Kuruki (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Nyota za kundinyota Kuruki (Grus) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya kundinyota Kuruki - Grus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia
Kundinyota zenye majina ya ndege kwenye anga la kusini, jinsi zilivyochora na Johann Bayer katika atlasi ya nyota "Uranometria"

Kuruki (kwa Kilatini na Kiingereza Grus) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu.

Mahali pake[hariri | hariri chanzo]

Kuruki inapakana na kundinyota Hutu Junubi (Piscis Austrinus) upande wa kaskazini, Hadubini (en: Microscopium) na Mhindi (Indus) upande wa mashariki, Tukani (Tucana) upande wa kusini na Zoraki (Phoenix) upande wa magharibi.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Jina la Kuruki linamtaja ndege inayojulikana zaidi kama Korongo. Kuruki inapatikana kati ya kundinyota zilizobuniwa tangu mabaharia Wazungu walipozunguka Dunia yote katika karne ya 16 na kuona mara ya kwanza nyota za kusini. Kabla ya hayo Waarabu waliona nyota zake kati ya nyota za Hutu Junubi (Pisces Australis). Kundinyota ya Kuruki - Grus ilielezwa mara ya kwanza na mabaharia Waholanzi Pieter Dirkszoon Keyser na Frederick de Houtman katika safari yao ya kuelekea Indonesia zikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1598 katika globu ya nyota ya Petrus Plancius na kupokelewa katika "Uranometria" ya Johann Bayer.

Keyser alitumia jina la Kiholanzi “Reygher” (ndege kama Kingoyo) iliyochukuliwa baadaye katika lugha nyingine kama ndege aina ya korongo na kutajwa kwa jina la Kilatini „Grus“ (korongo). Waarabu waliitafsiri kwa كركي kurkiya iliyokuwa "Kuruki" kati ya mabaharia Waswahili[2].

Grus iko pia katika orodha ya kundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Gru.[4]

Nyota[hariri | hariri chanzo]

Kuna nyota angavu mbili katika Kuruki na hizi ni Nairi au α Alfa Gruis yenye mwangaza unaoonekana wa mag 1.73 ikiwa na umbali kutoka Dunia wa miaka ya nuru 101[5]. Mabaria waliita Nairi[6] kutokana na jina la Kiarabu Alnair (ar. النّيّر, "angavu") ambayo ni jina la kimataifa. Rangi yake ni nyeupe, nafasi yake katika Kuruki ni bawa la kulia.

Nyota angavu ya pili ni β Beta Gruis yenye umbali wa miaka ya nuru 170 na mag 2.0.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Grus" katika lugha ya Kilatini ni "Gruis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Gruis, nk.
  2. linganisha Knappert 1993
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71.
  5. Alnair (Alpha Gruis), tovuti ya Prof. Jim Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. linganisha Knappert 1993

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Astrowiki.PNG
Mradi wa Astronomia

Makala hii imewahi kukaguliwa na kuboreshwa kwenye warsha ya pamoja ya Jenga Wikipedia ya Kiswahili, Wikimedia Community User Group Tanzania na ASSAT. Imepewa hali ya ulinzi. Tunaomba mapendekezo yote ya usahihisho na nyongeza zipelekwe kwanza kwenye ukurasa wa majadiliano