Nenda kwa yaliyomo

Jeshi Jekundu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bendera ya Jeshi Jekundu
Leon Trotsky (wa tatu kutoka kushoto) alianzisha Jeshi Jekundu

Jeshi Jekundu (kwa Kirusi Красная армия Krasnaya armiya, kwa Kiingereza Red Army) lilikuwa jina la majeshi ya Umoja wa Kisovyeti tangu kuanzishwa kwake hadi mwaka 1946.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Asili ya jina hilo ni kipindi baada ya mapinduzi ya Urusi ya 1917 ambapo vikundi vilivyoongozwa na Wakomunisti viliitwa "Wekundu" wakipigana na wapinzani wao walioitwa "Weupe" katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Urusi. Chanzo cha jeshi hilo kilikuwa wanamgambo kutoka wafanyakazi wa viwandani, pamoja na askari kutoka vikosi vya Jeshi la Urusi vya wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Mwanasiasa mkomunisti Leon Trotsky alipanga vyanzo hivyo katika jeshi moja na kuanzisha Jeshi Jekundu. Tangu mwanzo chama cha Kikomunisti kililenga kusimamia Jeshi Jekundu kwa njia ya makamisaa wa siasa kwenye kila ngazi ya jeshi hilo.

Baada ya kushinda wapinzani "Weupe" wa ndani Jeshi Jekundu lilishindwa katika vita dhidi ya Poland mnamo 19191921.

Baada ya ushindi wa Wakomunisti jeshi lote la Urusi na Umoja wa Kisovyeti lilitwa "Jeshi Jekundu".

Kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia jeshi hilo liliathiriwa na takasa ya kisiasa, ambako majenerali wengi walishtakiwa kuwa wasaliti na kuuawa. Ukosefu wa viongozi bora ulionekana wakati wa mashambulio dhidi ya Ufini ya miaka 1939-1940 ambako Stalin alipaswa kukubali amani bila kufikia shabaha zake zote.

Wakati Umoja wa Kisovyeti ulishambuliwa na Ujerumani mwaka 1941, Jeshi Jekundu lilikuwa na matatizo makubwa kutetea nchi na uhaba wa viongozi wenye uzoefu umetajwa kama sababu mojawapo. Lakini kwa jitihada kubwa Jeshi Jekundu lilifaulu kusimamisha Jeshi la Ujerumani na kutetea mji mkuu Moscow na jiji kubwa la pili, Leningrad (leo: Sankt Peterburg). Baada ya kupokea msaada wa teknolojia kutoka Marekani, hali ya jeshi ilikuwa afadhali likafaulu kurudisha Wajerumani polepole hadi mwaka 1944, ambapo Marekani na Uingereza zilishambulia Wajerumani upande wa magharibi kwa uvamizi wa Ufaransa.

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia jina lilibadilishwa kuwa Jeshi la Kisovyeti (rus. Советская армия (СА)/sovjetskaya armiya).

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu: