Utoto wa kiroho

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha halisi ya Mt. Teresa wa Mtoto Yesu, 1896.

Utoto wa kiroho ni njia ya maisha ya kiroho inayofundisha kufuata Injili ya Yesu kwa kujifanya wadogo.

Mwalimu bora wa njia hiyo ni Teresa wa Mtoto Yesu, aliyeiita njia ndogo[1].

Njia ya utoto wa Kiroho iliyofundishwa naye[2] inadhihirisha utume wake wa kulea binadamu wa wakati huu. Njia hiyo inafuata sifa njema za umbile la mtoto[3] na kulingana na mafundisho ya teolojia kuhusu neema inayotia utakatifu, maadili ya kumiminiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu.

Tutachimba hayo kwa kuzingatia sifa hizo za mtoto, sifa kuu za mtoto wa Mungu na tofauti zilizopo kati ya utoto wa Kiroho na ule wa kimaumbile. Hivyo tutaona mwanga mwingi kuhusu teolojia ya neema.

Sifa za kimaumbile za mtoto[hariri | hariri chanzo]

Mbali ya kasoro ndogondogo, mtoto kwa kawaida ni sahili na anafahamu udhaifu wake. Hasa kama amebatizwa na kulelewa Kikristo, unyofu unajitokeza ndani yake: anasema anavyowaza na anaeleza bila ya mizunguko anavyotaka, asiogope watu watasema nini; haigizi kwa ujanja bali anajionyesha alivyo. Halafu anafahamu udhaifu wake, kwa kuwa peke yake hawezi kitu, bali anawategemea wazazi na inampasa apokee vyote toka kwao; kujifahamu dhaifu ni aina ya unyenyekevu.

Ujuzi huo unaelekeza kutekeleza maadili ya Kimungu kwa dhati na usahili. Kwanza mtoto anaelekea kusadiki anayoambiwa na wazazi wanapomzungumzia Mungu na kumfundisha kusali. Anaelekea kuwatumainia wanapomfundisha kumtegemea Mungu kabla hajajifunza sala ya tumaini katika katekisimu na kuitumia asubuhi na jioni. Hatimaye mtoto anawapenda wazazi kwa moyo kwa kuwa anawawia vyote, na ikiwa hao ni Wakristo kweli wanaelekeza moyo huo mdogo kwa Mungu, kwa Yesu na kwa Mama yake.

Katika unyofu huo, katika ujuzi wa udhaifu wake na katika utekelezaji sahili wa maadili ya Kimungu mna kiini cha maisha ya Kiroho ya hali ya juu. Ndiyo sababu Yesu, alipotaka kuwafundisha mitume wake umuhimu wa unyenyekevu, alimuita mtoto katikati yao akasema, “Amin, nawaambia: Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Math 18:3). Nyakati hizi wengine wameona kutimia utabiri wa Papa Pius X, “Kutakuwa na watakatifu kati ya watoto” walioalikwa mapema kupokea ekaristi mara nyingi.

Kwa kawaida mtoto akifikia ubalehe, anapotewa na usahili wake na ujuzi wa udhaifu wake; anataka kujifanya mtu mzima kabla ya wakati, na ndani mwake vinaanza kujitokeza undumakuwili na kiburi. Akisifu maadili, si yale ya Kimungu, bali nguvu inayodhihirisha anavyoanza kukomaa, pamoja na busara fulani ambayo haitofautishi vizuri na ile ya bandia na inaweza ikawa ujanja tu wa kuficha kasoro.

Baadaye, magumu ya maisha yatamkumbusha udhaifu wake; pengine atagongana na utovu wa haki ambao utamuonyesha thamani ya adili hilo; atasikitikia ma[[singizio] na hivyo atavumbua thamani ya unyofu. Hatimaye, akiendelea kusali ataelewa maneno ya Bwan: “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yoh 15:5), na maana ya dhati ya Baba Yetu itadhihirika kwake kwa namna mpya. Atarudia sala hiyo ya utoto wake akitumia pengine dakika kumi kuisali mara moja kutoka kilindi cha moyo wake: hapo atakuwa ameona tena njia yake.

Maadili makuu ya mtoto wa Mungu[hariri | hariri chanzo]

Maadili hayo ni yale yanayokuza sifa za umbile la mtoto lakini si kasoro zake, tuwe tulivyo kadiri ya neema ipitayo maumbile, si kadiri ya kasoro zetu.

Kwanza mtoto wa Mungu anatakiwa kuwa sahili na mnyofu, kukwepa unafiki na uongo asijaribu kuonekana tofauti na alivyo. “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru” (Math 6:22). Maana yake, ikiwa mtazamo wa roho ni mnyofu, na nia ni nyofu, maisha yote yatajaa mwanga.

Mtoto wa Mungu anatakiwa kujitambua daima dhaifu na mhitaji, akikumbuka mfululizo kwamba Baba yetu ametuumba kwa hiari toka utovu wa vyote, na kwamba pasipo neema hatuwezi kufanya lolote kuelekea utakatifu na wokovu. Akikua katika unyenyekevu huo atazidi kusadiki Neno la Mungu kwa dhati, kuliko watoto wanavyosadiki maneno ya wazazi wao. Atakuwa na imani isiyoogopa watu na atakayojivunia kuwa nayo; mara nyingine imani hiyo itapenya mafumbo pasipo mifuatano ya mawazo; ataishi kulingana nayo na kuyaonja, akiyatazama kwa mshangao kama mtoto anavyomtazama machoni baba yake mpendwa. Akifuata njia hiyo, mtoto wa Mungu ataona tumaini lake likiimarika siku kwa siku na kugeuka kujiachilia katika mikono ya Baba ambayo ni kama lifti inayotuinua hadi kwake. Hatimaye, mtoto wa Mungu atampenda kila siku zaidi, kwa ajili yake mwenyewe, si kwa ajili ya fadhili zake, kama vile mtoto mwema anavyompenda mama yake kuliko mabembelezo anayompatia. Mtoto wa Mungu anampenda Baba katika majaribu kama katika furaha, naye wakati mgumu anakumbuka wajibu wa kumpenda kwa nguvu zote hata kwa roho yote na kuunganika naye mfululizo ili kumuabudu katika Roho na ukweli.

Jambo hilo la mwisho linathibitisha kuwa mara nyingi katika majaribu njia ya utoto inadai ushujaa, adili la nguvu pamoja na kipaji cha nguvu. Tunaliona hilo hasa mwishoni mwa maisha ya Teresa wa Mtoto Yesu, alipopitia usiku wa roho kwa imani ya ajabu akiwaombea wasiosadiki, kwa kujiachilia kikamilifu kwa upendo safi na wa nguvu uliomfikisha hadi muungano wa kutugeuza. Njia ya utoto ikieleweka hivyo inalinganisha maadili yanayoonekana kupingana: upole na nguvu, unyofu na busara. Katika ulimwengu unaoonekana kupotoka tunahitaji busara, lakini pia nguvu hata kufia dini kama mahali pengi katika karne XX: ili tuwe nazo ni lazima tuwe na vipaji vya shauri na nguvu, ambavyo ili tuwe navyo tuzidi kuwa wanyofu na watoto mbele ya Mungu na ya Mama Maria. Kadiri tunavyoacha kuwa watoto kwa watu, tunapaswa kuwa watoto kwa Mungu. Kutoka kwake tu tunaweza kupata nguvu na busara tunazozihitaji katika mapambano ya nyakati hizi. Njia ya utoto ikieleweka vizuri inalinganisha pia unyenyekevu halisi na hamu ya kuzama kwa upendo katika mafumbo ya wokovu, ambako si karama ya pekee kama njozi na fadhili nyingine za nje ambazo hazikupatikana katika maisha ya mtakatifu huyo [4].

Kinachotofautisha utoto wa kiroho na ule wa kimaumbile[hariri | hariri chanzo]

“Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu; lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima” (1Kor 14:20). Basi, tofauti ya kwanza kati ya aina hizo mbili za utoto ni ukomavu katika kupima mambo. Lakini ipo nyingine: kwamba upande wa maumbile, kadiri mtoto anavyokua anatakiwa kujitegemea, kwa sababu siku moja wazazi watamuacha peke yake. Kumbe upande wa neema, kadiri mtoto wa Mungu anavyokua anaelewa kuwa hataweza kamwe kujitegemea bali kumtegemea Mungu tu. Kadiri anavyokua anatakiwa kuishi kwa uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu, ambaye kwa vipaji vyake anafidia kasoro za maadili, hivi kwamba hatimaye mtu anatendewa na Mungu kuliko kutenda mwenyewe, na wakati uliopangwa ukifika ataingia tumboni mwa Baba ambamo ataona heri yake. Kijana akikua anawaacha wazazi ili kuanza maisha yake; kisha kufikia utu uzima hawategemei tena, bali anawategemeza. Kinyume chake mtoto wa Mungu akikua anazidi kumtegemea asitake tena kufanya chochote peke yake, pasipo miangaza na mashauri ya Baba yake. Hapo maisha yote yanakolezwa na sala: ndilo fungu bora ambalo hatanyang’anywa kamwe.

“Kubaki wadogo ni kujitambua si kitu, ni kutarajia yote toka kwa Mungu mwema, kama vile mtoto anavyotarajia yote toka kwa baba yake; ni kutohangaikia chochote, ni kutolenga faida. Hata kati ya mafukara, mpaka mtoto ni mdogo anapewa anavyovihitaji, lakini akishakua tu baba hataki tena kumlisha bure, hivyo anamuambia, ‘Sasa fanya kazi, unaweza kujitegemea’. Basi, ili nisiambiwe maneno hayo, sikutaka kamwe kukua, nikijiona siwezi kujitegemea katika kupata uzima wa milele mbinguni. Hivyo nimebaki daima mdogo, asiye na kazi nyingine isipokuwa kuchuma maua ya upendo na ya sadaka nimtolee Mungu mwema ili kumpendeza. Tena kuwa mdogo ni kutoamini kuwa maadili ninayoyatekeleza ni ya kwangu, kana kwamba naweza kitu, bali ni kukiri kuwa Mungu mwema anaweka hazina hiyo ya maadili mikononi mwa mtoto wake ili aitumie atakavyohitaji, ikibaki daima mali ya Mungu mwema” (Teresa wa Mtoto Yesu). Ndivyo ulivyosema mtaguso wa Trento, “Wema wa Mungu kwetu ni mkubwa hivyo hata atake zawadi zake zitugeukie stahili zetu”. Tunaweza kumtolea yale tu anayotupa; ila tunayoyapokea kama neema tunamtolea kama stahili, ibada, sala, fidia na shukrani. “Hatimaye kuwa wadogo ni kutokata tamaa kwa kasoro zetu, kwa sababu watoto wanaanguka mara nyingi, lakini ni wadogo hivi hata wasiweze kuumia sana” (Teresa wa Mtoto Yesu).

Katika mafundisho hayo, ya juu kuliko mifuatano yoyote ya mawazo ya kibinadamu, linang’aa hasa lile la neema ambalo mababu wa Kanisa na wanateolojia waliandika mengi juu yake, na ambalo humo limetekelezwa kwa usahili na udhati na mtu aliyekubali kuongozwa na Roho Mtakatifu hadi bandari ya wokovu. Wenye heri wanateolojia watakaoweza kuongoa watu wengi kama mtakatifu huyo alivyofanya! “Tuseme nini sisi wenye ndevu na udhaifu pamoja, tuliowaona wasichana kuingia ufalme wa mbinguni kwa upanga, wakati hasira inatushinda, kiburi kinatuvimbisha na uchu wa madaraka unatuvuruga?” (Gregori Mkuu). Hakika Teresa wa Mtoto Yesu ameelekeza njia nyofu inayofikisha juu sana.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. (Kifaransa) Thérèse de l'Enfant-Jésus (1985). Histoire d'une âme. Manuscrits autobiographiques. Paris: Cerf. pp. 236, 302. ISBN 2-20402076-1.  Kigezo:Access-date
  2. Cumming, Owen F. (2006). Prophets, Guardians, and Saints: Shapers of Modern Catholic History. Mahwah, N.J.: Paulist Press. ISBN 978-0-8091-4446-4. Retrieved 24 May 2013. 
  3. Therese found a passage from Proverbs that struck her with particular force: "Whosoever is a little one, let him come to me" (Proverbs 9:4). She was struck by another passage from the Book of Isaiah: "you shall be carried at the breasts, and upon the knees they shall caress you. As one whom the mother caresseth, so will I comfort you." (Isaiah 66:12–13
  4. In May 1897, Therese wrote to Father Adolphe Roulland, "My way is all confidence and love." To Maurice Bellière she wrote, "and I, with my way, will do more than you, so I hope that one day Jesus will make you walk by the same way as me." {{blockquote|Sometimes, when I read spiritual treatises in which perfection is shown with a thousand obstacles, surrounded by a crowd of illusions, my poor little mind quickly tires. I close the learned book which is breaking my head and drying up my heart, and I take up Holy Scripture. Then all seems luminous to me; a single word uncovers for my soul infinite horizons; perfection seems simple; I see that it is enough to recognize one's nothingness and to abandon oneself, like a child, into God's arms. Leaving to great souls, to great minds, the beautiful books I cannot understand, I rejoice to be little because only children, and those who are like them, will be admitted to the heavenly banquet.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Utoto wa kiroho kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.