Wabusinenge

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kijiji cha Wabusinenge kwenye mto Surinam mnamo 1955

Wabusinenge (pia: kiholanzi: Bosneger (weusi wa porini), Maroon) ni neno katika kikreoli cha Surinam kwa ajili ya wakazi wenye asili ya Kiafrika ambao mababu yao walipelekwa Surinam kama watumwa lakini walikimbia na kuanza maisha huru porini mbali na mashamba ya mabawana wa zamani.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Kuanzia mwaka 1651 Waingereza walileta watumwa katika eneo la Surinam kama wafanyakazi kwenye mashamba ya miwa. Waholanzi walipochukua utawala wa sehemu hii ya "Guyana" waliendelea kujenga uchumi wa mashamba makubwa na kuingiza watumwa kutoka Afrika. Waafrika haya walitokea hasa kutoka Afrika ya Magharibi (Ghana, Togo, Benin, Dahomey) hadi Angola.

Waafrika wengine walifaulu kutoroka na kukimbia porini. Hapa porini walijenga makazi yao na kuishi maisha huru. Walianzisha makabila mapya na kuchagua viongozi wao. Makabila haya kwa kawaida yalitokana na ukoo wa mama aliyekumbukwa kuwa ametoka Afrika na kuzaa Amerika. Vikundi vikubwa ni: Wandyuka (pia: Aukani) na Wasaamaka. Wengine huitwa Paramaccani, Matawai, Aluku, Boni na Kwinti. Katika sensa ya Surinam ya mwaka 2004 wakazi 72,553 walijitaja katika kundi fulani ya Wabusinenge.

Historia yao ilianza baada ya Waingereza kuanzisha mashamba ya kwanza walipotumia kazi ya watumwa. Kuna taarifa ya 1690 ya kuwa kikosi cha weusi wa porini walishambulia shamba la mmoja Imanuel Machato kwenye mto Cassewijne, kumwua mwenyewe na kuondoka na watumwa wake. Waholanzi na pia Waingereza walijaribu mbinu mbalimbali kuwashinda wale weusi wa porini walioonekana na tishio kwa utaratibu wa utumwa na uchumi wa koloni. Lakini kuanzia mwaka 1749 Waholanzi walijaribu kupatana na Wabusinenge na 1760 ikawa na mkataba wa kwanza wa amani ambamo serikali ya koloni ilikubali uhuru wa kabila moja la Wabusinenge. Wale waliahidi kutopokea watumwa wapya wakimizi bali kuwarudisha kwa Waholanzi.

Katika koloni jirani ya Kiholanzi ya Berbice (leo: Guyana) kulitokea uasi mkubwa wa watumwa dhidi ya mabwana wao kuanzia tarehe 23 Februari 1763. Wazungu wote waliacha mashamba yao na kukimbilia mjini walipoweza kujitetea. Watumwa wengi waliondoka na kujificha porini baada ya kufika kwa wanajeshi Waholanzi waliokuja kukandamiza ghasia hii.

Kwa jumla Wabusinenge walifaulu kujipatia uhuri zaidi ya miaka 100 kabla ya Waholanzi kutangaza mwisho wa utumwa. Kutokana na maisha yao ya pori wameendeleza utamaduni tofauti na weusi walioendelea kuishi kwenye mashamba na mjini na kupewa uhuru tangu 1863. Hadi leo wanaonekana kama kikundi cha pekee katika Surinam. Utamaduni huu wa pekee ulikuwa pia tabia muhimu katika vita ya wenyewe kwa wenyewe katika Surinam mnamo mwaka 1985/1987 ambako Wabusinenge walikuwa na jeshi lao la pekee.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]