Nenda kwa yaliyomo

Mizizi ya dhambi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hieronymus Bosch alivyochora Mizizi Saba ya Dhambi na Vikomo Vinne.
Vilema vikuu

Mizizi ya dhambi, au vilema vikuu au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za mababu wa Kanisa[1] katika maadili ya Ukristo yanahesabiwa kuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. [2]

Kwa kawaida inatajwa kuwa saba,[3] zote zikitokana na umimi usiozingatia ukweli.

Mizizi ya dhambi, yaani majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinifu, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyotusogeza zaidi mbali na Mungu na kututumbukiza katika makosa makubwa zaidi, k.mf. uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole, akiteleza kwenye mteremko.

Ni muhimu tutafiti kwanza asili yenyewe ya mizizi saba ya dhambi. Yote inatokana na kujipendea, yaani umimi unaotuzuia tusimpende Mungu kuliko yote. “Kujipendea ni chanzo cha kila dhambi” (Thoma wa Akwino). “Mapendo mawili yamejenga miji miwili: kujipenda hadi kumdharau Mungu kumejenga mji wa Babuloni; kumbe kumpenda Mungu hadi kujidharau kumejenga mji wa Mungu” (Augustino). Tunampa kisogo kwa sababu tu kwa kujipendea tunataka mambo kinyume na sheria yake. Basi, tunatakiwa kufisha hiyo asili ya dhambi zote ili tujipende kitakatifu: ndio tendo la pili la upendo, ambalo tunajipenda kwa ajili ya Mungu, ili kumtukuza sasa na milele. Mwenye dhambi ya mauti anajipenda kuliko yote, hata kuliko Mungu. Kumbe mwadilifu anampenda Mungu kuliko nafsi yake, halafu anapaswa kujipenda ndani ya Mungu na kwa ajili ya Mungu; anapaswa kuupenda mwili wake ili usaidie roho, badala ya kuzuia uhai wake wa juu; anapaswa kuipenda roho yake ili aishi milele kwa uzima wa Kimungu; anapaswa kupenda akili yake na utashi wake ili vizidi kuishi kwa mwanga na upendo wa Mungu.

Kujipendea ndio chanzo cha mambo yale matatu yanayotokeza wazi roho ya ulimwengu kuhusu mwili, mali na roho. Dhambi za mwili zinatia aibu kuliko zile za roho, kwa kuwa zinatushusha kwenye ngazi ya wanyama; lakini zile za roho (k.mf. kiburi), ambazo peke yake zinapatikana ndani ya mashetani, ni mbaya zaidi, kwa kuwa zinapingana na Mungu na kutusogeza mbali naye zaidi.

Tamaa za mwili ni kupenda pasipo utaratibu vitu vinavyofaa kudumisha uhai wetu binafsi na wa ubinadamu kwa jumla; pendo hilo lisiloratibiwa linasababisha utovu wa kiasi na uzinifu. Hivyo uchu unaweza ukawa mungu bandia na kutupofusha zaidi na zaidi.

Tamaa za macho ni kupenda pasipo utaratibu vile vinavyopendeza macho: umaridadi, utajiri, hasa pesa inayowezesha kujipatia chochote. Ndipo unapotokea uroho unaofanya hazina yetu iwe mungu wetu tukiiabudu na kuitolea sadaka muda, nguvu, familia, hata uzima wa milele.

Kiburi cha maisha ni kupenda pasipo utaratibu ukuu wetu, yale yote yanayoweza kutukuza, hata kama ni magumu. Anayefuata hicho kiburi, mwishowe anajiabudu kama shetani. Ndipo zinapoweza zikatokea aina zote za dhambi, halafu upotovu wa milele. Kiburi si mmojawapo tu kati ya mizizi ya dhambi, bali ni asili hasa ya vilema vinne vifuatavyo: majivuno, uzembe, kijicho na hasira. Majivuno ni kupenda pasipo utaratibu sifa na heshima. Uzembe unahuzunikia kazi ya kulenga utakatifu kwa sababu inadai juhudi na kujikana. Kijicho kinatufanya tusikitikie mema ya wenzetu, kwa kuwa yanaonekana kuzuia ukuu wetu. Hasira isiyoratibiwa (si ya haki) inatufanya tupinge kwa nguvu yale yasiyotupendeza. Vilema hivyo - hasa uzembe, kijicho na hasira - vinazaa huzuni mbaya inayogandamiza roho, kinyume cha amani na furaha zinazotokana na upendo.

Mbegu hizo zote za mauti tunapaswa kuzifisha, si kuziratibu tu: kwanza umimi, unaozaa hayo matatu yanayosababisha mizizi saba ya dhambi: “Kama mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi” (Rom 8:13). Ukweli huo unaonekana wazi katika maisha ya watakatifu, ambapo neema inakuja kutawala mielekeo yote ya umbile lililoanguka ili kuliponya na kulishirikisha uhai bora zaidi. Haja hiyo ni wazi kwa roho ya Kikristo, na utekelezaji wake wenye bidii unaandaa kutakaswa na Mungu kwa ndani zaidi ili kuangamiza viini vya kifo vilivyobaki bado katika hisi, akili na utashi.

Mizizi ya dhambi inaitwa hivyo kwa sababu ni vyanzo vya vilema vingine. Hivyo majivuno yanazaa ukaidi, majigambo, unafiki, ushindani, kupenda mapyamapya, ubishi. Hayo yanaweza yakafikisha kwenye maanguko mabaya zaidi na uasi wa dini. Uzembe au ukinaifu kuhusu mambo ya Kiroho unapingana moja kwa moja na upendo wa Mungu na kuzaa uovu wa moyo, kinyongo au ukali kwa jirani, kutotaka kuwajibika, kukata tamaa, usingizi wa roho, kusahau amri na kutafuta yaliyokatazwa. Wakiteleza kwenye mteremko huo wa kiburi, majivuno na uzembe, wengi wamepoteza wito wao. Kijicho kinazaa chuki, masengenyo, masingizio, furaha kwa mabaya yanayowapata wengine na huzuni kwa mafanikio yao. Utovu wa kiasi na uzinifu vinazaa upofu wa roho, ugumu wa moyo, kushikilia maisha haya hata kupotewa na tumaini la uzima wa milele, kujipendea hata kumchukia Mungu, hatimaye kutotubu wakati wa kufa.

Mara nyingi mizizi hiyo ni dhambi za mauti, ila ni nyepesi ikiwa jambo husika ni dogo au hiari inapolichagua si kamili. Inaweza kupatikana kwa namna ya chini, kama inavyowatokea wengi wenye dhambi za mauti, lakini inaweza pia kuwemo ndani ya watu wenye neema inayotia utakatifu kama namna za upotovu wa maisha ya Kiroho: k.mf. kiburi kuhusu maisha ya Kiroho kinatufanya tukwepe wanaotukosoa, hata kama wana haki na mamlaka ya kufanya hivyo, halafu tuwe na kinyongo nao; ulafi kuhusu maisha ya Kiroho unaweza ukatutamanisha faraja za kihisi katika sala, hata tuzitafute kuliko Mungu. Hiyo miwili pamoja inasababisha njozi bandia n.k.

Tofauti na maadili, vilema havishikamani, tena vingine havipatani: hivyo tunaweza kuwa na kimoja pasipo vingine. Hata hivyo tunapaswa kutekeleza maadili mengi, kama arubaini, ambayo karibu kila mojawapo ni kilele kati ya vilema viwili vinavyopingana. Tena, kasoro kadhaa zinafanana na maadili kwa namna fulani: basi, ni muhimu tuwe na upambanuzi ili kuvitofautisha, la sivyo katika kinanda cha maadili tutatoa noti zisizotakiwa, tukidhani uzembe ni unyenyekevu, ukali ni haki, udhaifu ni huruma.

Kujitafiti

[hariri | hariri chanzo]

Orodha hiyo ya matunda mabovu ya kujipendea inatuelekeza kujitafiti na kukubali upana wote wa ufishaji unaohitajika ili tuishi kwa dhati uzima halisi. Kwa kuwa ukweli wa miguso yetu haueleweki kwa urahisi, tunapaswa kujitafiti wa makini. Kazi hiyo, badala ya kuondoa mawazo yetu yasimuelekee Mungu, iturudishe kwake mfululizo. Tunapaswa kuomba mwanga wake ili tujione kidogo anavyotuona yeye au tutakavyojiona siku ya hukumu. Kila jioni tutafiti kwa unyenyekevu na majuto makosa tuliyoyafanya kwa mawazo, maneno, matendo na kutotimiza wajibu. Lakini tusizidishe kwa kutafuta makosa madogo mno hata tukahangaishwa na kusahaulishwa mambo muhimu zaidi. Lengo si kuorodhesha kikamilifu makosa, bali ni kuona kwa unyofu chanzo chake ndani mwetu. Ili kuponya upele, hatuwazi kuponya vijipu kimojakimoja, bali kusafisha damu. Tusisimame mno kujitazama hata tukaacha kumkazia macho Mungu, bali tujiulize mbele yake anatuonaje. Ndivyo tunavyoona masharti matakatifu ya dhamiri ya Kikristo, yanayopita yale ya mwanafalsafa yeyote. Tusitenganishe kamwe makosa na huruma isiyo na mipaka, bali tuyaone katika mwanga wa wema wa Mungu ulio tayari daima kusaidia. Hivyo utafiti hautasababisha tukate tamaa, bali utazidisha tumaini letu kwake.

Kuona makosa yetu kunatuonyesha pia thamani ya maadili yaliyo kinyume chake. Tunathamini haki hasa tunapoonja uchungu wa kukosewa haki. Ubaya wa uzinifu utuonyeshe thamani ya usafi wa moyo; vurugu za hasira na kijicho zitufanye tuthamini upole na upendo halisi; uharibifu unaotokana na uzembe uchochee ndani mwetu hamu ya juhudi na furaha ya Kiroho; upotovu wa kiburi ututambulishe hekima na ukuu wa unyenyekevu halisi.

Tumuombe Bwana atutie chuki takatifu kwa dhambi, kwa kuwa dhambi inatuondolea wema mkuu wa Mungu aliyetujaza fadhili za ajabu na anayetuahidia nyingine za thamani zaidi tukidumu kuwa waaminifu. Kwa namna fulani chuki hiyo ni upande wa pili wa upendo kwa Mungu. Haiwezekani kupenda ukweli pasipo kuchukia uongo, wala kumpenda Mungu pasipo kuchukia yanayotusogeza mbali naye. Watakatifu wanyenyekevu na wapole wana chuki takatifu kwa uovu iliyo na nguvu sawa na upendo wao kwa Mungu. Tujiombee chuki hiyo dhidi ya kiburi na vinginevyo ili upendo halisi kwa Mungu na kwa watu uzidi kustawi ndani mwetu. Njia ya kushinda kiburi ni kuzingatia mara nyingi Yesu alivyodhalilishwa, pamoja na kujiombea unyenyekevu. Ili kuzima kijicho tumuombee jirani yale tunayojitakia. Tujifunze pia kuzuia mara hasira ikipanda kwa kusogea mbali na kile kinachoisababisha, pamoja na kuzoea kutenda na kusema kwa upole. Ufishaji huo ni wa lazima. Ili tuendelee kuelekea ukamilifu, tufikirie malipizi ya watakatifu, tukizingatia kuwa sisi pia tunatakiwa kufia dhambi zaidi na zaidi kwa ustawi wa maadili yote, hasa upendo.

  1. Introduction to Paulist Press edition of John Climacus: The Ladder of Divine Ascent by Kallistos Ware, p63.
  2. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, n. 1866.
  3. Boyle, Marjorie O'Rourke (1997) [1997-10-23]. "Three: The Flying Serpent". Loyola's Acts: The Rhetoric of the Self. The New Historicism: Studies in Cultural Poetics,. Juz. la 36. Berkeley: University of California Press. ku. 100–146. ISBN 978-0-520-20937-4.
  • Refoule, F. (1967) Evagrius Ponticus. In Staff of Catholic University of America (Eds.) New Catholic Encyclopaedia. Volume 5, pp644–645. New York: McGrawHill.
  • Schumacher, Meinolf (2005): "Catalogues of Demons as Catalogues of Vices in Medieval German Literature: 'Des Teufels Netz' and the Alexander Romance by Ulrich von Etzenbach." In In the Garden of Evil: The Vices and Culture in the Middle Ages. Edited by Richard Newhauser, pp. 277–290. Toronto: Pontifical Institute of Mediaeval Studies.

Marejeo mengine

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.