Nenda kwa yaliyomo

Mwangaza unaoonekana

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mag)
Mwangaza unaonekana kwa mfano wa kundinyota la Tauri:
mjini penye nuru nyingi nyota hadi mag 4 zinaonekana,
mashambani penye giza hadi mag 6

Mwangaza ni tabia ya nyota inayosaidia kuzitofautisha baina yake. Kuna tofauti kati ya mwangaza unaoonekana (ing. apparent magnitude) na mwangaza halisi (ing. absolute magnitude).

Umbali kati ya vitu kwenye anga-nje ni kubwa sana. Nyota kubwa kama iko mbali inaweza kuonekana hafifu, nyota ndogo kama iko karibu inaonekana angavu sana.

  • Mwangaza unaoonekana ni kipimo cha ukali wa nuru wa gimba la angani jinsi unavyoonekana kwa mtazamaji kwenye dunia yetu. Unatajwa kwa namba na kizio chake ni magnitudo, kifupi mag. Jinsi uang‘avu ulivyo juu ndivyo kiasi cha "mag" kinakuwa kidogo.[1] Kitu ang‘avu zaidi angani ni jua letu lenye uang‘avu unaonekana wa -−26,73 mag. Nyota ya Rijili Kantori ( en:Alpha Centauri) inaonekana ang‘avu kuliko nyota kubwa zaidi ya Ibuti la Jauza kwa sababu iko karibu zaidi na dunia.
  • Mwangaza halisi ni kipimo cha ukali wa nuru jinsi ingeonekana kwa mtazamaji aliyeko katika umbali sanifu. Umbali huu ulisanifishwa kuwa miakanuru 32.6[2][3] Kipimo hiki kinawaruhusu wanaastronomia kulinganisha uang‘avu wa magimba kwa kutumia umbali sanifu.

Kipimo cha magnitudo

[hariri | hariri chanzo]

Kwa kutaja kiasi cha mwangaza wanaastronomia hutumia kizio cha "magnitudo" (kifupi mag). Neno hili la Kilatini linamaanisha "ukubwa". Kadri mwangaza ulivyo mkubwa kiasi cha "mag" kinakuwa kidogo.

Kwa mfano nyota ya Sumbula ina magnitudo ya mag +1,04. Rijili ya Jabari inayojulikana pia kama Rigel ina mwangaza unaoonekana wa mag +0.12 na hapa tunaona ni kati ya nyota ng'avu zaidi kwenye anga.

Iwapo gimba la anga inang'aa sana, linakuwa na mag hasi.Mfano wake ni nyota ng'avu sana kama Shira (Sirius) na sayari za Zuhura (Venus) au Mshtarii (Jupiter).

Kipimo hakifuati mstari bali vizio vyake vinafuatana kwa hatua za logi. Kwa hiyo ongezeko la mwangaza kutoka kizio kimoja hadi kidogo kinachofuata ni takriban mara 2.5.

Kuonekana kwa nyota kunategemea mazingira. Tukiwa mjini penye mwanga mwingi tunaona nyota hadi mag 4, tukiwa mashambani penye giza tunaona nyota nyingi zaidi hadi mag 6-7.

Historia ya kipimo

[hariri | hariri chanzo]

Chanzo cha vipimo hivi ni kazi ya Hipparchos wa Nikaia mtaalamu wa Ugiriki ya Kale. [4] Aliorodhesha nyota kufuatana na ung'avu akazipanga nyota angavu zaidi kwenye daraja la kwanza, zile zilizoonekana hafifu zaidi katika madaraja ya pili, tatu na kadhalika hadi daraja la sita. Orodha yake ilikuwa msingi wa kitabu mashuhuri cha Almagest cha Klaudio Ptolemaio kilichoendelea kuwa msingi wa utaalamu wa nyota hadi mwisho wa karne ya 16 na kazi za Nicolaus Kopernikus, Galileo Galilei na Johannes Kepler.

Baadaye skeli ya kale ilipanuliwa pande zote mbili kwa kupokea pia magimba angavu zaidi au hafifu zaidi. Kufuatana na ufafanuzi wa mwaka 1850 kiasi cha ungavu wa nyota ya daraja la kwanza (1.0 mag) ni mara 100 mwangaza wa nyota ya 6.0 mag, na hiyo mara 100 kuliko nyota ya 11.0 mag.

Mwanzoni nyota ya Kutubu (Polaris) ilifafanuliwa kuwa na mag +2. Baada ya kutambua ya kuwa Kutubu ni nyota badilifusasa ni Vega inayotumiwa kama nyota ya kurejelea yenye mag 0 (inaweza kuonekana angavu zaidi kidogo). Kuna nyota nne tu zinazoonekana angavu zaidi nazo ni Shira Shira ''(Sirius)'', Suheli (Canopus), Rijili Kantori (Rigil Kentaurus, α Cen) na Simaki (Arcturus)), Shira ina mag -1.46.

Mifano ya mwangaza unaoonekana

[hariri | hariri chanzo]
Kiwango cha juu cha mwangaza unaoonekana
wa magimba ya angani kadhaa
Jina Aina ya kiolwa Magnitudo
ya juu
iliyotazamiwa
Jua Nyota mag −26,73
Jua ikitazamiwa
kutoka
Neptuni
nyota mag −19,35
Mwezi mpevu Mwezi mag −12,73
Satelaiti ya Iridium satelaiti mag −9,00
ISS chombo cha angani mag −5,00
Zuhura (Venus) sayari mag −4,67
Mshtarii sayari mag −2,94
Mirihi sayari mag −2,91
Utaridi sayari mag −1,90
Shira (Sirius) nyota mag −1,46
Suheli (Canopus) nyota mag −0,73
Zohali sayari mag −0,47
Vega nyota mag 0,03[5]
Kutubu nyota mag 1,97
Galaksi ya Andromeda galaksi mag 3,40
Uranus sayari mag 5,50
1 Ceres sayari kibete mag 6,60
Neptuni sayari mag 7,80
Pluto sayari kibete mag 13,90
Eris sayari kibete mag 18,80
  1. Robert Bruce Thompson; Barbara Fritchman Thompson, Astronomy Hacks (Sebastopol, CA: O'Reilly, 2005), p. 88
  2. Rony De Laet, The Casual Sky Observer's Guide: Stargazing with Binoculars and Small Telescopes (New York: Springer, 2012), p. 29
  3. au parsec 10
  4. Leila Belkora, Minding the Heavens: The Story of our Discovery of the Milky Way (Bristol: Institute of Physics, 2003), pp. 19–20
  5. Imefafanuliwa kidesturi kama “0“ katika skeli ya mwangaza unaoonekana; hali halisi kuna tofauti ndogo