Baraza la Kiswahili la Taifa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mwalimu wa somo la Kiswahili, Mussa Makange Shekinyasi - ambaye pia ni mwandishi wa riwaya yaDaladala kutoka Mbagala iliyotoka Agosti 1, 2020.

BAKITA ni kifupi cha Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania.

BAKITA ni chombo cha serikali chini ya wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.

Baraza hilo liliundwa na sheria ya bunge Na. 27 ya mwaka 1967 kwa shabaha ya kukuza, kuimarisha na kuendeleza Kiswahili hasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanyika mwaka 1983 kwa Sheria ya Bunge Na. 7, BAKITA imepewa uwezo wa kufuatilia na kusaidia ukuzaji wa Kiswahili katika nchi za nje pia.

Pamoja na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) cha Kenya na wawakilishi kutoka Uganda BAKITA imeunda Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki (BAKAMA).

Majukumu ya BAKITA

  1. Kukuza maendeleo ya matumizi ya lugha ya Kiswahili mahali pote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  2. Kushirikiana na vyombo vingine katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo vinahusika na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili na kuratibu kazi zao.
  3. Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli za Serikali na kwa shughuli za umma.
  4. Kuhimiza matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili na kuzuia upotoshaji wake.
  5. Kushirikiana na mamlaka yanayohusika katika kuanzisha tafsiri sanifu ya istilahi za Kiswahili.
  6. Kwa kushirikiana na vikundi vyovyote vya kimataifa, taasisi, au kundi la watu na watu binafsi, kufuatilia, kushauri na kuratibu shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili.
  7. Kuchunguza vitabu vya au maandishi yaliyoandikwa na kufasiriwa katika Kiswahili na kuhakikisha kwamba lugha iliyotumika ni sanifu na inakubaliwa na Baraza.
  8. Kutoa huduma za tafsiri kwa mashirika, idara, wizara, balozi na watu binafsi
  9. Kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ya Taifa kuthibitisha vitabu vya kiada vya Kiswahili kabla ya kuchapishwa, kwa ajili ya taasisi za elimu.
  10. Kuratibu na kutoa huduma za ukalimani kwenye mikutano ya kitaifa na ya kimataifa ndani na nje ya nchi.

Kamusi Kuu ya Kiswahili

Mwaka 2015 BAKITA ilifanikisha mradi wake wa kutunga kamusi mpya iliyoitwa Kamusi Kuu ya Kiswahili.[1]

Tanbihi

  1. Ed. Longhorn, Nairobi, Kampala, Dar es Salaam 2015.

Viungo vya nje