Amerigo Vespucci

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Amerigo Vespucci

Amerigo Vespucci (Firenze, Italia, 9 Machi 1451 - Sevilla, Hispania, 22 Februari 1512) alikuwa mfanyabiashara, nahodha na mpelelezi kwenye pwani za Amerika Kusini. Bara la Amerika limepokea jina kutoka kwake (Amerigo - Amerika).

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Mtoto wa tatu wa mwanasheria wa Firenze, Amerigo alifanya kazi kwa kampuni ya Medici akatumwa nayo mwaka 1491 kwenda Sevilla katika Hispania. Huko alikutana na Kolumbus amerudi kutoka Amerika.

Mwaka 1499 alichukua nafasi yeye mwenyewe na kibali cha akina Medici akajiunga na safari kwenda Amerika kufuata nyayo za safari ya tatu ya Kolumbus kwa kusudi la kugundua zaidi ya pwani. Mbele ya pwani ya Guyana (leo: Surinam) aliachana na wenzake akaendelea kusini akafika hadi mdomo wa mto Amazonas akiamini ya kwamba amefika Uhindi jinsi ilivyokuwa imani ya kawaida wakati ule.

Katika safari ya pili kwenda Amerika Kusini mwaka 1501 / 1502 alipita mwambao wa Brazil na Argentina hadi Patagonia. Aliporudi aliamini ya kwamba nchi ng'ambo ya Atlantiki si Asia bali "dunia mpya" au bara jipya. Maandiko yake yalisambaa kote Ulaya na mwanajiografia Mjerumani Martin Waldseemüller alitumia jina "Amerika" kwa heshima ya Amerigo alipochora ramani yake ya dunia mwaka 1507.

Upande wa dini, alikuwa Mkristo wa Kanisa Katoliki, tena mwanachama wa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko.