Nenda kwa yaliyomo

Dubu Mkubwa (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa maana mengine ya jina hili angalia hapa Dubu Mkubwa

Nyota za kundinyota Dubu Mkubwa (Ursa Major) katika sehemu yao ya angani (kwa mtazamaji huko Lamu, Kenya)
Ramani ya Dubu Mkubwa - Ursa Major, jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini

Dubu Mkubwa (kwa Kilatini na Kiingereza Ursa Major) [1] ni jina la kundinyota kubwa kwenye angakaskazi ya Dunia yetu.

Jina

Ursa Major (Dubu Mkubwa) ni kati ya makundinyota yaliyootambuliwa tangu zama za kale katika mataifa mengi. Mabaharia Waswahili waliijua kama Dubu Mkubwa.[2] wakitafsiri jina la Kiarabu الدب الأكبر ad-dubb al-ʾakbar. Waarabu waliwahi kutafsiri jina la Wagiriki wa Kale waliosema Μεγάλη Άρκτος megale arktos. Mataifa mbalimbali waliiona kama dubu; Mgiriki Aristoteli alieleza jina hili kutokana na mahali pake katika kaskazini na imani kuwa dubu ni mnyama mkubwa wa pekee anayeweza kuishi katika mazingira ya baridi kali.

Mataifa wanaotumia lugha za Kigermanik waliona hapa gari kubwa wakitazama nyota saba angavu zaidi; α, β, γ na δ kama matairi ya gari na ε, η na ζ kama mpini wa gari. Katika Uingereza na Marekani nyota hizi 7 zinajulikana pia kwa jina la "Big Dipper" zikitazamiwa kama upawa mkubwa wa kuchotea maji. Ursa Major ilikuwa moja ya makundinyota 48 yaliyo orodheshwa na Klaudio Ptolemaio. Hii ilithibitishwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia katika orodha ya makundinyota 88 za kisasa iliyotolewa mwaka 1930. Kifupi rasmi ni ‘Uma’ [3] [4]

Mahali pake

Dubu Mkubwa - Ursa Major iko karibu na ncha ya anga ya kaskazini. Kwa hiyo inafika tu kidogo juu ya upeo wa macho kwa mtazamaji wa Tanzania; picha inaonyesha anga jinsi inavyoweza kutazamiwa huko Lamu- Kenya.

Inapakana na makundinyota jirani ya Tinini (Draco), Twiga (Camelopardalis), Pakamwitu (Lynx), Simba Mdogo (Leo Minor), Asadi (Leo), Nywele za Berenike (Coma Berenikes), Mbwa Wavindaji (Canes Venatici) na Bakari (Bootes).

Nyota

Dubu Mkubwa - Ursa Major ni kundinyota kubwa lenye nyota nyingi.

Nyota angavu zaidi ni ε Epsilon Ursae Majoris inayojulikana pia kama Alioth yenye mwangaza unaoonekana wa mag 1.76 ikiwa umbali wa miakanuru 81 kutoka Duniani.[5]

Nyota angavu ya pili ni Dubhe au α Alpha Ursae Majoris[6].

ζ Dzeta Ursae Majoris au Mizar ni nyota ya katikati kwenye "mpini" wa sehemu inayoitwa gari au Dipper. Ni nyotamaradufu inayotambuliwa kwa macho matupu.


Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
ε 77 en:Alioth 1,69 bis 1,83 81 A0p
α 50 Dubhe (Dhahari ya Dubu) 1,81 124 K1II-III
η 85 Alkaid (Kaidi) 1,86 101 B3 V
ζ 79 Mizar (Mizari) 2,23 78 A2 V
β 48 Merak (Maraki) 2,34 79 A1 V
γ 64 Phekda (Fahidhi) 2,41 84 A0 V SB
ψ 52 3,00 147 K1 III
μ 34 Tania Australis 3,06 ca. 230 M0 III
δ 69 Megrez 3,32 81 A3 V

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Ursa Major" katika lugha ya Kilatini ni "Ursae Majoris" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Ursae Majorise, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Oktoba 2017
  4. "The IAU list of the 88 constellations and their abbreviations" ya mwaka 1922, iliangaliwa Mei 2017
  5. Stars: "Alioth", tovuti ya Prof Jim Kaler, Chuo Kikuu cha Illinois
  6. Star Tales: Dubhe, tovuti ya Prof Jim Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 63 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331