Tahajia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Tahajia (kutoka neno la Kiarabu; pia othografia au orthografia kutoka neno la Kiingereza orthography ambalo lina asili ya Kigiriki) ni utaratibu wa kuandika maneno kwa namna inayokubalika kwa mujibu wa sheria, kanuni na mapatano ya lugha husika. Kila lugha huwa na kanuni na mapatano kuhusu jinsi ya kuandika maneno.

Sauti na herufi[hariri | hariri chanzo]

Tahajia inaeleza jinsi ya kutumia herufi za alfabeti kuandika sauti za lugha. Idadi ya sauti inazidi idadi ya herufi, kwa mfano Kiswahili ina sauti 36 [1] zinazoandikwa kwa kutumia herufi 26. Hapa herufi zinaweza kuunganishwa kwa kutaja sauti kama sh, ch, th, dh au ng'. Herufi nyingine zinataja zaidi ya sauti moja, kwa mfano vokali zote zinaweza kuonyesha sauti fupi au ndefu.

Umuhimu wa kusanifisha tahajia[hariri | hariri chanzo]

Matamshi ya maneno mengi ni tofauti kati ya wasemaji wa lugha fulani kutokana na lahaja au uzoefu wa maeneo au vikundi. Kama kila mtu anaandika jinsi anavyosikia mwenyewe matokeo ni magumu si rahisi kwa wengine kusoma matini haraka hadi kutoelewana kabisa. Kwa sababu hii taratibu ziliundwa kwa lugha zote kupatana kuhusu namna ya kuandika.

Kamusi za mwongozo[hariri | hariri chanzo]

Nchi nyingi huwa na taasisi ambako wataalamu hushughulika kazi hii na kutunga kamusi ambazo ni mwongozo kwa watumiaji wa lugha husika, hasa walimu, wanahabari na waandishi wa vitabu.

Mfano wa kuandika Kiswahili kabla ya usanifishaji[hariri | hariri chanzo]

Ukurasa wa kwanza wa tafsiri ya Krapf iliyochapishwa mwaka 1840.

Zamani Kiswahili kiliandikwa kwa herufi za Kiarabu ambako hapakuwa na utaratibu wowote: kila mwandishi aliandika jinsi alivyoona sawa; kwa hiyo matini za Kiswahili cha kale zinaonyesha tofauti kubwa katika tahajia.

Matini ya kwanza ya Kiswahili iliyoandikwa kwa herufi za Kilatini ilikuwa tafsiri ya Biblia ya Ludwig Krapf aliyeandika hivi akitumia utaratibu wa matamshi ya Kiingereza pamoja na msamiati wa lahaja ya Mombasa:

Keetoo-o dja quanza
Mooanzo alioomba Mooigniazimoongo oowingo na n'tee.

(soma: Kituo cha kwanza.

Mwanzo aliumba Mwenyezimungu uwingu na nchi.)[2]

Ni baadaye tu kwamba Krapf aliacha matamshi ya Kiingereza na kukaribia tahajia ya leo kwa kutumia matamshi ya Kijerumani. Katika miaka ya 1920/1930 kamati ya Inter-territorial Language (Swahili) committee iliweka misingi inayokubalika hadi leo kwa tahajia ya Kiswahili.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Kamusi ya Kiswahili Sanifu³, ilitolewa na Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili, Dar es Salaam 2014, uk. xvi
  2. Three chapters of Genesis, translated into the Sooaheele language, by the Rev. Dr. Krapf, Journal of the American Oriental Society, Vol.1; Boston 1849, p. 266, kwenye tovuti ya archive.org, iliangaliwa Septemba 2018

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tahajia kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.