Urithi wa Dunia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Urithi wa dunia)
Nembo ya Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO.

Urithi wa Dunia ni maeneo yenye thamani kubwa ya kiutamaduni au kimazingira duniani yanayoangaliwa na shirika la UNESCO.

Hadi Septemba 2023 sehemu 1,172 katika nchi 166 zimekubaliwa. Nchi zinazoongoza kwa wingi wa mahali ni Italia (59) na China (57) zikifuatwa na Ujerumani (52), Ufaransa (51) na Hispania (50).

Afrika ina mahali 147 (8.56%) katika nchi 46, zikiongoza Afrika Kusini (10), Ethiopia na Moroko (9), Tunisia (8), Algeria, Misri, Senegal na Tanzania (7).

Orodha rasmi ya UNESCO ina mahali 913 pa urithi wa dunia wa kiutamaduni na mahali 220 pa urithi wa dunia wa kimazingira, mbali ya 39 pa mseto.

Mwanzo wa jitihada za kuhifadhi urithi wa dunia ulikuwa ujenzi wa bwawa la Assuan lililoelekea kuzamisha majengo mbalimbali ya utamaduni wa Misri na Nubia wa kale chini ya maji. Wakati ule UNESCO ilifaulu kukusanya pesa ili hekalu la Abu Simbel liweze kuhamishwa mlimani kabla ya kujaa kwa bwawa.

Tangu 1972 kuna mkataba wa kimataifa wa Stockholm kuhusu hifadhi ya urithi wa dunia kiutamaduni na kimazingira.

Kila mahali panapopendekezwa ili pakubaliwe panahitaji angalau sifa moja kati ya sita zifuatazo:

  • kuwa na thamani ya pekee ya kisanii
  • kuwa na athira muhimu katika eneo fulani au kipindi cha historia
  • kuwa kitu cha pekee kisichopatikana tena au kuwa na umri mkubwa
  • kuwa mfano bora wa kipindi fulani cha historia ya ujenzi
  • kuwa muhimu katika uhusiano na fikra muhimu au watu muhimu wa historia

Kamati ya Urithi wa Dunia hukutana kila mwaka na kuangalia maombi ya kupokelewa katika orodha ya urithi wa dunia. Kamati inapokea taarifa kuhusu hifadhi na hali ya urithi uliopo tayari orodhani. Kila baada ya miaka miwili orodha inatolewa upya.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

UNESCO World Heritage List travel guide kutoka Wikisafiri Kigezo:Library resources box