Kimondo cha Mbozi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Majiranukta kwenye ramani: 9°06′28″S 33°02′14″E / 9.10778°S 33.03722°E / -9.10778; 33.03722Kimondo cha Mbozi

Kimondo cha Mbozi[1] ni kimondo ambacho kilianguka kutoka anga-nje karibu na mji wa Vwawa. Kinakadiriwa kuwa na uzito wa takriban tani 16, kilianguka katika kilima cha Mlenje, wilayani Mbozi katika mkoa wa Songwe, Tanzania.

Kipo kati ya vimondo vizito 10 vinavyojulikana duniani. Kina urefu wa mita 3.3, upana wa mita 1.63 na kimo cha mita 1.22.

Kina maumbile maalum tofauti na vimondo vingine vinavyopatikana ulimwenguni kwa kuwa hiki ni hasa cha chuma. Chuma ni 90.45%, nikeli 8,69%, sulfuri 0,01% na fosfori 0,11% ya masi yake. Ndani yake vipande vidogo vya silikati vinapatikana.[2]

Wenyeji wa eneo walijua kimondo hiki tangu muda mrefu; kilielezwa kisayansi mara ya kwanza mwaka 1930 na wakati ule hapakuwa na dalili za kasoko; kwa hiyo inawezekana ya kwamba ama kilifika kwenye uso wa Dunia kwa pembe butu sana na kuvingirika hadi kukaa au muda wa kugonga uso wa dunia ni mrefu sana hadi dalili zote za kasoko asilia zilipotea tayari kutokana na mmomonyoko.

Tanbihi

  1. Wakati mwingine kinatajwa kama "Mbosi meteorite" kwa kufuata tahajia ya Kijerumani ya jina la Mbozi
  2. [https://onlinelibrary.wiley.com/doi/abs/10.1111/j.1945-5100.1996.tb02036.x Edward J. OLSEN, Robert N. CLAYTON, Toshiko K. MAYEDA, Andrew M. DAVIS, Roy S. CLARKE Jr., John T. WASSON; Mbosi: An anomalous iron with unique silicate inclusions], jarida la Meteoritics & Planetary Science, Volume31, Issue5, September 1996

Viungo vya Nje

Astrowiki.PNG
Mradi wa Astronomia Makala hii imewahi kukaguliwa na kuboreshwa kwenye warsha ya pamoja ya Jenga Wikipedia ya Kiswahili, Wikimedia Community User Group Tanzania na ASSAT. Imepewa hali ya ulinzi. Tunaomba mapendekezo yote ya usahihisho na nyongeza zipelekwe kwanza kwenye ukurasa wa majadiliano