Kambi ya Auschwitz
Kambi ya Auschwitz (tamka: aush-vits) ilikuwa idadi ya kambi za KZ zilizoanzishwa na serikali ya Ujerumani katika sehemu ya Poland iliyotawaliwa nayo tangu ushindi juu ya Poland katika mwanzo wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Kulikuwa na kambi tatu kubwa pamoja na kambi nyingi ndogo katika eneo lilelile:
- Auschwitz I ilikuwa kambi kuu yenye wafungwa kuanzia mwaka 1940 hadi 1945.
- Auschwitz II (Birkenau) ilikuwa kambi ya mauti kubwa iliyoendeshwa kwa kusudi la kutekeleza sehemu kubwa ya Maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya
- Auschwitz III (Monowitz) na kambi ndogo zilikuwa kambi za kazi ya kulazimishwa ambako hasa wafungwa Wapoland walipaswa kutekeleza kazi ya kiutumwa.
Kambi hizo zilikuwa karibu na mji wa Poland wa Oświęcim. Auschwitz ilikuwa jina la Kijerumani kwa "Oświęcim." Kambi zilitawaliwa na kikosi cha SS (Schutzstaffel)[1].
Haijulikani kikamilifu ni watu wangapi waliopelekwa katika kambi za Auschwitz, au ni wangapi waliokufa huko. Maana wakati ilipoonekana watashindwa, Wajerumani walijitahidi kuharibu kumbukumbu zote za kambi hizo. Wataalamu wa historia hukadiria kuwa kati ya miaka 1940 hadi 1945 angalau watu milioni 1.3 walitumwa Auschwitz, na milioni 1.1 waliuawa moja kwa moja au walikufa kwa njia nyingine kama njaa na magonjwa[2].
Wafungwa wengi waliotumwa Auschwitz waliteuliwa wauawe moja kwa moja. Kwa kawaida walifika kwa treni. Wakati wa kutoka pale kwenye kambi, maafisa wa SS walitenga watoto, asilimia kubwa ya wanawake na wazee wote na kuwapeleka moja kwa moja kwenye sehemu ya vyumba vya gesi ya sumu. Hapo waliambiwa wavue nguo na waingie ili waoge. Baada ya kuingia, milango ilifungwa na gesi ya sumu iliingizwa katika vyumba hivyo na kuua wote katika kipindi cha dakika 20 hivi. Wengine walioonekana wana uwezo wa kufanya kazi walipelekwa kwenye sehemu ya wafungwa na kupewa kazi. Ilhali walipata chakula kidogo mno, wengi walikuwa wagonjwa na kuuawa baadaye. Idadi ndogo walipelekwa kwenye viwanda vilivyoandaliwa karibu na kambi: katika kundi hilo wako walioweza kuishi hadi mwisho wa vita na ukombozi wao.
Mwisho wa kambi
[hariri | hariri chanzo]Kuanzia Oktoba 1944 Jeshi Jekundu la Urusi lilikuwa limeshaingia katika sehemu nyingi za Poland. Wafungwa wa mwisho walipelekwa kwenye kambi mwishoni mwa Oktoba. Katika Novemba 1944 Heinrich Himmler, mkuu wa SS, aliamuru kusitisha mauaji kwa njia ya gesi na kubomoa vyumba vya gesi, pamoja na tanuri za kuchoma maiti, kwa shabaha ya kuficha dalili za jinai zilizotekelezwa[3]; katika Januari 1945, wakati Jeshi Jekundu lilikaribia zaidi, wafungwa walilazimishwa kusafiri kwa miguu kutoka kambi bila chakula katika hali ya hewa baridi, mnamo 28.000 walifariki njiani au waliuawa na walinzi wa SS. Takriban 20,000 walifika kwenye vituo vya reli wakapelekwa katika kambi za KZ kwenye sehemu za magharibi za Ujerumani, hadi kukombolewa pale na wanajeshi wa mataifa ya ushirikiano[4]
Jeshi Jekundu lilifika Auschwitz tarehe 27 Januari 1945 likakuta wafungwa wapatao 7,000 walioachwa nyuma kwa sababu walikuwa wagonjwa mno kwa safari; wengi wao walikufa katika siku za kwanza baada ya ukombozi[5].
Ukombozi wa Auschwitz huadhimishwa kwenye Kumbukizi ya Kimataifa ya Maangamizi ya Wayahudi kwenye tarehe 27 Januari.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ https://encyclopedia.ushmm.org/content/en/article/auschwitz
- ↑ Auschwitz, Holocaust Encyclopedia, iliangaliwa Januari 2021
- ↑ Steinbacher, Sybille; Auschwitz: a History, London 2005; online hapa archive.org uk. 125–127
- ↑ "Auschwitz". www.ushmm.org (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2018-03-13.
- ↑ Steinbacher, uk 128
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Liberation of Auschwitz - 60th Anniversary Ilihifadhiwa 13 Juni 2006 kwenye Wayback Machine. (United States Holocaust Memorial Museum)
- Holocaust Encyclopedia - Auschwitz (United States Holocaust Memorial Museum)
- Virtual Reality panoramas of Auschwitz and Birkenau (Interactive Virtual Reality panoramas of Auschwitz and Birkenau)
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kambi ya Auschwitz kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |