Nenda kwa yaliyomo

Najari (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Najari (Sculptor) katika sehemu yao ya angani


Najari (Sculptor kwa Kilatini na Kiingereza) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia.

Mahali pake

[hariri | hariri chanzo]

Najari ni kundinyota dogo karibu na nyota angavu Kinywa cha Hutu (Formalhaut). Linapakana na Dalu (Aquarius) na Ketusi (Cetus) upande wa kaskazini, Tanuri (Fornax) upande wa mashariki, Zoraki (Phoenix) upande wa kusini na Hutu Junubi (Piscis Austrinus) upande wa magharibi.


Najari lilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kwa mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2] Jina la Najari linatokana na Kiajemi نجاری najjaari ambalo linamaanisha fundi wa useremala; na hili lilichukuliwa jina la Kilatini la “sculptor” linalomtaja msanii au fundi anayejua kuchonga sanamu.

Najari ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa katika kipindi cha kisasa. Kundinyota hili lilielezwa kwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “Atelier du sculpteur “ lililomaanisha “karakana ya mchongaji ». Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) akitazama nyota za anga ya kusini ambazo zilianza tu kujulikana na wanaastronomia wa Ulaya wakati ule. Alipima nyota 10,000 akizipanga katika kundinyota na kutunga majina kwa kundinyota mpya 14[3]. Jina lilitafsiriwa kwa Kilatini na kufupishwa kama "Sculptor" (mchongaji) na kutafsiriwa katika mashariki kwa jina la mchonga ubao sawa na seremala.

Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya teknolojia kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale.

Najari ina nyota 53 zinazoweza kuangaliwa kwa macho matupu lakini hazing’ai sana ni dhaifu. Mahali pa ncha ya kusini ya anga iko ndani ya Najari lakini tofauti na anga ya kaskazini hakuna nyota inayolingana na mahali pake.

Nyota angavu zaidi ni Alfa Sculptoris yenye [[mwangaza unaoonekana]] wa 4.3 ikiwa umbali wa miakanuru 780.

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Sculptor" katika lugha ya Kilatini ni "Sculptoris" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Sculptoris, nk.
  2. ling. Knappert 1993; bado haieleweki ni lini ya kwamba majina ya “kundinyota mpya” yaliyobuniwa na Wazungu wakati wa karne za 18 na 19 yalipokelewa na Waarabu na Waswahili
  3. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 75 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Najari (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.