Johannes Hevelius

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Johannes Hevelius jinsi alivyochorwa na Daniel Schulz wa Danzig
Makumbusho ya Hevelius mjini Gdansk

Johannes Hevelius (16111687) alikuwa mwanaastronomia na mfanyabiashara Mjerumani[1] wa dola-mji Danzig (Gdansk) katika falme ya Poland.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa katika familia ya wafanyabiashara kwa jina la Johann Hewelcke akatumia kwa maandiko ya kitaalamu umbo la Kilatini la jina lake. Kwa Kipoland jina lake linatajwa kama Jan Heweliusz.

Akiwa mrithi wa biashara ya familia yake kupika bia aliendesha utafiti wa astronomia uliojenga sifa yake katika Ulaya wa wakati wake.

Alipata elimu ya hisabati na nyota kwake nyumbani akaendelea kusoma sheria na hisabati kwenye Chuo Kikuu cha Leyden (Uholanzi).

Baada ya kurudi aliendesha biashara ya bia ya familia yake na kujenga kituo cha kutazama nyota juu ya nyumba yake mjini Danzig. Vifaa vya upimaji vya nyota alivitengeneza mwenyewe. Alisisitiza kufanya vipimo vyake bila matumizi ya darubini kwa sababu alikuwa na mashaka juu ya ubora wa lenzi zilizopatikana[2]

Alichora atlasi ya Mwezi ("Selenographia" ya mwaka 1647) alipotunga ramani za kuonyesha sehemu nyingi za uso wa Mwezi. Majina kadhaa alizobuni yanatumiwa hadi leo, kwa mfano “Alpi za Mwezi”. Kasoko ya Hevelius ilipokea jina lake katika matumizi ya kimataifa.

Mwaka 1679 mwanastronomia Mwingereza Edmond Halley alimtembelea Danzig akiangalia nyota pamoja na Hevelius na kulinganisha vipimo. Halley alishangaa jinsi gani vipimo vya Hevelius aliyekataa matumizi ya darubini vililingana kabisa na vyake mwenyewe alivyochukua kwa njia ya kifaa hiki.

Baada ya kifo cha mke wake wa kwanza aliendelea na kazi ya nyota pamoja na mke wake wa pili Elisabeth Hevelius akatunga orodha ya nyota 1,564 iliyokuwa orodha kubwa ya wakati wake. Humo alibuni kundinyota mpya na saba kati ya hizi zinaendelea kutumiwa kati ya orodha ya kundinyota 88 za kisasa za Ukia. Hizi ni: Mbwa wawindaji (Canes Venatici), Mjusi (Lacerta), Simba Mdogo (Leo Minor), Pakamwitu (Lynx), Ngao (Scutum), Sudusi (Sextans) na Mbweha (Vulpecula). Orodha hii pamoja na atlasi ya nyota (Prodromus Astronomiae) zilitolewa mwaka 1690 na mke wake anayetazamiwa kuwa mwanastronomia wa kwanza wa kike anayejulikana.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Hevelius anatajwa mara nyingi kuwa Mpoland; alitoka katika familia wa raia Wajerumani wa mji wa Danzig iliyokuwa sehemu ya kujitawala wa Milki ya Poland-Lithuania. Idadi kubwa wa wakazi walikuwa Wajerumani kiutamaduni katika kipindi kile kabla ya kuanzishwa kwa utaifa wa baadaye. Linganisha tovuti ya Galileo Project
  2. Hevelius and the Firmamentum Sobiescianum, tovuti ya Ian Ridpath "Star Tales", iliangaliwa Oktoba 2017