Wingu Kubwa la Magellan

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Njia Nyeupe na Mawingu ya Magellan jinsi inavyoonekana katika jangwa la Atacama, Chile; nyota angavu ni Suheili

Wingu Kubwa la Magellan (ing. Large Magellanic Cloud, kifupi LMC) ni galaksi ndogo iliyo karibu na galaksi yetu ya Njia Nyeupe na sehemu ya kundi janibu letu. Inakadiriwa kuwa na nyota mnamo bilioni 10 - 15. Umbali wake na Dunia yetu ni takriban miaka ya nuru 160,000.

Kwenye usiku penye giza sana pasipo na ukungu hewani inaonekana kama wingu au doa kubwa linalong'aa. Inaonekana pamoja na doa jeupe la pili iliyo karibu linaloitwa Wingu Dogo la Magellan na kwa mpamoja hujulikana kama Mawingu ya Magellan.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Ilhali inaonekana vema kwenye anga ya nusutufe ya kusini kwa macho matupu mataifa na makabila mengi yana majina kwa ajili ya mawingu ya Magellan.

Jina la kimataifa latokana na nahodha na mpelelezi Mreno Ferdinand Magellan aliyekuwa mtu wa kwanza aliyeleta habari zake Ulaya.

Ushuhuda wa kwanza wa kimaandishi unaojulikana ni "Kitabu cha Nyota" cha Mwajemi Abd-al-Rahman Al Sufi aliyetaja "Ngombe Dume Mweupe" inayoonekana kwa Waarabu wa kusini ilhali wingu halikuonekana katika kaskazini ya Uarabuni[1].

Amerigo Vespucci aliyetembelea pwani za Amerika mnamo mwaka 1500 alitaja sehemu mbili angavu alizotazama kwenye anga la kusini na inaaminiwa ya kwamba alitaja hapa mawingu ya Magellan.

Maelezo ya kwanza yaliyoeleweka yalitolewa na Ferdinand Magellan aliyekuwa mtu wa kwanza wa kuzunguka Dunia yote katika safari ya miaka 1519 - 1522. Hapo alichora pia ramani za nyota na kufanya vipimo vya kwanza vya mawingu angavu vya anga yaliyopokea baadaye jina lake.

Tabia zake[hariri | hariri chanzo]

Wingu Kubwa la Magellan inaonekana katika eneo la kundinyota za Panji (Dorado) na Meza (Mesa) kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia. Haionekani kwa watazamaji wanaokaa upande wa latitudo ya 20° za kaskazini.

Zamani makadirio ya umbali wake yalitofautiana sana. Tangu mwaka 2013 umbali wa kitovu chake uliweza kupimwa kwa hakika kubwa kuwa parsek 49,970 (49.97 kpc)[2] au miaka ya nuru 162,902.

Masi ya Wingu Kubwa ya Magellan ni takriban sehemu ya kumi ya Njia Nyeupe (galaksi yetu). Kipenyo chake ni takriban miaka ya nuru 14,000 (Njia Nyeupe ni zaidi ya 100,000). Umbo lake halifuata muundo maalumu sana kama galaksi nyingi. Kuna mkusanyiko wa nyota na mata nyingi katika kitovu chake [3] na pia mkono mmoja tu mwenye umbo la parafujo[4] . Umbo lake ni dalili ya kwamba athira ya graviti ya Njia Nyeupe na Wingu Ndogo kwa pamoja zilivurugisha mfumo wa awali wa Wingu Kubwa ambao labda ilikuwa la parafujo.[5]

Wingu Kubwa inatembea kwenye anga la nje kwa kasi ya kilomita 378 katika kila sekunde, pamoja na Wingu Dogo lenye kasi ya 302 km/sec. Hapa wataalamu hawana uhakika kama mawingu yote mawili ni sehemu ya mfumo wa Njia Nyeupe zikishikwa na graviti yake na kuizunguka, au kama ni galaksi geni zinazopita tu karibu na Njia Nyeupe.[6]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Abd-al-Rahman Al Sufi , tovuti ya Messier Catalogue, iliangaliwa Oktoba 2017
  2. An eclipsing binary distance to the Large Magellanic Cloud accurate to 2 per cent, G. Pietrzynski et al. 7 Machi 2013 , tovuti ya European Southern Observatory, iliangaliwa Oktoba 2017
  3. A Cosmic Zoo in the Large Magellanic Cloud, tovuti ya European Southern Observatory, tar. 1 Juni 2010, iliangaliwa Oktoba 2017
  4. [linganisha http://adsabs.harvard.edu/full/1955AJ.....60..126D de Vaucouleurs, G. (1955), Diemsnsions and Structure of the Large Cloud], Astronomical Journal Vol 60, p 126ff, tovuti ya harvard.edu, iliangaliwa Oktoba 2017
  5. Besla. G. et al: "Low Surface Brightness Imaging of the Magellanic System: Imprints of Tidal Interactions between the Clouds in the Stellar Periphery", (2016). The Astrophysical Journal. 825 (1): 20, tovuti ya Institute of Physics IOP science publishing, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. Magellanic Clouds May Be Just Passing Through, tovuti ya Harvard-Smithsonian Center for Astrophysics, release Release No.: 2007-02 / January 9, 2007; iliangaliwa Oktoba 2017


Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]