Maadili ya kiutu
Maadili bawaba |
---|
Maadili ya kiutu ni yale yanayotakiwa kupatikana katika binadamu yeyote ili aweze kutenda kwa uadilifu kadiri ya utu wake unaomtofautisha na wanyama, yaani hasa akili inayomwezesha kufikiria na kuelewa maana na matokeo ya matendo yake.
Kadiri ya wanafalsafa wa Ugiriki wa kale Plato na Aristotle, maadili hayo ni mengi (si chini ya 40), lakini yanategemea manne (maadili bawaba): busara, haki, nguvu na kiasi.
Katika Biblia ya Kikristo[hariri | hariri chanzo]
Katika Biblia, upendo unadai pamoja na imani na tumaini (maadili ya Kimungu), maadili ya kiutu, ambayo yote yanategemea manne ya msingi: busara, haki, nguvu na kiasi. “Huwafundisha watu kiasi, na ufahamu, na haki, na ushujaa; wala hakuna mambo ya kuwafaa zaidi kwa maisha” (Hek 8:7).
Maadili ya kiutu yanapatikana na kukua kwa juhudi za kutenda mema hadi kuzoea na kupata msimamo. Katika kufanya hivyo tunasaidiwa na neema ya Mungu. “Uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa... mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo” (2Pet 1:3,5-8).
Tunahitaji busara kwa sababu ndiyo adili linalotakiwa kuongoza utekelezaji wa mengine yote, kwa kuzingatia kila mara yaliyo mema kweli kwetu na kuchagua namna inayofaa kuyafikia. “Iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua” (Math 10:16). “Wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao” (Math 25:4). “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza’” (Lk 14:28-30).
Tunahitaji haki kwa sababu ndiyo msimamo wa kumpatia kila mmoja kile anachostahili. “Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula afanye vivyo hivyo... Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu” (Lk 3:11,14). “Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu” (Mk 12:17).
Tunahitaji nguvu kwa sababu ndiyo msimamo wa kutorudi nyuma mbele ya ugumu wa kutenda mema yanayotupasa. “Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Math 24:13).
Tunahitaji kiasi kwa sababu ndio msimamo wa kutumia vitu kadiri inayotufaa tu. Hasa ni muhimu kuwa na kiasi katika masuala ya jinsia. “Usizini. Wala usiibe... Wala usimtamani mke wa jirani yako... wala kitu chochote alicho nacho jirani yako” (Kumb 5:18-19,21). “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe” (1Kor 6:18).
Kati ya maadili mengine, Yesu alihimiza hasa upole na unyenyekevu, yanayotulinganisha naye kwa namna ya pekee. “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Math 11:29). “Mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Mk 10:43-45).
[hariri | hariri chanzo]
Maadili ya kiutu yanainuka katikati ya pande mbili tofauti, ambazo mmoja umezidisha na mmoja una upungufu. Kwa mfano, adili la nguvu linainuka katikati ya woga (unaokimbia hatari bila ya sababu yenye msingi) na ushupavu (unaotaka kuvunjika kichwa bila ya sababu ya kutosha).
Lakini, ebu! Hiyo katikati isieleweke vibaya. Wanaopenda anasa na watu vuguvugu wanataka kusimama katikati si kwa kupenda uadilifu, bali kusudi waepe matatizo ya vilema vinavyopingana pande hizo mbili. Hao wanachanganya hiyo katikati na ule wastani ambao haupatikani kama kilele katikati ya vilema viwili vinavyopingana bali katikati ya uovu na uadilifu.
Wastani huo unakimbia uadilifu wa juu ukijisingizia kuwa “pengine yaliyo bora yanazuia yaliyo mema”, ukiwa na maana ya kwamba, eti! “Mara nyingi au daima yaliyo bora yanazuia yaliyo mema”.
Kumbe hiyo katikati halisi ya uadilifu haisimami tu kati ya vilema viwili vinavyopingana, bali inainuka juu ya upotovu wa pande hizo mbili tofauti: busara halisi iko juu ya upumbavu na ya ujanja; ukarimu uko juu ya uroho na ya ubadhirifu; adili la ibada liko juu ya kudharau dini na ya ushirikina.
Tena hiyo katikati inaelekea kuinuka zaidi na zaidi, pasipo kupotoka upande mmoja wala upande mwingine, kadiri uadilifu unavyokua, kwa kuwa inafuata kanuni ya juu na lengo la juu.
Maadili ya kiutu katika teolojia ya Kikatoliki[hariri | hariri chanzo]
Ili tuzielewe taratibu za muundo wa Kiroho, ni muhimu tujue vizuri maadili ya kiutu, yaliyo chini ya yale ya Kimungu. Jina linavyosema, ya kwanza, yanayopatikana kwa kurudiarudia vitendo vyake, yanajulikana na Wapagani pia kwa kuwa lengo lake linajulikana na akili. Baadhi ya vijana waliojitoa kwa Mungu hawayajali vya kutosha; kinyume chake wengine wenye umri mkubwa zaidi, kisha kutambua umuhimu wake hawajali tena vya kutosha maadili ya Kimungu, ambayo ni bora pasipo mfano, kwa kuwa ndiyo yanayotuunganisha na Mungu.
Basi tupande ngazi kwa ngazi hadi uadilifu unaopita maumbile. Tuone kwanza mtu mwenye dhambi ya mauti anavyoweza kuwa na maadili ya bandia, k.mf. kiasi cha mchoyo; yeye anakitekeleza si kwa kupenda uadilifu, bali kwa kupenda fedha. Vilevile akilipa madeni si kwa kutekeleza haki bali kwa kukwepa gharama za kesi.
Juu kuliko hayo maadili ya bandia, mtu mwenye dhambi ya mauti anaweza kuwa na maadili halisi ya kiutu aliyojipatia. Wako wengi wanaofuata kiasi ili kuishi akili inavyotaka, na kwa ajili hiyohiyo wanalipa madeni na kuwalea vizuri watoto wao. Lakini mtu akibaki katika dhambi ya mauti, ni dhaifu katika kutekeleza uadilifu, hata ule wa kiutu. Maadili yake hayana msimamo, kwa kuwa utashi wake haumuelekei Mungu: badala ya kumpenda kupita yote, anajipenda kuliko Mungu. Halafu, maadili mengine yanayotakiwa kuyasaidia hayo hayapo, hivyo yanakosa mshikamano. Anayeendesha gari la kukokotwa na farasi kadhaa, anahitaji kila mmojawao awe amezoea kazi hiyo: vilevile adili moja haliendi bila ya lingine; yote yanahusiana na kuongozwa na busara. Basi, ili maadili ya kiutu yawe imara ni lazima yashikamane, na hiyo inadai mtu asibaki katika dhambi ya mauti, bali utashi wake ulenge kuishi na Mungu; ni lazima ampende kuliko nafsi yake, jambo lisilowezekana pasipo neema ya utakaso. Akiipata tu, maadili yote yanaweza kushikamana na kuwa imara; nayo chini ya upendo yanakuwa chanzo cha matendo yanayostahili uzima wa milele.
Maadili ya Kimungu yanatuinua na kuturekebisha kuhusu lengo lipitalo maumbile na kuhusu njia zipitazo maumbile zinazoweza kulifikia. Bila ya hayo, maadili ya kiutu hayatoshi: kuna tofauti ya dhati kati ya kiasi walichokieleza Wapagani na kile cha Kikristo (k.mf. kati ya ufukara wa mwanafalsafa na ule wa Kiinjili), kwa sababu kanuni na lengo ni tofauti. Cha kwanza kinataka mtu ale tu kipimo cha wastani ili kufuata akili, kutodhuru afya au kufikiri vizuri. Kumbe kiasi cha Kikristo kinamtaka ajipatie chakula ili kuishi kama mtoto wa Mungu, akielekea uzima wa milele; hivyo kinadai maisha magumu zaidi: kinadai mtu autese mwili wake “na kuutumikisha” (1Kor 9:27), kusudi asiwe tu raia mwadilifu wa nchi yake, bali pia mwenyeji “pamoja na watakatifu” na mtu “wa nyumbani mwake Mungu” (Ef 2:19). Tofauti hiyohiyo ipo kati ya adili la ibada linalotakiwa kumpatia Muumba heshima anayostahili, na adili la ibada la Mkristo linalomtolea Mungu, asili ya neema, sadaka ya misa ipitayo maumbile. Kwa kuwa ni tofauti ya ngazi, aina ya kwanza inaweza kustawi mfululizo kwa kurudiarudia vitendo vyake, bila ya kufikia kiwango kidogo cha aina ya pili iliyoinuliwa na neema inayotia utakatifu.
Kinachoongoza maadili hayo mawili yenye jina lilelile ni tofauti: upande mmoja ni akili ya binadamu tu, upande wa pili ni imani iliyomiminwa na Mungu.
Ni malengo mawili tofauti na nia mbili tofauti, ambapo busara haijui nia zipitazo maumbile, ila ikiangaziwa na imani inakuja kuzijua kwa kujua ukuu usio na mipaka wa lengo letu, yaani kumuona Mungu; hapo inakuja kujua uovu wa dhambi ya mauti, thamani ya neema inayotia utakatifu na ya neema za msaada ambazo ziombwe kila siku, na hazina ya sakramenti zilizowekwa kwa faida yetu. Vilevile kuna tofauti kubwa kati ya utaratibu ulioelezwa na mwanafalsafa Aristotle na unyenyekevu wa Kikristo unaozitegemea kweli za imani. Kuna tofauti kubwa kati ya ubikira wa wanawake waliokabidhiwa kuchochea daima moto wa miungu, na ule wa Mkristo aliyejiweka wakfu mwili na moyo kwa Mungu ili kumfuata Yesu kikamilifu zaidi.
Upendo unapoturekebisha tulenge uzima wa milele, unarekebisha maadili pia kuhusu njia zipitazo maumbile za kufikia wokovu. Walioendelea Kiroho wanaongozwa zaidi na kwa namna wazi na hiyo nia ipitayo maumbile, kumbe nia ya kibinadamu ndiyo inayozidi kuwaongoza wengine. Katika dhambi ya mauti mtu anajipenda kuliko Mungu na kwa umimi anaelekea kutotimiza hata wajibu wa kiutu.
Maelekezo ya teolojia ya kiroho[hariri | hariri chanzo]
Hatimaye, tuzingatie Injili na walimu wa Kiroho walivyosisitiza baadhi ya maadili ya kiutu ambayo yanahusiana zaidi na Mungu na kulingana zaidi na maadili ya Kimungu: ibada na toba (zinazompatia Mungu heshima na malipizi anavyostahili), upole (ukiambatana na subira), usafi kamili (au ubikira) na unyenyekevu ambao ukituinamisha mbele ya Mungu unatuinua juu ya ufinyu wa moyo na ya kiburi na kutuelekeza tuzame katika mambo ya Mungu na kuungana naye. “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Math 11:29). Yesu tu, kwa jinsi alivyojengeka katika ukweli, aliweza kusema juu ya unyenyekevu wake pasipo kuupoteza papo hapo.
Maadili ya kiutu na yale ya Kimungu (ambayo yayaongoze ya kwanza) ni utendaji wa aina mbalimbali wenye kulingana vizuri ajabu, dhambi nyepesi isipokuja kuvuruga. Sehemu zote za muundo huo wa Kiroho zinakua pamoja kama vidole vya mkono mmoja. Kutokana na mshikamano uliopo maadili yote yanakua pamoja na upendo, hasa maadili ya kumiminiwa, kwa kuwa yale ya kujipatia pengine yanastawi kidogo zaidi yasipofanyiwa mazoezi. Hatuwezi kuwa na upendo mkubwa pasipo unyenyekevu mkubwa; ni kama tawi la juu la mti linalozidi kuinuka kadiri mzizi unavyozidi kupenya ardhi. Tunapaswa kukesha kitu chochote kisije kikaharibu ulinganifu huo, kama inavyowatokea wale ambao wanadumu katika neema inayotia utakatifu lakini wanajali elimudunia na mafungamano na watu kuliko ustawi wa imani, tumaini na upendo wa Mungu.
Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]
- Practice Virtues Daily for a More Extraordinary Life
- The Large Clickable List of Virtues at VirtueScience.com Archived 15 Aprili 2010 at the Wayback Machine.
- An overview of Aristotle's ethics, including an explanation and chart of virtues Archived 8 Mei 2009 at the Wayback Machine.
- Virtue Epistemology
- Virtue, a Catholic perspective
- Virtue, a Buddhist perspective
- Greek Virtue (quotations)
- Peterson & Seligman findings on virtues and strengths (landmark psychological study)
- Illustrated account of the images of the Virtues in the Thomas Jefferson Building, Library of Congress, Washington DC Archived 11 Oktoba 2016 at the Wayback Machine.
- The Science of Virtues Project at the University of Chicago Archived 10 Novemba 2008 at the Wayback Machine.