Nenda kwa yaliyomo

Umimi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Umimi (kwa Kiingereza: "egoism") ni tabia ya kujijali kupita kiasi, bila kutia maanani vya kutosha watu wengine na jamii kwa jumla.

Ni kinyume cha ukarimu na unamfanya mtu azingatie mno kinachompendeza au kinachomfaidisha yeye, badala ya kulenga pia kinachowafaa wengine.[1][2]

Umimi unatazamwa kwa namna mbalimbali na dini, falsafa, elimunafsia, uchumi na fani nyingine.

Katika Ugiriki ya Kale[hariri | hariri chanzo]

Aristotle aliungana na wananchi wenzake wengi katika kulaumu wanaolenga faida yao wenyewe tu.[3]

Seneca alipendekeza watu wajistawishe lakini ndani ya jamii.[4]

Karne za Kati/Renaissance[hariri | hariri chanzo]

Dante Alighieri aliona umimi kama mzizi wa vilema vikuu vyote saba kwa jina la kiburi.[5]

Francis Bacon aliendeleza msimamo huo alipoandika, “Wisdom for a man's self...[a]s the wisdom of rats”.[6]

Ulimwengu wa kisasa[hariri | hariri chanzo]

Ubepari ulipoenea, Bernard Mandeville alisema maendeleo ya jamii na uchumi yanategemea umimi.[7]

Adam Smith alitumia mfano wa mkono usioonekana kusema mfumo wa uchumi unatumia umimi ili kuleta faida kubwa.[8]

Vilevile John Locke aliona jamii ijengwe juu ya mtu binafsi, halafu Ayn Rand alitetea umimi kama adili la kijamii ambalo ni mzizi wa maendeleo.[9]

Jacques Maritain alipinga hoja hizo kwa kukumbusha ile ya Aristotle kwamba binadamu ni kiumbe cha kijamii, hivyo anaweza kustawi kweli pande zote ikiwa tu analenga faida ya wengine.[10]

Katika Biblia[hariri | hariri chanzo]

Biblia ya Kikristo inaonyesha ugumu wa kuishi kwa uadilifu unatokana na hali tuliyorithi, yaani kuwa na madonda nafsini mwetu na kuishi katika mazingira maovu yaliyo chini ya shetani. Hayo yote yanatuelekeza kujipendea daima badala ya kumpenda Mungu kwanza na kuwapenda wenzetu kama tunavyojipenda. “Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu...” (Isa 6:5).

Maovu yanayotawala ulimwengu ni hasa kiburi na tamaa. Ni kwa kupitia umimi huo kwamba shetani anatawala watu. “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia... Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu, na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu” (1Yoh 2:15-16; 5:19).

Katika ulimwengu tunahitaji msimamo wa kutofuata mkondo wake. Kinyume chake, tuzingatie daima Baba anataka nini, Yesu Mwanae alifanya vipi na Roho Mtakatifu anatuelekeza njia gani. “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache” (Math 7:13-14). “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu” (Rom 12:1-2). “Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?” (Yoh 5:5).

Tunapokubali kufuata umimi wetu, tunazidi kuharibika na kuharibu jamii, tukistawisha utawala wa shetani badala ya ule wa Mungu: ndicho kinachomsikitisha Baba yetu mwema. “Alikuwa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu... ‘Huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana’” (Lk 15:16,24).

Basi, ili tusipotoshwe na umimi tunahitaji kujikana katika yote na kumfuata Yesu hadi upeo wa upendo. Hivyo hiari yetu itazidi kukombolewa. “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?” (Lk 9:23-25).

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. "Selfish", Merriam-Webster Dictionary, accessed on 23 August 2014
  2. Selfishness - meaning, reference.com, accessed on 23 April 2012
  3. Aristotle, Ethics (1976) p. 301-3
  4. G. Gutting ed., The Cambridge Companion to Foucault (2003) p. 138-30
  5. Dante, Purgatorio (1971) p. 65
  6. Francis Bacon, The Essays (1985) p. 131
  7. Mandeville, The Fable of the Bees (1970) p. 410 and p. 81-3
  8. M. Skousen, The Big Three in Economics (2007) p. 29
  9. P. L. Nevins, The Politics of Selfishness (2010) p. xii-iii
  10. Maritain, Jacques (1973). The Person and the Common Good. Notre Dame, IN: University of Notre Dame Press. ISBN 978-0268002046.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]