Kreta ya Chicxulub
Kreta ya Chicxulub (tamka chik-shulub) ni kreta kubwa kwenye pwani ya rasi ya Yucatan (Meksiko) iliyosababishwa na pigo la asteroidi miaka milioni 66 iliyopita. Inaaminiwa ya kwamba tukio hilo lilisababisha kuangamia kwa dinosauri pamoja na spishi nyingine nyingi Duniani.
Kreta hii ina kipenyo cha zaidi ya km 180, hivyo ni kreta kubwa ya tatu duniani iliyosababishwa na pigo la asteroidi (en:impact crater) [2] Asteroidi iliyogonga huko ilikuwa na kipenyo cha angalau km 10. Pigo hilo lilisababisha tsunami, kuwaka kwa moto katika sehemu nyingi za Dunia, matetemeko ya ardhi na kulipuka kwa volkeno nyingi. Kutokana na vumbi na majivu yaliyorushwa angani nuru ya jua ilizuiliwa na hivyo kilitokea kipindi kirefu cha giza na baridi kali kote duniani.[3]
Kreta haionekani tena kwa macho au kutoka ndege maana mmomonyoko kwenye uso wa ardhi umeshasawazisha milima na kufukia shimo. Lakini vipimo vinaonyesha mabadiliko katika miamba ya eneo hilo na mabadiliko katika uga wa graviti ya eneo hili yanayotokana na densiti kubwa ya miamba pale ambako pigo lilikandamiza mwamba. Umri wa mwamba ulipimwa na kukadiriwa kuwa takriban miaka milioni 65 - 66. Umri huo unalingana na kupotea ghafla kwa spishi nyingi kote duniani jinsi inavyoonekana katika mabaki ya kisukuku.[4][5]
Marejeo
- ↑ PIA03379: Shaded Relief with Height as Color, Yucatan Peninsula, Mexico. Shuttle Radar Topography Mission. NASA. Iliwekwa mnamo October 28, 2010.
- ↑ Earth Impact Data Base: [1]
- ↑ Climate model simulations of the effects of the asteroid impact at the end of the Cretaceous, Brugger, J., G. Feulner, and S. Petri (2017), Baby, it's cold outside: Climate model simulations of the effects of the asteroid impact at the end of the Cretaceous, Geophys. Res. Lett., 44, 419–427, doi:10.1002/2016GL072241.
- ↑ Schulte, Peter et al. (5 March 2010). "The Chicxulub Asteroid Impact and Mass Extinction at the Cretaceous-Paleogene Boundary". Science (AAAS) 327 (5970): 1214–1218. . . . http://www.sciencemag.org/cgi/content/abstract/327/5970/1214. Retrieved 5 March 2010.
- ↑ *Rincon, Paul. "Dinosaur extinction link to crater confirmed", BBC, 2010-03-04. Retrieved on 2010-03-05.