Dira (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Dira ( Pyxis) katika sehemu yao ya angani

Dira (kwa Kilatini na Kiingereza Pyxis[1]) ni jina la kundinyota dogo kwenye angakusi ya Dunia yetu. Jina linataja zana ya dira.

Mahali pake

Dira ipo jirani na makundinyota ya Tanga (Vela) upande wa kusini, halafu Shetri (Puppis), Shuja (Hydra) na Pampu (Antlia). Haipo mbali na nyota angavu sana ya Shira (Sirius).

Jina

Dira ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kwenye angakusi pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu kwa hiyo pia wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nayo. Kundinyota hili lilielezwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “ la Boussole“ lililomaanisha "dira ya merikebu".

Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) alipotazama nyota za angakusi ambazo zilianza tu kujulikana na wanaastronomia wa Ulaya wakati ule. Alipima nyota 10,000 akazipanga katika makundinyota na kutunga majina kwa makundinyota mapya 14[2]. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kwa Kilatini na kufupishwa kama "Pyxis" (Dira).

Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale.

Dira ipo kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] kwa jina la Pyxis. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Pyx'.[4]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Alpha Pyxidis[5] ambayo ina mwangaza unaoonekana wa mag 3.68 ikiwa umbali wa miakanuru 880 kutoka Dunia.[6]. Ni nyotajitu yenye rangi nyeupe-buluu; mwangaza halisi ni mara 22,000 kushinda Jua letu na kipenyo chake mara 9-10 cha Jua.[7].

Mwangaza wake unaoonekana ungekuwa kubwa zaidi lakini takriban theluthi moja ya nuru yake inafichwa na vumbi ya nyota. [5]

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno " Pyxis " katika lugha ya Kilatini ni " Pyxidis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Pyxidis, nk. „ Pyxis“ kwa maana hii ni tofauti na neno „coelum“ inayoandikwa pia „ Pyxis“ yenye maana ya „anga, mbingu“
  2. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. 5.0 5.1 Kaler, Jim. "Alpha Pyxidis". Stars. University of Illinois. Iliwekwa mnamo 6 October 2012.  Check date values in: |accessdate= (help)
  6. van Leeuwen, F. (2007). "Validation of the new Hipparcos reduction". Astronomy and Astrophysics 474 (2): 653–664. Bibcode:2007A&A...474..653V. arXiv:0708.1752. doi:10.1051/0004-6361:20078357. 
  7. Nieva, María-Fernanda; Przybilla, Norbert (2014). "Fundamental properties of nearby single early B-type stars". Astronomy & Astrophysics 566: 11. Bibcode:2014A&A...566A...7N. arXiv:1412.1418. doi:10.1051/0004-6361/201423373. 

Viungo vya Nje