Darubini (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Darubini (Telescopium ) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Darubini (Telescopium)

Darubini (kwa Kilatini na Kiingereza Telescopium) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye angakusi.

Mahali pake

Darubini iko jirani na makundinyota ya Tausi (Pavo) upande wa kusini, Madhabahu (Ara) upande wa mashariki, Kobe (Corona Australis) na Kausi (Mshale) upande wa kaskazini halafu Mhindi (Indus) upande wa magharibi.

Mshale (zamani Kausi, lat.. Sagittarius) ipo karibu.

Jina

Darubini ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kwenye angakusi pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu kwa hiyo wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nazo. Kundinyota hili lilielezwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “le Telescope“ lililomaanisha “Darubini“.

Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) alipotazama nyota za angakusi ambazo wakati ule zilianza tu kujulikana kati ya wanaastronomia wa Ulaya. Alipima nyota 10,000 akazipanga katika kundinyota na kutunga majina kwa makundinyota mapya 14[2]. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kwa Kilatini na kufupishwa kama "Telescopium“(Darubini).

Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale.

Telescopium - Darubini iko kati ya makundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] kwa jina la Telescopium. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Tel'.[4]

Nyota

Kuna nyota 57 zenye mwangaza unaoonekana wa zaidi ya mag 6.5 ambazo hivi zinaonekana penye giza kabisa[5]. Nyota angavu zaidi ni Alpha Telescopii yenye mag 3.5 ikiwa umbali wa Miakanuru 350 kutoka Dunia[6].

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Telescopium " katika lugha ya Kilatini ni "Telescopii" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Telescopii, nk.
  2. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. linganisha orodha ya Ridpath Constellations 2 Lacerta–Vulpecula , tovuti ya ianridpath.com, mwanaastronomia, Fellow of the Royal Astronomical Society, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. Alpha Tel, tovuti ya Prof. Jima Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje