Nenda kwa yaliyomo

Shuja (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sehemu kubwa ya nyota za Shuja (Hydra) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya kundinyota Shuja (Hydra) jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia.

Shuja (kwa maana „nyoka“, kwa Kilatini na Kiingereza Hydra) [1] ni jina la kundinyota kubwa iliyopo upande wa kusini wa ikweta ya anga.

Kutokana na urefu wake Shuja inapakana na kundinyota nyingi ikiwa karibu na kundinyota za Zodiaki za Saratani (Cancer), Asadi (Leo) na Nadhifa (Virgo).

Shuja ilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2] Jina la Shuja limepokelewa kutoka kwa Waarabu wanaosema الشجاع ash-shujaaʿ kwa maana „nyoka“ [3] na hapo walitafsiri jina la Wagiriki wa Kale walioona ama nyoka au joka na kumwita Ύδρα hidra, lililotafsiriwa kwa Kilatini kama "Hydra" ambalo ni sasa jina la kimataifa.

Katika mitholojia ya Kigiriki kuna hadithi mbili kuhusu Hydra; alikuwa joka mwenye vichwa vingi aliyekaa katika kinamasi na kumeza watu waliopita; nusu mungu Herakles alipambana naye lakini aliona ya kwamba akikata kichwa kimoja kiliota upya. Hapa alipata msaada wa kijana aliyewasha moto na kuchoma mashingo kila baada ya kukata kichwa kimoja.

Hadithi nyingine ya Wagiriki kuhusu nyota hizi ilitaja nyoka katika masimulizi ya Mungu Apollo na kunguru Ghurabu. Mungu Apollo alimtuma ndege wa kunguru (Ghurabu) kumchukulia maji kwa bakuli lakini ndege alichelewa kwa sababu alikula matunda njiani. Aliporudi akaeleza kuchelewa kwake kwa uwongo ya kuwa nyoka alimzuia akamwonyesha nyoka kwa kuishika kwenye miguu yake. Apollo alijua ni uwongo akakasirika na kumrusha kunguru (Ghurabu) pamoja na bakuli (Batiya-Crater) na nyoka (Shuja-Hydra) kwenye anga wanapokaa kama nyota. [4]

Shuja ni kati ya kundinyota 48 zilizotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Lipo pia katika orodha ya kundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [5] kwa jina la Hydra. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Hya'.[6]

Nyota za Shuja ni dhaifu kiasi kuna moja pekee ambayo ni angavu na hii ni Faridi (Alphard)[7]. Ina mwangaza unaonekana wa mag 2.0. Jina lake lamaanisha „Kipweke“ kwa Kiarabu yaani الفرد (al-fard) kwa sababu ni nyota angavu ya pekee, hakuna nyingine jirani nayo iliyopo angani. ,

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Hydra" katika lugha ya Kilatini ni " Hydrae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Hydrae, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. neno la Kiarabu kimsingi ina maana sawa kama Kiswahili „shujaa“ yaani mtu hodari asiye na hofu; kwa Kiarabu ilikuwa pia namna ya kutaja nyoka asiyejificha lakini ni tayari kushambulia (tazama Lane uk 1508 Book I) ; kwa hiyo imekuwa tafsiri ya Kiarabu kwa Kigiriki „Hydra“
  4. Hydra Constellation - Myth, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Septemba 2017
  5. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  6. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  7. "IAU Catalog of Star Names", iliangaliwa Septemba 2017

Lane, Edward William: Arabic-English Lexicon (London: Willams & Norgate 1863), online hapa http://www.tyndalearchive.com/tabs/lane/