Ufahamu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kuielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi.

Ufahamu wa mtu waweza kupimwa katika kusikiliza jambo au katika kusoma.

Kusikiliza

Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe.

Mambo ya kuzingatia katika ufahamu wa kusikiliza

Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha:

  • Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa
  • Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza
  • Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa.

Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo:

  • Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema.
  • Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha hoja.
  • Msomaji anatakiwa kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumasidia kukumbuka hapo baadae.
  • Kuwa makini na ishara mbambali za mwili kama vile kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho. Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika mazungumzo.

Kusoma

Ni namna ya kuangalia maandishi na kuyasoma. Kuna aina tatu za kusoma:

  • 1. kusoma kimyakimya.
  • 2. kusoma kwa sauti.
  • 3. kusoma kwa burudani.

Kusoma kimyakimya

Katika usomaji huu, msomaji hufumba kinywa na kupitisha macho katika kila mstari harakaharaka. Macho hayo huunganisha neno lililotangulia na lile linalofuata. Ubongo wake huchambua mambo muimu yanayojitokeza, huku akiyahifadhi kichwani.

Mtu akijizoeza kusoma kimya, ananufaika ifuatavyo:

  • Hupata nafasi ya kupima mwendo wake na kiasi cha welewa
  • Hujiepusha na lawama ya kusumbua wengine
  • Hukwepa kuzingatia kanuni za matamshi
  • Huweza kusoma maandishi mengi kuliko ambavyo angesoma kwa sauti

Kusoma kwa sauti

Kusoma kwa sauti ni namna ya kuyaangalia maandishi na kuyatamka kwa sauti inayosikika.

Mambo ya Kuzingatia katika Ufahamu wa Kusoma. Kuna vipengele viwili vinavyounda mchakato wa ufahamu wa kusoma:

Uelewa wa msamiati na Uelewa wa matini

Ili kuilelewa habari/matini ni lazima msomaji awe na uwezo wa kuelewa msamiati uliotumika katika matini hiyo. Endapo maneno yaliyotumika hayataeleweka vilevile matini yote haitaeleweka.

Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:

  • Kubaini mawazo makuu; msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatakiwa ajiulize, Je, kinachoongelewa hapa ni nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi kwake kuielewa habari hiyo.
  • Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi, kwa kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
  • Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
  • Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.

Kwa kuzingatia haya yote msomaji atakuwa na uelewa mzuri juu ya habari aliyoisoma na pia anaweza kufupisha habari hiyo aliyoisoma.

kusoma kwa burudani

Huu ni usomaji ambao lengo lake kuu huwa ni kujiburudisha tu. Katika usomaji wa aina hii, msomaji hujisomea zaidi magazeti, majarida na vitabu tofauti na vile vinavyotumika darasani.

Mambo ya Kuzingatiwa katika Ufahamu wa Kusoma kwa Burudani

Wakati mwingine si lazima msomaji awe na vitabu vyote ambavyo anahitaji kuvisoma au magazeti na majarida. Inapotokea hivyo, msomaji anaweza kwenda maktaba kuazima kitabu nachokihitaji.

Ingawa lengo la msomaji huwa ni kujiburudisha tu, lakini pia hujiongezea maarifa. Hii ni kwa sababu, magazeti, majarida na vitabu sambamba na kutuamia lugha sanifu huelezea mambo mabalimbali yanayoihusu jamii.

Hivyo msomaji kutokana na kusoma vitabu na majarida mbalimbali hujiongezea kiwango cha welewa wa lugha na mambo mengine ya kijamii yanayojadiliwa humo.

Ni jambo zuri kwa msomaji kujijengea tabia ya kujipima ili aweze kuelewa kiwango cha maarifa aliyopata katika kujisomea. Kujipima huku kunaweza kufanywa kwa kujiundia utaratibu wa kuweka kumbukumbu ya vitu au makala zilizosomwa na kufanya ufupisho wa kila makala.

Tazama pia

Viungo vya nje

Ufahamu Katika Shule Direct