Maraki
Kundinyota | Dubu Mkubwa (Ursa Major) |
Mwangaza unaonekana | 2.37 |
Kundi la spektra | A1 V |
Paralaksi (mas) | 40.9 |
Umbali (miakanuru) | 79.7 |
Mwangaza halisi | +0.61 |
Masi M☉ | 2.7 |
Nusukipenyo R☉ | 3 |
Mng’aro L☉ | 63 |
Jotoridi usoni wa nyota (K) | 9377 |
Majina mbadala | Mirak, 48 Ursae Majoris, BD+57°1302, FK5 416, GC 15145, HD 95418, HIP 53910, HR 4295, PPM 32912, SAO 27876 |
Maraki (lat. & ing. Merak pia β Beta Ursae Majoris, kifupi Beta UMa, β UMa) ni kati ya nyota angavu za kundinyota la Dubu Mkubwa (Ursa Major).
Jina
Maraki inayomaanisha "kiuno" (cha dubu) ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota[2]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema المراق al-maraq inayomaanisha "kiuno" (cha Dubu Mkubwa). Hivyo walitafsiri maelezo ya Ptolemaio katika Almagesti aliyeandika "(nyota) iliyo kiunoni"[3]
Kwa matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulikubali jina la Kiarabu na kuorodhesha nyota hii kwa tahajia ya "Merak" [4].
Beta Ursae Majoris ni jina la Bayer ingawa ni nyota angavu ya tano katika Dubu Mkubwa na Beta ni herufi ya pili katika Alfabeti ya Kigiriki basi Maraki ingepaswa kuitwa Epsilon. Ni mfano jinsi gani Bayer mara nyingi hakufuata mwangaza kikamilifu.
Tabia
Maraki iko katika umbali wa miakanuru karibu 80 kutoka Jua letu. Mwangaza unaoonekana ni mag 2.37.
Vipimo vya spektra vinaonyesha ya kwamba iko kwenye safu kuu ya nyota ikipangwa katika kundi la spektra A1 V.
Merak ni nyota nusu-jitu jeupe yenye masi mara 2.6, kipenyo mara 3 na mng’aro mara 70 ya Jua letu. Jotoridi kwenye uso wa nyota iko takriban nyuzi 9500 °K. Hii ni nyotabadilifu kwa kiasi kidogo, mwangaza wake unacheza kwa kiwango cha mag 0.05.
Kielekezo cha Nyota ya Ncha ya Kaskazini
Kwenye angakaskazi ya Dunia nyota hii ni moja kati ya mbili zinazosaidia kuikuta Kutubu (Polaris) ambayo ni nyota ya ncha ya kaskazini. Mtazamaji anaweza kufuata mstari wa kudhaniwa kati ya Dhahari ya Dubu (α UMa) na Maraki na kukuta nyota ya Kutubu kwa kuongeza umbali kati ya α UMa na β UMa mara tano.
Tanbihi
- ↑ vipimo kufuatana na Lyubimkov, Leonid S.; et al. (February 2010)
- ↑ ling. Knappert 1993
- ↑ Tooner (1984), Almagest , uk 342 na Heiberg (1903) uk.40
- ↑ Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017
Viungo vya Nje
- Constellation Guide:Ursa Major
- Ursa Major, kwenye tovuti ya Ian Ridpath, Star Tales, iliangaliwa Oktoba 2017
- Merak (Beta Ursae Majoris), kwenye tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017
Marejeo
- Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 437 (online kwenye archive.org)
- Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
- Ptolemy's Almagest, translated and annotated by G.J. Toomer, London 1984, ISBN 0-7156-1588-2 online hapa
- J.L. Heiberg: Claudii Ptolemaei opera quae extant omnia Vol. I, Syntaxis Mathematica, Pars II libros VII-XIII continens; Leipzig, Teubner 1903 (Maandiko yote yaliyopo ya Klaudio Ptolemaio)