Jitu jekundu
Jitu jekundu (kwa Kiingereza red giant) ni jina la nyota kubwa zinazoonekana kung'aa kwa rangi nyekundu. Mifano ni Dabarani (en:Aldebaran, jina la kisayansi Alfa Tauri) katika kundinyota ya Tauri na Ibuti la Jauza (en:Betelgeuse au Alfa Orionis) kwenye Jabari (en:Orion).
Wanaastronomia hufikiri ya kuwa karibu nyota zote zinapita kwenye ngazi ya jitu jekundu katika mwisho wa maisha yake yanayotazamiwa kufuata mageuzi ya nyota (en:stellar evolution).
Nyota hizi zina uangavu mkubwa kwa sababu zilipanuka na hivyo kuwa na uso mkubwa wa kung'aa. Si lazima masi yake iwe kubwa sana lakini masi hii ilipanuka kwenye mjao mpana zaidi. Upanuzi unasababisha kupoa kwa jotoridi kwenye uso wa nyota na hapa ni asili ya rangi nyekundu.
Katika maisha ya nyota hali ya jitu jekundu inatokea baada ya kumaliza sehemu kubwa ya hidrojeni kwenye kitovu cha nyota iliyobadilishwa tayari kuwa heli. Hapo kiini cha nyota kinajikaza kiasi na humo kuongeza jotoridi. Hii inasababisha hata hidrojeni ya tabaka za nje za nyota kuingia katika myeyungano nyuklia (nuclear fusion) na hapa nyota inapanuka na kuongeza uangavu.