Nenda kwa yaliyomo

Tunguska

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Tunguska ni eneo kubwa la Siberia kati ya mito miwili inayoitwa Tunguska ya mawe na Tunguska ya chini ambalo liko kusini-mashariki mwa mkoa Krasnoyarsk Krai wa Urusi. Ni eneo lisilokaliwa na watu wengi. Imekuwa maarufu duniani kutokana na Tukio la Tunguska ambako asteroidi iliangukia na kusababisha uharibifu mwingi.

Tukio la Tunguska

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1908 ulitokea mlipuko mkubwa juu ya eneo la Tunguska unaoaminiwa kusababishwa na gimba kubwa kutoka anga-nje (kama kimondo kikubwa au asteroidi ndogo) lililoingia katika angahewa na kupasuka kilomita kadhaa juu ya Tunguska.

Mashahidi walitoa taarifa juu ya mlio mkubwa kama mfululizo wa milipuko au mapigo ya mabunduki kwa mbali mnamo saa 7.15 asubuhi tarehe 30 Juni 1908 (tarehe 17 Juni katika kalenda ya Juliasi). Watu wachache walisimulia ya kwamba walisikia milipuko mbalimbali. Katika eneo kubwa miti iliangushwa. Milango na madirisha ya nyumba katika kijiji cha Vanavara kilichokuwa na umbali wa kilomita 65 kutoka eneo la mlipuko vilivunjika.

Kwa umbali wa kilomita 500 mwako wa nuru na tetemeko zilihisiwa na abiria kwenye reli ya Siberia.

Hakuna uhakika kama watu walikufa kwa sababu wakazi pekee wa eneo hili walikuwa wawindaji wa kabila la Waevenki.

Taarifa ya kwanza la eneo lenyewe linapatikana kutokana msafara wa mwanasayansi Mrusi Leonid Kulik aliyekaribia Tunguska mwaka 1922; 1927 alifika hadi kiini cha uharibifu na 1938 picha zilipigwa kutoka eropleni. Alikuta ya kwamba miti ilianguka katika kanda ya upana wa 70 km na urefu wa 55 km jumla eneo la 2,150 km², eneo linalolingana na ukubwa wa wilaya ya Tanzania kama Muranga. Kitovu chake kilikuwa kanda la kilomita 8 lenye miti iliyochomwa na bila matawi ilhali ilisimama.

Hakuna kasoko lililoonekana na wataalamu wakati ule.

Maelezo mbalimbali

[hariri | hariri chanzo]

Leonid Kulik alikuwa mtaalamu wa kwanza aliyehisi ya kwamba uharibifu ilisaabishwa na mshtuko kutokana na kimondo kilichoingia katika angahewa ya dunia na kupashwa joto hali halafu kupasuka kilomita kadhaa juu ya uso wa ardhi.

Hadi leo wataalamu wengi wanakubali elezo hili ingawa kuna majadiliano kama gimba la Tunguska lilikuwa kimondo, nyotamkia au asteroidi. Tatizo la maelezo yote ni ukosefu wa vipande vinavyotazamiwa kuwa na asili ya kimondo. Kinyume chake nyotamkia kubwa inaweza kueleza kutokuwepo kwa vipande kwa sababu inafanywa na barafu na vumbi tu lakini wengi hawaamini ya kwamba ingeweza kufikia karibu na uso wa ardhi vile bila kuyeyuka tayari katika kimo kikubwa.

Mwaka 2007 wanasayansi kutoka Italia walichungulia ziwa lililopo katika Tunguska wakaamini ya kwamba ziwa hili linajaza kasoko lililosababishwa na kipande cha gimba la Tunguska ingawa wataalamu wengine wana mashaka.

Wanasayansi wachache Warusi na Wajerumani waliunda nadharia ya kwamba sababu ya uharibufu ilikuwa tukio kutoka ndani ya ardhi ambako kiputo kikubwa cha gesi asilia ndani ya la ardhi kilipasuka na kutoka ghafla hewani ilipowaka kilomita kadhaa juu ya ardhi.

Tunguska kama mfano wa hatari kutoka anga-nje

[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu wengi wanaotazama gimba la Tunguska kama gimba la angani wanatumia uharibifu uliosababishwa nalo kama mfano wa hatari kutoka anga-nje. Tunguska haikupata vifo vingi vya wanadamu mwaka 1908 kwa sababu ilikuwa eneo tupu bila makazi ya watu. Lakini kama gimba la Tunguska lingeanguka juu ya mji mkubwa idadi ya wafu ingeweza kufikia malakhi au hata mamilioni ya watu. Tena astronomia imegundua ya kwamba kuna magimba mengi na makubwa zaidi yanayozunguka Jua. Inajulikana ya kwamba yale magimba makubwa yanaweza kuvutwa na graviti ya dunia na kuanguka hapa. Kasoko kubwa sana zimetazamiwa duniani na pia kwenye sayari nyingine zilizosababishwa na mapigo ya vimondo na asteroidi. Sayansi imekadiria ya kwamba nishati ya mapigo yaliyosababsha kutokea kwa kasoko hizi kubwa inapita nguvu ya mabomu makubwa ya kinyuklia.

Hapa mataifa ya dunia yameanza majadiliano juu ya ushirikiano wa kutambua magimba ya angani yanayolenga Dunia yetu na kuandaa mbinu za kuzizuia kwa mfano kwa kupeleka mabomu katika anga-nje na kuyapasua mbali na Dunia au kuyalenga upande mwingine.

Siku ya asteroidi ilianza kukumbukwa duniani tangu mwaka 2014 kwenye tarehe ya Juni 30, tarehe ya anguko la asteroidi ya Tunguska kwenye 30 Juni 1908.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]