Ghurabu (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Ghurabu (Corvus) katika sehemu yao ya angani

Ghurabu (kwa maana „kunguru“ , kwa Kilatini na Kiingereza Corvus) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakusi ya dunia yetu.

Mahali pake

Ghurabu lipo jirani na kundinyota la Mashuke (Virgo) na nyota yake angavu Sumbula (Spica). Makundinyota jirani mengine ni Shuja (en:Hydra) na Batiya (en:Crater). Nyota zake angavu zaidi zina umbo la pembenne.

Jina

Ghurabu lilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2]

Jina la Ghurabu limepokelewa kutoka kwa Waarabu wanaosema الغراب al-ghuraab na hao walitafsiri jina la Wagiriki wa Kale walioona hapa ndege wa kunguru na kumwita Κόραξ koraks[3], lililotafsiriwa kwa Kilatini kama "Corvus" ambalo ni sasa jina la kimataifa.

Katika mitholojia ya Kigiriki kuna hadithi jinsi gani mungu Apollo alimtuma ndege ya kunguru (Ghurabu) kumchukulia maji kwa bakuli lakini ndege alichelewa kwa sababu alikula matunda njiani. Aliporudi akaeleza kuchelewa kwake kwa uwongo ya kuwa nyoka alimzuia akamwonyesha nyoka kwa kuishika kwenye miguu yake. Apollo alijua ni uwongo akakasirika na kumrusha kunguru (Ghurabu-Corvus) pamoja na bakuli (Batiya-Crater) na nyoka (Shuja-Hydra) kwenye anga wanapokaa kama nyota. Alimwadhibu ndege kwa kuweka bakuli ya maji (Batiya-Crater) karibu naye lakini hawezi kunywa.[4]

Ghurabu ni kati ya makundinyota 48 yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [5] kwa jina la Corvus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Crv'.[6]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Jinaha la Ghurabu au γ Corvi yenye mwangaza unaoonekana wa mag 2.6. Iko kwa umbali wa miakanuru 190 kutoka Dunia na rangi yake ni buluu-nyeupe.

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina la Ukia
(si rasmi)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
γ 4 Jinaha la Ghurabu 2,59m 190 B8 III
β 9 (Kraz) 2,65m 140 G5 II
δ 7 Algorab 2,94m 120 B9 V
ε 2 (Minkar) 3,02m 303 K2 III
α 1 (Alchiba) 4,02m 49 F2 IV

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Corvus" katika lugha ya Kilatini ni " Corvi" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Corvi, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. Jina la Kigiriki "koraks" linaiga sauti ya ndege mwenyewe
  4. Allen, Star-Names and their Meanings uk 180 na Crater Constellation - Myth, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Septemba 2017
  5. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  6. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 75 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331