Lamu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Lamu
Lamu is located in Kenya
Lamu
Lamu
Mahali pa mji wa Lamu katika Kenya
Majiranukta: 2°16′0″S 40°55′0″E / 2.26667°S 40.91667°E / -2.26667; 40.91667
Nchi Kenya
Kaunti Lamu
Idadi ya wakazi
 - 10,000
Lamu town square.jpg
Lamu coast.jpg

Lamu ni mji mkubwa wa kisiwa cha Lamu kwenye pwani ya Kenya mwenye wakazi mnamo 10,000. Mji ni pia makao makuu ya Kaunti ya Lamu.

Mji upo upande wa kaskazini-mashariki wa kisiwa kando la kanali inayotenganisha visiwa vya Lamu na Manda. Kanali hii ni bandari asilia inayohifadhiwa na dhoruba na mawimbi makali ya bahari.

Mji wa Lamu[hariri | hariri chanzo]

Lamu lina umbo la kanda ndefu mwambaoni. Mji wa kale umegawiwa kwa mitaa arobaini lakini kuna hasa sehemu mbili ni Mkomani upande wa kaskazini penye nyumba kubwa ya mawe na Langoni upande wa kusini ambako wakazi wapya walijenga nyumba za udongo.

Jengo kubwa la mji ni boma lililokaa zamani moja kwa moja ufukoni.

Mwambao wa leo imepatikana tu tangu karne ya 19. Mwambao wa kale unaonekana kwa barabara ya Harambee (au: Usita wa Mui). Wakati wa kujenga Boma ufuko wa kale ulikuwa na maji yenye kina kidogo hivyo ikaamuliwa kujaza sehemu hizi na kupanusha eneo la mji kuingia ufukoni. Watu wenye uwezo walijenga nyumba zao kubwa na mstari wa ufuko ukaimarihswa kwa ukuta.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu wengi huamini ya kwamba mji wa Lamu uliundwa katika karne ya 14. Historia ya Kilwa ambayo ni taarifa iliyoandikwa kwa lugha ya Kiarabu mnamo karne ya 16 inadai ya kwamba chanzo cha mji kilitokea wakati wa kufika kwa familia moja kutoka Shiraz (Uajemi) katika karne ya tatu baada ya Hijra iliyonunua kisiwa kutoka watu wa bara.

Biashara ya Kimataifa[hariri | hariri chanzo]

Mji ulistawi kwenye biashara kati ya pwani la Afrika Mashariki na Bara Arabu pamoja na Uhindi. Kilwa ilikuwa kituo kwa ajili ya majahazi yaliyopita njiani. Miji yote ya Uswahilini ilinunua bidhaa kutoka Waarabu na Wahindi na kuuza pembe za ndovu, ganda la kobe na mazao pamoja na watumwa. Biashara kubwa ya Lamu ilikuwa miti aina ya mkoko yenye ubao usiooza rahisi hasa hauliwi na mchwa hivyo unafaa vizuri kwa ujenzi wa nyumba. Mikoko ilipatikana tele kwenye funguvisiwa ya Lamu lakini siku hizi imepungua mno hivyo serikali imekataa kuziuza nje.

Kipindi cha Wareno[hariri | hariri chanzo]

Wareno walifika Lamu mwaka 1506. Watawala wa Lamu walipaswa kupatana nao ingawa kuna taarifa za majaribio kadhaa za kuasi. Lamu haikuwa kati ya miji kama Malindi iliyoshikamana na Wareno kwa hiari yao. Mji ulitumia nafasi mbalimbali kuasi dhidi ya Wareno ukaabishiwa vikali kila safari hadi mwishowe Waarabu wa Omani waliwaondoa Wareni mnamo 1696 kabla ya kuteka kituo chao cha mwisho huko Mombasa 1698.

Karne za dhahabu[hariri | hariri chanzo]

Kuja kwa Wareno kulikuwa kumevuruga biashara ya Bahari Hindi pamoja na heri ya miji mingi ya Waswahili. Kuondoka kwao kulimaanisha ya kwamba nafasi zikapatikana tena. Omani ilikuwa na utawala wa pwani la Afrika ya Mashariki lakini kwa mbali tu na utawala wake haukuwa mzogo sana. Lamu ilianza kustawi kushinda miaka ya nyuma. Majengo mazuri yanayopamba mji wa kale yalijengwa wakati wa karne za 18 na hasa ya 19.

Mwisho wa karne ya 18 Lamu ikajikuta katika mashindano makali na Pate. Sultani Fumo Madi ibn Abi Bakrwa Pate alifaulu kuteka Lamu akaanza kujenga boma kubwa lililopo hadi leo. Mwanzo wa karne ya 19 Lamu iliweza kujiondoa katika utawala wa majirani kwa ushindi wake juu ya jeshi la Pate katika mapigano ya Shela mwaka 1813. Hadi mwisho wa karne Lamu ilikuwa mji wa kwanza katika funguvisiwa. Umuhimu wa biashara ya watumwa waliouzwa Zanzibar na Arabuni ikaongezeka na kazi ya watumwa iliwezesha mabwana kulima mashamba makubwa wakiuza mazao nje.

Kukwama na kurudi nyuma[hariri | hariri chanzo]

Sehemu ya pili ya karne ya 19 iliona mabadiliko tena. Usultani wa Zanzibar ulikuwa umerithi ubwana wa pwani kutoka Omani lakini uliweza kukazia utawala wake kwa sababu haukuwa mbali mno. Katika miaka tangu 1880 nchi za Ulaya zilianza kujenga ukoloni wao. Wajerumani walianzisha koloni yao katika Witu wakajenga ofisi ya Posta ya Kijerumani kwenye mji wa Lamu kwa sababu palikuwa na bandari iliyo karibu zaidi. Lakini kuja kwa Wazungu na meli zao kubwa kuliondoa pia sehemu ya biashara kutoka Lamu. Meli kubwa zilipendelea mabandari makubwa zaidi kama Mombasa au Malindi.

Headline text[hariri | hariri chanzo]

Mwisho wa utumwa[hariri | hariri chanzo]

Pigo kubwa kwa Lamu ilikuwa kukatazwa kwa utumwa. Waingereza walikuwa wakilazimisha Zanzibar kukataza kwanza biashara ya watumwa na baadaye utumwa mwenyewe. Mabwana wote wenye mashamba makubwa kwenye pwani la Uswahilini walishindwa kuendelea na mashamba yao na kupata faida kwa sababu waliokuwa watumwa hawakutaka tena kuwahudumia kama watu huru.

Eneo lililosahauliwa katika Kenya huru[hariri | hariri chanzo]

Lamu ikakwama na kurudi nyuma katika Kenya iliyoona mabadiliko ya haraka wakati wa ukoloni na baadaye wakati wa uhuru. Wilaya ya Lamu ilipaswa kubeba mzigo wa kusahauliwa kama maeneo mengine ya nchi nje ya nyanda za juu. Barabara ya lami haikufika wilaya ya lamu hadi mwaka 2006.

Miaka ya nyuma utalii umeleta tena biashara mpya lakini mara nyingi ni watu wa nje ya Lamu wanaofaidika.

Utamaduni[hariri | hariri chanzo]

Mifano bora ya usanifu wa Uswahilini inapatikana Lamu. Hivyo imepokelewa na UNESCO katika orodha la urithi wa dunia kwa sababu ni "mji wa Uswahilini uliohifadhiwa kushinda miji yote mingine".

Boma la Lamu lililojengwa na watu wa Pate leo hii ni makumbusho yanayotembelewa na wageni wengi.

Makumbusho madogo yanakumbusha kituo cha kwanza cha posta ya Kijerumani katika Afrika ya Mashariki; Lamu ilikuwa kituo cha posta kwa koloni ya Kijerumani huko Witu.

Lamu kote magari hayaruhusiwi isipokuwa gari mojamoja la mkuu wa wilaya, polisi a hospitali. Meginevyo watu hutembea na kutumia sana usafiri kwa punda.

Sherehe ya Maulidi[hariri | hariri chanzo]

Katika karne ya 20 Lamu imekuwa mahali pa sherehe ya maulidi inayovuta wageni kutoka pande zote za Uswahilini na nchi za jirani. Sheikh Habib Saleh al Habshi alifika Lamu kutoka Hadramaut (Yemeni) katika miaka ya 1880 akafundisha kwenye madrasa. Akapata wanafunzi wengi akajenga Ribat ar-Riyada mwaka 1900. Chini ya uongozi wake sherehe ya maulidi ikasheherekewa na wanafunzi wake wengi walioimba aya za sifa kwa Allah na mtume Muhammad.

Sherehe imeendelea kuvuta washiriki na watazamaji wengi hata baada ya kifo chake mwaka 1935 hadi leo.

Jahazi ya maulidi.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]