Johann Bayer

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Kundinyota ya Orion (Jabari) katika Uranometria ya Johann Bayer

Johann Bayer (15727 Machi 1625) alikuwa mwanasheria na mwanaastronomia kutoka nchi ya Ujerumani. Alianzisha mfumo unaotumika hadi leo wa kutaja mahali pa nyota angani kufuatana na kundinyota na uangavu unaoonekana.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa mwaka 1572 mjini Rain katika Bavaria.

Alipokuwa na miaka 20 alianza masomo yake ya falsafa na sheria katika chuo kikuu cha Ingolstadt.

Baada ya kumaliza masomo yake alihamia Augsburg alipofanya kazi ya mwanasheria akawa mshauri wa kisheria wa halmashauri ya mji kuanzia mwaka 1612.[1]

Nje ya kazi yake alijisomea elimu katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na akiolojia, hisabati na astronomia.

Hakuunda familia yake, bali alibaki kapera bila kuoa akafa mwaka 1625.

Kazi[hariri | hariri chanzo]

Bayer amekuwa maarufu kwa atlasi yake ya nyota "Uranometria Omnium Asterismorum" ("Ramani ya anga ya kundinyota zote") iliyochapishwa mara ya kwanza mjini Augsburg mwaka 1603.

Hii ilikuwa ramani ya nyota ya kwanza iliyoonyesha pia nyota zinazoonekana tu kutoka nusutufe ya kusini ya Dunia, kazi iliyowezeshwa na safari za upelelezi tangu meli za Ferdinand Magellan kuzunguka Dunia yote mara ya kwanza mwaka 1521. [2] 

Bayer alitumia kazi ya Tycho Brahe, inawezekana alitumia pia atlasi ya nyota ya Alessandro Piccolomini ya mwaka 1540 ingawa Bayer aliongeza zaidi ya nyota 1,000 kwa orodha za watangulizi wake.

Katika kitabu cha Uranometria alianzisha mfumo mpya wa kutaja nyota inayojulikana kama "majina ya Bayer". Humo alipanga kila nyota katika kundinyota fulani. Ndani ya kundinyota aliipa kila nyota herufi ya Kigiriki kufuatana na uangavu: nyota angavu zaidi iliitwa Alfa, iliyofuata Beta, halafu Gamma na kadhalika.

Katika atlasi yake aliingiza kundinyota 12 mpya zilizobuniwa miaka michache iliyopita kutaja nyota za anga ya kusini ambazo hazikujulikana na wataalamu wa Ugiriki ya Kale na Roma ya Kale.[3]

Heshima baada ya kufa[hariri | hariri chanzo]

Kwenye Mwezi wa Dunia kuna kasoko iliyopokea jina la Bayer kwa heshima yake.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Hockey, Thomas (2009). The Biographical Encyclopedia of Astronomers. Springer Publishing. ISBN 978-0-387-31022-0. Retrieved on August 22, 2012. 
  2. Ridpath, Ian. Johann Bayer's southern star chart.
  3. Kanas, Nick (2009). Star Maps: History, Artistry, and Cartography, 2nd, Springer, 119-120. ISBN 978-1-4614-0916-8.