” (Hadubini).[3]. Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale.

Microscopium - Hadubini lipo kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kwa jina la Microscopium. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Mic'. [4]

Nyota

Kuna nyota 57 zenye mwangaza unaoonekana wa zaidi ya mag 6.5 ambazo zinaonekana penye giza kabisa. Kwa jumla zote ni hafifu. Nyota angavu zaidi ni γ Gamma Microscopii yenye mag 4.67 ikiwa umbali wa mwakanuru 350 kutoka Dunia[5]. α Alfa Microscopii inafuata kwa mag 4.9 [6].

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Microscopium " katika lugha ya Kilatini ni "Microscopii" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Microscopii, nk.
  2. linganisha orodha ya Ridpath Constellations 2 Lacerta–Vulpecula , tovuti ya ianridpath.com, mwanaastronomia, Fellow of the Royal Astronomical Society, iliangaliwa Oktoba 2017
  3. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. gammamic.html Gamma Tel, tovuti ya Prof. Jim Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. Alpha Tel, tovuti ya Prof Jim Kaler

Viungo vya Nje