Nenda kwa yaliyomo

Shira (nyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa matumizi tofauti ya jina hili angalia Shira

Shira (Alpha Canis Majoris, Sirius)
Shira inaonekana kama nyota pacha katika picha hii iliyopigiwa na darubini ya angani Hubble.Shira A ni nyota kubwa, Shira B iko chini yake upande wa kushoto.
Kundinyota Mbwa Mkubwa (Canis Major)
Mwangaza unaonekana -1.46
Kundi la spektra A0 mA1
Paralaksi (mas) 379.21 ± 1.58[2] mas
Umbali (miakanuru) 8.6
Mwangaza halisi 1.43 A – 11.43 B
Masi M☉ 2.12 A, 0.97 B
Nusukipenyo R☉ 1.7 A – 0.008 B
Mng’aro L☉ 25.4 A – 0.027 B
Jotoridi usoni wa nyota (K) 9900 A – 25193 B
Muda wa mzunguko siku 5.5
Majina mbadala α Canis Majoris (α CMa), 9 Canis Majoris (9 CMa), HD 48915, HR 2491, BD−16°1591, GJ 244, LHS 219, ADS 5423, LTT 2638, HIP 32349


Ramani ya Mbwa Mkubwa - Canis Major jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini

Shira (ing. na lat. Sirius si-ri-us, pia α Alpha Canis Majoris, kifupi Alpha CMa, α CMa) ni nyota angavu zadi katika kundinyota ya Mbwa Mkubwa (Canis Major). Ni pia nyota angavu kabisa kwenye anga ya usiku. Mwangaza unaoonekana ni -1.46 mag.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Shira ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [1]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema الشعرى اليمانية ash-shi’ra al-yamaniya ambalo linamaanisha “nyota inayoonyesha upande wa Yemen = Kusini”[2]. Hapa Waarabu wanatumia jina la utamaduni wao ingawa walitafsiri pia jina la Kigiriki Κύων Ki-on yaani mbwa waliokuta kwa Ptolemaio katika kitabu chake cha Almagesti. Hivyo kulikuwa zamani pia kwa Kiarabu jina la "nyota ya mbwa" kwa ajili ya Shira. Asili ya jina la Kiarabu الشعرى ash-shi'ra inaweza kutoka kwa Kigiriki Σείριος sei-ri-os inayomaanisha "ya kuchoma, moto sana". Wagiriki walitumia jina hili pamoja na "Nyota ya Mbwa" kwa sababu wakati ule nyota hii ilianza kuonekana vema kwenye anga ya asubuhi katika siku za joto kuu. Hapo kulitokea pia jina la "siku za mbwa" (ing. dog days) kwa ajili ya kipindi cha siku za joto katika lugha mbalimbali.[3]

Katika matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulichagua "Sirius"[4].

Tabia[hariri | hariri chanzo]

Shira - Sirius ina mwangaza unaoonekana wa -1.46 mag na mwangaza halisi ni 1.43. [5]. Ni nyota ya karibu na umbali wake na Dunia ni miakanuru 8.60 [6].

Shira si nyota 1 tu bali nyota maradufu. Tangu karne ya 19 inajulikana ya kwamba hapa kuna nyota kubwa inayoitwa sasa Sirius A pamoja na nyota ndogo Sirius B. Zote mbili zinashikamana zikizungukuka kitovu cha graviti cha pamoja (ing. barycenter). Vipimo vya mwendo wa Shira B vinaonyesha uwezekano wa kuwepo kwa nyota ndogo ya tatu lakini Shira C haikuthibitishwa bado.[7] Shira A na B zinazungukana kwa umbali kati ya vizio astronomia 8.2 na 31.5.

Masi ya Shira A ni M☉ 2.02 na nusukipenyo chake R☉ 1.711 (vizio vya kulinganisha na Jua letu) [8].

Masi ya Shira B ni M☉ 1.02 na nusukipenyo chake R☉ 0.0084.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

 1. ling. Knappert 1993
 2. Allen uk. 119 anataja jina asilia kuwa « Al Shi ra al Abur al Yamaniyyah, the Brightly Shining Star of Passage of Yemen, in the direction of which province it set.« 
 3. Leo hii kuonekana vile kwa Shira kumeshahamia kipindi cha siku 30 hivi tangu nyakati za kale kwa sababu mbili: a) mwendo wa nyota yenyewe katika anga la nje, b) Mzunguko wa kuinama wa mhimili wa Dunia inayobadilisha polepole pembe jinsi tunavyoona nyota.
 4. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017
 5. Bond &al, uk 4
 6. SIRIUS (Alpha Carinae), tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
 7. Benest-Duvent: Is Sirius a triple star?, Astronomy and Astrophysics, 299, 621-628 (1995), tovuti ya chuo Kikuu cha Harvard, iliangaliwa Novemba 2017
 8. Liebert &al, uk 4 kwa kurejea Holberg na Kervella

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 59 (online kwenye archive.org)
 • Bond, Howard E.; Schaefer, Gail H.; Gilliland, Ronald L.; Holberg, Jay B.; Mason, Brian D.; Lindenblad, Irving W.; Seitz-Mcleese, Miranda; Arnett, W. David; Demarque, Pierre; Spada, Federico; Young, Patrick A.; Barstow, Martin A.; Burleigh, Matthew R.; Gudehus, Donald (2017). "The Sirius System and Its Astrophysical Puzzles: Hubble Space Telescope and Ground-based Astrometry". The Astrophysical Journal. 840 (2): 70, online hapa
 • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
 • Lane, Edward William: Arabic-English Lexicon (London: Willams & Norgate 1863), Book I, Part 4 س - ص, uk. 1560, online hapa
 • Liebert, J.; Young, P. A.; Arnett, D.; Holberg, J. B.; Williams, K. A. (2005). "The Age and Progenitor Mass of Sirius B". The Astrophysical Journal. 630 (1): L69–L72. online hapa

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]