Surinam

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Republiek Suriname
Jamhuri ya Surinam
Bendera ya Surinam Nembo ya Surinam
Bendera Nembo
Wito la taifa: Kilatini: Justitia - Pietas - Fides
("Haki - Imani - Uaminifu")
Wimbo wa taifa: Opo kondreman
Lokeshen ya Surinam
Mji mkuu Paramaribo
5°50′ N 55°10′ W
Mji mkubwa nchini Paramaribo
Lugha rasmi Kiholanzi
Serikali Demokrasia
Dési Bouterse
Uhuru
Tarehe

25 Novemba 1975
Eneo
 - Jumla
 - Maji (%)
 
163,820 km² (ya 91)
1.10%
Idadi ya watu
 - Julai 2005 kadirio
 - 2004 sensa
 - Msongamano wa watu
 
449,000 (ya 170)
487,024
2.7/km² (ya 223)
Fedha Dollar ya Surinam (SRD)
Saa za eneo
 - Kiangazi (DST)
ART (UTC-3)
(haifuatwi) (UTC-3)
Intaneti TLD .sr
Kodi ya simu +597

-Ramani ya Surinam (maeneo yanayodaiwa na Surinam lakini kutawaliwa na majirani kwa rangi kijani-nyeupe)

Surinam ni nchi katika kaskazini ya Amerika Kusini. Imepakana na Guyana, Guyana ya Kifaransa na Brazil. Kuna pwani la bahari ya Atlantiki. Zamani za ukoloni ilijulikana kama "Guyana ya Kiholanzi". Mji mkuu ni Paramaribo.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Surinam ni nchi ndogo ya Amerika Kusini ikiwa na eneo la 163,820 km² pekee. Mlima wa juu ni Julianatop mwenye 1,280 m juu ya UB.

Kwa jumla kuna kanda mbili nchini:

  • kaskazini penye mashamba na idadi kubwa ya wakazi (takriban 20% ya eneo)
  • kusini penye misitu minene na savana lakini wakazi wachache (80% ya eneo)

Hali ya hewa ni kitropiki. Mvua hunyesha mara mbili kila mwaka: mvua mkubwa kati ya Aprili hadi Agosti na mvua mdogo kati ya Desemba hadi Februari. Usimbishaji ni kuanzia millimita 1,500 kwa mwaka karibu na pwani hadi millimita 3,000 katika kusini-mashariki ya nchi.

Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Wakazi wa Surinam ni wa asili mbalimbali kutokana na historia ya nchi.

Nyumba za zamani ya Uholanzi mjini Paramaribo.

Wenyeji asilia ni wachache sana kati ya 1-3% ya . Kuna Waindio wa makabila ya Waarawak, Wakaribi na wengine.

Wote wengine ni watoto wa wahamiaji waliofika wakati wa ukoloni.

Vikundi vikubwa ni:

Dini[hariri | hariri chanzo]

  • Wakristo ni 40,7 % (watu 200,744): Wakatoliki kati ya hao ni 22.8%, Waprotestant ni 25.2%. Kanisa kubwa la kiprotestant ni "Evangelische Broedergemeente in Suriname" (Kanisa la Moravian).
  • Wahindu ni 19,9 % (watu 98,240)
  • Waislamu ni 13,5 % (watu 66,307)
  • wafuasi wa dini za asili ni 5 %
  • Wayahudi ni 0,07 %

Lugha[hariri | hariri chanzo]

Lugha rasmi ni Kiholanzi inayotumika katika ofisi za serikali, bungeni na shuleni.

Pamoja na Kiholanzi kuna lugha ya kikreoli ya Sranan-Tongo inayotumiwa na sehemu kubwa ya wananchi, halafu Kihindi cha Sarnami, Kijava, lugha za kikreoli za Wabusinenge, lugha za Waindio na lahaja mbalimbali za Kichina na Kiarabu.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Wakazi asilia wa Surinam walikuwa Waindio hasa Waarawaki na Wakaribi waliokalia sehemu za pwani na savana.

Waindio, Wahispania na Waingereza[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1498 Kristoforo Kolumbus alipita mwambaoni aliyefuatwa 1499 na Amerigo Vespucci. Msafara wa upelelezi sehemu za bara ulifanywa na Wahispania mwaka 1500.

1651 Waingereza walijenga kituo cha kwanza cha kudumu kwenye mdomo wa mto Surinam (karibu na Nieuw Amsterdam wa leo) kilichotekwa na Waholanzi mwaka 1667. Kutokana na mkataba wa amani ya Breda wa mwaka uleule eneo hili lilibadilihswa na eneo la New York (Marekani) ya leo iliyowahi kukaliwa na Waholanzi.

Utawala wa Uholanzi[hariri | hariri chanzo]

Mtumwa apigwa kwenye shamba la miwa

Hivyo Surinam ya leo imekuwa koloni ya Uholanzi tangu 1667 kwa jina la "Guyana ya Kiholanzi". Wakati ule ilikuwa pamoja na Guayana (1815-1966: Guyana ya Kiingereza).

Waholanzi waliendeleza biashara ya mashamba makubwa ya miwa, pamba, kokoa na kahawa wakitumia kazi ya watumwa Waafrika.

Kati ya 1799 hadi 1815 Uholanzi ilivamiwa na Ufaransa na kutawaliwa kama sehemu ya himaya ya Napoleoni. Wakati ule Uingereza ilitwaa koloni za Uholanzi na kuzitawala. Baada ya Mkutano wa Vienna 1815 Surinam ilirudishwa lakini Guayana ya leo ilibaki kama koloni ya Guayana ya Kiingereza.

Kijiji cha Wabusinenge kwenye mto Surinam mnamo 1955

Utumwa na kutokea kwa Wabusinenge[hariri | hariri chanzo]

Kati ya Waafrika wengi waliolazimishwa kuwafanyia kazi mabwana wa mashamba makubwa wengine walifaulu kutoroka na kukimbia porini. Hapa porini walianzisha makazi yao na kuishi maisha huru. Katika Guyana waliitwa Wabusinenge au "Bosneger" ("weusi wa porini"). Walianzisha makabila mapya na kuchagua viongozi wao.

Historia yao ilianza baada ya Waingereza kuanzisha mashamba ya kwanza walipotumia kazi ya watumwa. Kuna taarifa ya 1690 ya kuwa kikosi cha weusi wa porini walishambulia shamba la mmoja Imanuel Machato kwenye mto Cassewijne, kumwua mwenyewe na kuondoka na watumwa wake. Waholanzi na pia Waingereza walijaribu mbinu mbalimbali kuwashinda wale weusi wa porini walioonekana na tishio kwa utaratibu wa utumwa na uchumi wa koloni. Lakini kuanzia mwaka 1749 Waholanzi walijaribu kupatana na Wabusinenge na 1760 ikawa na mkataba wa kwanza wa amani ambamo serikali ya koloni ilikubali uhuru wa kabila moja la Wabusinenge. Wale waliahidi kutopokea watumwa wapya wakimizi bali kuwarudisha kwa Waholanzi.

Katika koloni jirani ya Kiholanzi ya Berbice (leo: Guyana) kulitokea uasi mkubwa wa watumwa dhidi ya mabwana wao kuanzia tarehe 23 Februari 1763. Wazungu wote waliacha mashamba yao na kukimbilia mjini walipoweza kujitetea. Watumwa wengi waliondoka na kujificha porini baada ya kufika kwa wanajeshi Waholanzi waliokuja kukandamiza ghasia hii.

Mwisho wa utumwa na wafanyakazi kutoka Asia[hariri | hariri chanzo]

1 Julai 1863 Uholanzi ulifuta utumwa na watumwa 35,000 walipewa uhuru lakini walipaswa kuendelea kama wafanyakazi kwa muda wa miaka 10.

Baadaye wengi wao hawakutaka tena kufanya kazi mashambani. Hivyo wafanyakazi walitafutwa Uhindi, Uchina na katika koloni ya Uhindi ya Mashariki ya Kiholanzi (leo: Indonesia). Hao ni asili ya sehemu kubwa ya wakazi wa Surinam ya leo.

Uhuru[hariri | hariri chanzo]

1954 Surinam pamoja na Antili za Kiholanzi ilipewa madaraka ya kujitawala. Tangu 1973 kulikuwa na majadiliano kuhusu uhuru kamili uliopatikana tar. 25 Novemba 1975. Serikali za kwanza zuilikuwa na matatizo ya kisiasa. Wakazi wengi sana -jumla 1/3 ya wananchi- walihamia Uholanzi kwa hofu ya kwamba mambo yatakuwa mabaya.

Udikteta na vita ya wenyewe kwa wenyewe[hariri | hariri chanzo]

Baada ya miaka minne ya kwanza kulitokea mapinduzi ya kijeshi tarehe 25 Februari 1980. Serikali ya kijeshi iliongozwa na soli Desi Bouterse. Awali wananchi wengi na pia serikali ya Uholanzi walikubali watawala wapya. Lakini tangu 1982 mbinu za mabavu na unyama zilionekana kwa kuuawa kwa wapinzani mbalimbali.

1985 kikundi cha Wabusinenge chini ya Ronnie Brunswijk waliojiita "Jungle Comando" kilianza vita ya msituni dhidi ya serikali. Vita ilipiganiwa kwa ukali na unyama miaka miwili hadi shindikizo kutoka nchi za nje -hasa Uholanzi- lililazimisha serikali ya kukubali uchaguzi huru.

Uchaguzi wa Novemba 1987 ulileta ushindi wa vyama vya upinzani walioanzisha serikali mpya chini ya Ramsewak Shankar. Lakini Bouterse alifanya mapinduzi tena na kumwondoa Shankar madarakani tar. 24 Desemba 1990. Hali ya wasiwasi iliendela hadi uchaguzi mpya wa 1991 ulioleta serikali ya Ronald Venetiaan.

Agosti 1992 mkataba wa mani ulisainiwa na wapinzani wa "Jungle Comando" na kumaliza kipindi cha vita ya ndani.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Nchi na maeneo ya Amerika Kusini

Argentina | Bolivia | Brazil | Chile | Ekuador | Guyana | Guyana ya Kifaransa | Kolombia | Paraguay | Peru | Surinam | Uruguay | Venezuela

WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
South America.svg Makala hii kuhusu maeneo ya Amerika Kusini bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Surinam kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.