Samaki (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Hutu (kundinyota))
Nyota kuu za Hutu (Pisces)
Mistari imeongezwa kwenye picha tu
Uchoraji wa nyota za Hutu - Pisces kama samaki wa angani (mtazamo kwenye nusutufe ya kaskazini)

Samaki (pia: Hutu) ni kundinyota ya zodiaki inayojulikana kimataifa kwa jina lake la kimagharibi la Pisces[1]. Ni moja ya makundinyota yanayotambuliwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2]

Nyota za Samaki huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Samaki" inaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Duniani.

Jina

Mabaharia Waswahili wamejua nyota hizi kwa jina la Hutu linalotokana na Kiarabu الحوت al-ḥuut ambalo linamaanisha "samaki". Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa Wagiriki wa Kale waliosema Ιχθύες ikhthies na majina yenye maana hiyohiyo ya "samaki" yalitumiwa pia na mataifa mengi ya kale.

Katika mitholojia ya Wagiriki nyota zake zilionyesha mungu wa kike wa mapenzi Aphrodite pamoja na mwanawe Eros waliokimbia dubwana Typhoni kwa kuruka katika mto Frati na kuchukua umbo la samaki. Ili wasipoteane kwenye maji walifunga kamba kati yao, na hapo asili ya jina la Kiarabu la nyota Alfa Piscium "Al-Risha" linalomaanisha "kamba" maanake kwenye picha iko mahali pa kamba inayounganisha samaki mbili.

Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Hutu" limesahauliwa badala yake tafsiri „samaki“ imekuwa jina la kawaida.

Mahali pake

Hutu iko angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Ndoo (pia DAlu, lat. Aquarius) upande wa magharibi na Kondoo (pia Hamali, lat. Aries) upande wa mashariki.

Magimba ya angani

Nyota angavu zaidi ni

  • Kullat Nunu[3] (Eta Piscium) yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.62 ukiwa umbali wa miakanuru 294 kutoka Dunia.
  • Alresha (pia Al Rescha) au Alfa Piscium yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.82 na umbali wa mwakanuru 139 kutoka dunia
Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
η 99 Kullat Nunu 3,62m 294 G7 IIIa
γ 6 3,70m 131 G9 III Fe-2
α 113 Alrescha 3,82 139 A0pSiSr + A3m
ω 28 4,03 106 F4 IV

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Pisces" (ambalo linaonyesha uwingi) katika lugha ya Kilatini ni "Piscium" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Piscium, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Kullat Nunu si jina rasmi la Ukia. Hii ilikuwa jina la nyota katika utamaduni wa Babeli

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 336 ff (online kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331

Viungo vya Nje

Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)

Kaa (Saratani – Cancer )Kondoo (Hamali – Aries )Mapacha (Jauza – Gemini )Mashuke (Nadhifa – Virgo )Mbuzi (Jadi – Capricornus )MizaniLibra )Mshale (Kausi – Sagittarius )Ndoo (Dalu – Aquarius )Nge (Akarabu – Scorpius )Ng'ombe (Tauri – Taurus )Samaki (Hutu – Pisces )Simba (Asadi – Leo )