Jauza (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Nyota kuu za Jauza (Gemini) jinsi zinavyoonekana angani.
Mistari imeongezwa kwenye picha tu
Gemini iliyochorwa na msanii wa Uingereza mnamo mwaka 1825
Namna ya kuunganisha nyota kuu za Jauza kwa kuonyesha mapacha wanaoshikana kwa mikono
Sanamu ya Castor na Pollux kufuatana na mitholojia ya Kigiriki

Jauza ni kundinyota ya zodiaki inayojulikana pia kwa jina lake la kimagharibi la Gemini[1]. Ni moja ya kundinyota zinazotambuliwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [2]

Jina[hariri | hariri chanzo]

Jina la Kiswahili ni Jauza na linatokana na Kiarabu جوزاءا jauza linalomaanisha mapacha. Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa Wagiriki wa Kale waliosema Δίδυμοι didimoi kwa maana hiyohiyo na hao walipokea kundinyota hii tayari kutoka Babeli.

Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Jauza" limesahauliwa ikiwa kundinyota inaitwa kwa tafsiri tu "Mapacha".

Mahali pake[hariri | hariri chanzo]

Jauza iko angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Thauri (Taurus) upande wa magharibi na Saratani (Cancer) upande wa mashariki.

Magimba ya angani[hariri | hariri chanzo]

Nyota za Jauza huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Jauza" inaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Duniani.

Kuna nyota 85 katika eneo la kundinyota hii [3] na kuna mbili hasa zinazoonekaka vizuri kwa macho matupu zikikaa karibu na kuwa msingi wa jina la kundi ambazo zinaitwa Castor na Pollux kwa majina ya Kigiriki zilizotazamiwa na watu wa kale kama mapacha mawili. Nyota angavu zaidi ni Pollux inayofuatwa na Castor. Johann Bayer aliona kwa kosa kinyume hivyo aliandikisha majina ya Alfa Gemininis kwa Castor na Beta Geminis kwa Pollux katika orodha yake.

 • Castor (Alfa Geminis) inaonekana kwa darubini kama mfumo wa nyota 6 zinazoonekana kw macho kama nyota 1 tu. Ina umbali wa miaka ya nuru 52 kutoka dunia. Uangavu unaoonekana ni 1.6.
 • Pollux (Beta Geminis) ni nyota jitu jekundu yenye uangavu unaonekana wa .2 ikiwa na umbali wa miaka ya nuru 34 kutoka dunia. Pollux imegunduliwa kuwa na sayari ya nje inayoizunguka.

Mitholojia[hariri | hariri chanzo]

Katika elimu ya nyota ya Babeli nyota za Castor na Pollux zilijulikana kama "Mapacha Makubwa". Zilitazamiwa kuwa miungu miwili kwa jina la Meshlamtaea na Lugalirra[4]

Katika Mitholojia ya Kigiriki kundinyota hii ya Jauza (Gemini) iliunganishwa na masimulizi ya Castor na Pollux waliokuwa wana wa Leda. Pollux alikuwa mwana wa mungu mkuu Zeus aliyemtongoza Leda ilhali Castor alikuwa mwana wa Tyndareus mfalme wa Sparta na mumewe Leda. Castor na Pollux waliabudiwa kama wasaidizi wa mabaharia. [5]. Castor alikufa lakini Pollux akiwa mwana wa mungu aliishi ilele akamwomba Zeus kumpa kaka nafasi hiyohiyo. Zeus aliitikia kwa kuwaweka wote wawili kama nyota kwenye anga.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

 1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Gemini" katika lugha ya Kilatini ni "Geminis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Geminis, nk.
 2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
 3. The geography of the heavens and class book of astronomy by Elijah H. Burritt kupitia google books, iliangaliwa Julai 2017
 4. Babylonian Star-lore by Gavin White, Solaria Pubs, 2008, page 125
 5. Ridpath, Ian; Tirion, Wil (2001), Stars and Planets Guide, Princeton University Press, ISBN 0-691-08913-2, uk 150 - 152

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 • Levy, David H. (2005). Deep Sky Objects. Prometheus Books. ISBN 1-59102-361-0. 
 • H. A. Rey, The Stars — A New Way To See Them. Enlarged World-Wide Edition. Houghton Mifflin, Boston, 1997. ISBN 0-395-24830-2.
 • Ridpath, Ian; Tirion, Wil (2001), Stars and Planets Guide, Princeton University Press, ISBN 0-691-08913-2 
 • Ian Ridpath and Wil Tirion (2007). Stars and Planets Guide, Collins, London. ISBN 978-0-00-725120-9. Princeton University Press, Princeton. ISBN 978-0-691-13556-4.
 • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 413 ff (online kwenye archive.org)
 • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

 1. A Spring Sky Over Hirsau Abbey
 2. The Eskimo Nebula from Hubble
 3. The Medusa Nebula
 4. Open Star Clusters M35 and NGC 2158
 5. NGC 2266: Old Cluster in the NGC