Ufishaji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Joji na Joka ni mfano wa mapambano ya kiroho dhidi ya dhambi.

Ufishaji (kwa Kiingereza: mortification) ni juhudi za mtu za kumaliza dhambi katika maisha yake kwa kuondoa maovu yaliyomo moyoni mwake.

Katika Injili[hariri | hariri chanzo]

Yesu alijieleza kwamba hakuja duniani afanye kazi ya kibinadamu ya kusaidia watu, bali kazi ya Kimungu ya kuwapenda hadi kuangamia ili kuwaokoa. Yeye alifafanua haja ya kufia dhambi ili tupokee kwa wingi uzima mpya, akitoa mfano kwa kufa msalabani. Kufia dhambi na kuishi kwa hali ya juu ni mambo yanayokumbukwa daima pamoja, chini ya upendo wa Mungu. Mwinjili Luka ameandika wazi kuwa Yesu aliwaelekea “wote” aliposema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?” (Lk 9:23-25)[1].

Katika hotuba ya mlimani Yesu alionyesha haja ya ufishaji kwa kusisitiza ukuu wa lengo letu lipitalo maumbile: “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni… Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Math 5:20,48). Sababu ni kwamba Yesu ametuletea neema ambayo ni kushiriki uhai wa ndani wa Mungu, hivyo ni bora kuliko uhai wa kimaumbile hata wa malaika, lakini inadai ufishaji wa yale yote yasiyoratibiwa ndani mwetu. Bwana alisema wazi kuhusu ufishaji wa ndani na wa nje unaompasa Mkristo halisi na kuhusu roho ambayo iuongoze.

Tunatakiwa kuepa iwezekanavyo kinyongo na chuki moyoni: “Ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi” (Math 5:23-25). Tusimuone ni adui, bali ndugu, mtoto wa Mungu.

Tunapaswa kufisha tamaa: “Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe… Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe katika Jehanum” (Math 5:29-30). Bwana amesema kwa nguvu hivi kwamba watakatifu wanashauri kufunga, kukesha na kushika magumu mengine ambayo, yakitekelezwa kwa busara, utiifu na bidii, yanatumikisha mwili na kuhahikisha uhuru wa roho.

Tunapaswa kufisha hamu ya kulipa kisasi, “Mmesikia kwamba imenenwa: Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia: Msishindane na mtu mwovu” (Math 5:38-39). Yaani msilijibu tusi kwa ukali; mumkatalie hadi kuuawa anayetaka kuwakosesha, lakini mvumilie makosa yake bila chuki wala hasira. “Mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili” (Math 5:39). Yaani uwe tayari kukosewa haki kwa ustahimilivu; ndiyo subira inayoshinda hasira ya adui na pengine inamuongoa ilivyotokea katika dhuluma dhidi ya Kanisa. Ulenge kumpatia Mungu roho ya ndugu mwenye hasira kuliko kutetea haki zako za kidunia. Ndio ukuu wa haki ya Kikristo inayotakiwa kuendana daima na upendo. Haifai wakamilifu wagombane na watu wasipotakiwa kutetea tunu za juu zaidi.

Mwokozi anatudai tena tufishe umimi unaotufanya tumkwepe anayetaka kutuomba kitu (taz. Math 5:42), hukumu zisizo na msingi (taz. Math 7:1), kiburi cha roho na unafiki (taz. Math 6:1-16).

Hatimaye ametuonyesha roho ya ufishaji iwe ya namna gani: “Wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso, ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Math 6:17-18). Maana yake, jipake upendo, huruma na furaha ya Kiroho; takasa roho yako na elekeo lolote la kujionyesha. Ukitenda mema hukatazwi kuonekana, ila usijionyeshe, usitake kuonekana, la sivyo utapoteza usafi wa nia inayotakiwa kumuendea Baba moja kwa moja. Roho ya ufishaji ni upendo unaoangaza watu ili kuwaokoa: inawezekanaje kuwa wapole kwa mtu mkali bila kujitawala? Ni roho ya kumtolea Mungu tabu yoyote inayotupata isaidie kumkaribia na kuokoa watu, ili mambo yote yachangie kufanikisha wema, hata vizuio tunavyovikuta njiani, kama vile Yesu alivyofanya msalaba wake kuwa chombo bora cha wokovu.

Hivyo ufishaji wa Kikristo uko juu kuliko uzembe wa fikra za kidunia [2] na kuliko maisha yaliyo magumu kwa kiburi [3]. Ndio ufishaji tunaouona katika watu wenye sura ya Yesu msulubiwa: Mungu ni wa ajabu katika watakatifu wake!

Kadiri ya Mtume Paulo na teolojia ya Kikatoliki [4][hariri | hariri chanzo]

Mafundisho ya Injili kuhusu ufishaji yamefafanuliwa na Mtume Paulo aliyesema, “Nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa” (1Kor 9:27). Zaidi ya kutamka haja hiyo, yeye ametuonyesha ni lazima tufishe yale yote yasiyoratibiwa ndani mwetu kwa sababu ya: 1) matokeo ya dhambi asili; 2) matokeo ya dhambi zetu binafsi; 3) ukuu usio na mipaka wa lengo letu lipitalo maumbile; 4) wajibu wetu wa kumfuata Bwana msulubiwa.

Kwa kuzingatia sababu hizo, zinazokanushwa na fikra za kidunia, ufishaji wa ndani na wa nje unaeleweka ni nini. Unahusiana na maadili mengi, kwa sababu kila moja linapingana na vilema vilivyo kinyume chake, na kwa namna ya pekee unahusiana na adili la toba, ambalo linalenga kuangamiza ndani mwetu matokeo ya dhambi kwa sababu ni chukizo kwa Mungu, na ambalo linatakiwa litokane na upendo wake.

Matokeo ya dhambi asili[hariri | hariri chanzo]

Kwanza Mtume Paulo alimlinganisha Yesu Kristo, asili ya wokovu wetu, na Adamu, asili ya uharibifu wetu: “Kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti… Kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki… na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi… kwa Yesu Kristo Bwana wetu” (Rom 5:12,19-21).

Kifo ni mojawapo kati ya matokeo ya dhambi asili, lakini Paulo alitaja pia tabia mbovu ya “utu wa kale”, yaani utu jinsi ulivyozaliwa na Adamu, wenye umbile lililoanguka na kujeruhiwa. “Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho na nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli” (Ef 4:22-24). “Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba” (Kol 3:9-10). “Naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani; lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” (Rom 7:22-24).

Utu wa kale unakosa ule ulinganifu mzuri wa uadilifu asili ulioangamizwa na dhambi. Mtaguso wa Trento umetamka kwamba mtu wa kwanza kwa kosa lake “amepoteza kwake na kwetu utakatifu na uadilifu asili” na kuturithisha umbile lisilo na neema, tena lililojeruhiwa. Pasipo kuzidisha ubaya wa hali hiyo, tukiri tumezaliwa hali utashi wetu haumuelekei Mungu bali uovu; akili yetu inaelekea udanganyifu; hisi zetu zinaelekea anasa na hasira, vyanzo vya dhambi za kila aina. Ndipo vinapotokea kiburi, kumsahau Mungu, umimi wa namna nyingi ambao haujitambui na unataka raha duniani, badala ya kulenga juu zaidi. “Ubinadamu unajifanya daima lengo lake wenyewe, kumbe neema… inafanya yote kwa ajili ya Mungu tu” [5].

Utu ulioanguka, si tu kwamba umevuliwa neema na fadhili za asili, bali umejeruhiwa katika umbile lake. Hasa ni kwa sababu tumezaliwa hali utashi wetu haumuelekei Mungu, lengo lake kuu. Tungezaliwa katika hali ya maumbile tu, utashi ungeweza kumuelekea au kutomuelekea kwa hiari. Kumbe katika hali tuliyozaliwa nayo, kutokana na dhambi asili, tuko dhaifu katika kushika sheria ya kimaumbile, na pasipo neema hatuwezi kumpenda Mungu kuliko nafsi yetu. Vurugu za tabia mbovu, zinazoonekana wazi kutosha, ni “dalili inayothibitisha kwa kiasi kikubwa uwepo wa dhambi asili” (Thoma wa Akwino) uliofunuliwa na Mungu. Badala ya ulinganifu wa asili kati ya Mungu na roho, roho na mwili, mwili na vitu, zimezuka vurugu pande zote tatu.

Kwa stahili za Mwokozi ubatizo umetuondolea dhambi asili na kutupatia neema inayotia utakatifu na maadili ya kumiminiwa: kwa imani akili yetu imeangazwa Kimungu, na kwa tumaini na upendo utashi wetu umeelekezwa kwa Mungu. Lakini hata wabatizwa wanaodumu katika neema inayotia utakatifu, wanaendelea kuwa na madonda ambayo pengine yanatia uchungu na ambayo tumeachiwa kama fursa ya kupiga vita na kustahili taji. Mtaguso wa Trento umefundisha kuwa ndani ya waliobatizwa inabaki cheche ya tabia mbovu kusudi washindane nayo kwa neema ya Kristo, na kuwa wasipokubali cheche hiyo haiwezi kuwadhuru. “Utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena… Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake” (Rom 6:6,12).

Tusipoufisha “utu wa kale”, tutaendelea kutawaliwa na maono yetu: wasiotambua ukweli huo ni kwamba ndani mwao neema haina nguvu; umimi unawatawala, hata kama silika yao ina maelekeo mazuri yanayodhaniwa kuwa maadili halisi, kumbe siyo. Hatuna haja ya kujuta dhambi asili tuliyorithi tu bila kuitaka, ila tujitahidi kufuta matokeo yake, hasa tabia mbovu inayotuelekeza kutenda dhambi. Kwa kazi hiyo ya kudumu, madonda tuliyoyazungumzia yanazidi kugeuka makovu kwa ustawi wa neema ambayo inayaponya na kutuinua kwenye uzima mpya. Kwa njia ya ufishaji neema haiangamizi umbile, bali inalirekebisha likubali zaidi na zaidi kufanyiwa kazi na Mungu.

Matokeo ya dhambi zetu binafsi[hariri | hariri chanzo]

Ufishaji unahitajika pia kwa sababu dhambi ikirudiwarudiwa inazaa tabia mbaya inayoitwa kilema. Vilema ni mazoea ya kuona, kupima, kutaka na kutenda yanayojenga roho potovu isiyolingana na Mungu; vinaweza vikajitokeza katika mwili pia, hata ni haki kusema mtu wa makamo amesababisha sura yake iwe ilivyo. Tukiungama dhambi zetu kwa majuto ya kutosha, ondoleo lake linaacha maelekeo kadhaa yanayoitwa mabaki ya dhambi; k.mf. aliyetawaliwa na ulevi, akiondolewa dhambi anabaki na kilema hicho hivi kwamba asipokwepa nafasi ataiangukia tena. Maelekeo hayo mabaya yanatakiwa kufishwa, hasa upande wa kutopendana: “Mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana! Basi nasema: Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.” (Gal 5:15). Nafasi ya ufishaji ni pana kwa sababu vilema vinavyotokana na mizizi ya dhambi ni vingi na pengine vibaya kuliko hiyo.

Tunapaswa kufanya malipizi kwa dhambi tulizokwishaondolewa, kusudi tusizirudie. Adili la toba halimfanyi tu mtu achukie dhambi kwa sababu ni kinyume cha Mungu, bali pia aitolee haki yake fidia, kwa kuwa kila dhambi inastahili adhabu, kama vile kila tendo linalotokana na upendo linavyostahili tuzo. Ndiyo maana tunapoondolewa dhambi katika kitubio tunaagizwa malipizi fulani ili tuondolewe adhabu ya muda ambayo kwa kawaida inadumu kutupasa: hivyo tunalipa walau sehemu ya deni letu. Kwa ajili hiyohiyo tunapaswa kuvumilia tabu za maisha, halafu subira isipotosha kututakasa itatubidi tupitie toharani: kwa Wakatoliki dogma hiyo inathibitisha haja ya ufishaji, kwa kutuonyesha tunavyopaswa kulipa deni lote, ama duniani ama kisha kufa. Ila majuto yaliyojaa upendo yanaweza yakafuta dhambi na adhabu pia, kama yalivyofanya yale machozi yaliyobarikiwa na Yesu akisema, “Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47). Anayepinga ufishaji atakunywa uovu kama maji, akiziita dhambi nyepesi “mapungufu”, na dhambi za mauti “udhaifu wa kibinadamu”.

Halafu tunapaswa kupambana na roho ya ulimwengu na shetani: “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Ef 6:12). Ili tumshinde shetani, anayetushawishi kutenda kwanza makosa madogo, halafu yale makubwa, Bwana ametuambia tutumie sala, mfungo na sadaka: “Namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga” (Math 17:21). Hapo kishawishi kitakuwa nafasi ya kutekeleza imani, tumaini na upendo: tutajikuta tunahitaji kujitahidi na kustahili zaidi tusiridhike na matendo maadilifu mapungufu.

Ukuu wa lengo lipitalo maumbile unadai ufishaji wa pekee[hariri | hariri chanzo]

Kwa kuwa tumeitiwa lengo lipitalo maumbile ambalo ukuu wake hauna mipaka - yaani Mungu mwenyewe katika maisha yake ya ndani - haitoshi tufuate akili adili, tukiweka maono chini yake. Tunapaswa kutenda daima kama watoto wa Mungu, tukiweka akili chini ya imani, hivi kwamba upendo wa Mungu uongoze matendo yetu yote. Kwa hiyo ni lazima tutengane na yale yote ambayo ni ya kidunia tu au hayawezi kuwa njia ya kumuendea Mungu na ya kufikisha watu kwake. Tunapaswa kushinda mahangaiko mbalimbali ya kibinadamu yasije yakatawala utendaji wetu kwa hasara ya uzima wa neema: “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu… Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi” (Kol 3:1-3,5). “Muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu. Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita” (1Kor 7:29-31). Tukitaka kweli kwenda kwa Mungu, tusiweke makao yetu hapa, bali tutumie maisha haya ili kujipatia uzima wa milele. Lengo letu lipitalo maumbile linadai tujikanie yale yote yaliyo ya kibinadamu tu, hata kama ni halali, yasije yakatukwamisha.

Kwa mfano, “adili la kujipatia la kiasi linadai kwamba katika kutumia vyakula tufuate kipimo cha akili, yaani kiasi kinachoepuka yanayoweza kudhuru afya na kazi za akili na utashi. Kumbe kiasi cha Kikristo kinafuata kipimo cha Kimungu na kudai mtu aupe mwili wake mazoezi magumu na kuutia katika nidhamu kamili kwa kujinyima na kwa njia nyingine za namna hiyo. Lengo lake si la kimaumbile tu, bali ni kutufanya raia pamoja na watu wa Mungu, na watu wa jamaa ya Mungu” (Thoma wa Akwino). Hayo ni ya kweli zaidi kwa walioshika utume: “Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari” (2Tim 2:4). Vilevile askari wa Kristo asizame katika malimwengu, la sivyo atakuwa kama chumvi iliyoharibika: hapo “itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu” (Math 5:13).

Haja ya kumuiga Yesu msulubiwa[hariri | hariri chanzo]

“Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate” (Lk 9:23). Tunapaswa kumfuata Yesu aliyekuja si kutufundisha falsafa au elimujamii, bali kutuokoa kwa kufa msalabani. “Kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye. Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu” (Rom 8:17-18).

“Nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu… Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao… tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa” (1Kor 4:9,11,13). “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; sikuzote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu… Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu” (2Kor 4:8-10,12). Maneno hayo yanachora ukweli wa maisha ya mitume kuanzia Pentekoste hadi kifodini chao: kisha kuchapwa viboko walitoka “katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo” (Mdo 5:41). Walibeba msalaba wakachapwa sura ya Yesu ili waendeleze ukombozi kwa njia alizozifuata yeye. Roho hiyohiyo ya kulingana na Kristo imeonekana katika watakatifu wote, nasi tunapaswa kujilisha kila siku mifano yao. Ulimwengu hauhitaji wataalamu tu, bali hasa watakatifu wanaoleta tena kati ya watu sura hai ya Mwokozi.

Hizo sababu nne za ufishaji zinaweza kujumlishwa katika mbili tu: chuki kwa dhambi na upendo kwa Mungu. Ndiyo roho inayotakiwa kuchochea ufishaji wa nje na wa ndani. Jibu halisi kwa fikra za kidunia ni kumpenda Yesu msulubiwa; upendo huo unatufanya tufanane naye na kuokoa watu pamoja naye, tukifuata njia zilezile za kwake. Hivyo ufishaji, badala ya kuangamiza umbile letu, utalikomboa na kulirekebisha. Utatuwezesha kuelewa maana nzito ya msemo huu: kumtumikia Mungu ni kutawala. Ni kutawala juu ya maono, juu ya roho ya ulimwengu, juu ya mawazo yake ya uongo, juu ya mifano yake, juu ya shetani na juu ya uovu wake. Ni kutawala pamoja na Mungu kwa kushiriki zaidi na zaidi uzima wake wa ndani, kufuatana na sheria hii: maisha yasiposhuka, yanapanda. Mtu hawezi kuishi bila kupenda, na akijinyima kila pendo la chini linaloelekeza kwenye mauti, atazidi kufungua roho yake impende Mungu pamoja na watu ndani mwake.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. In the New Testament, Saint John the Baptist is the most clear example of a person practising corporal mortification. According to Mark 1:6, "John was clothed with a garment of camel’s hair, and had a leather girdle about his loins, and he ate locusts and wild honey"
  2. Fikra hizo, ambazo zinakanusha roho ya imani katika mwenendo, zinazuka upya daima kwa namna mbalimbali zikidharau ufishaji badala ya kuuona ni ukombozi unaochangia ustawi wa roho. Eti! Kwa nini kusema juu ya ufishaji, ikiwa Ukristo ni mafundisho ya uzima; juu ya kujinyima, ikiwa Ukristo unatakiwa kukoleza utendaji wote wa binadamu; juu ya utiifu, ikiwa Ukristo unaleta uhuru? Mbona umbile letu ni jema, linatokana na Mungu na kuelekea kumpenda kuliko vyote? Wanaosema hivyo wanasahau maneno ya Mwokozi: “Amin, amin, nawaambia: Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele” (Yoh 12:24-25). Wanasema tena: kwa nini kupinga maoni na matakwa yetu? Eti! Ni kujifanya watumwa wasioweza kutenda wanavyotaka, na ni kupoteza uhusiano na ulimwengu tunaopaswa kuuboresha, si kuudharau. Hawaelewi kwamba waandishi wa Kiroho kwa neno “matakwa yetu” walimaanisha yale yasiyolingana na ya Mungu. Fikra hizo, zikichanganya kiujanja ukweli na uongo, zinatumia hata maneno: “Neema haiangamizi umbile, bali inalikamilisha”. Uhaba wa imani unayapotosha, kwa kuwa hapo Thoma wa Akwino alizungumzia umbile lenyewe lilivyoumbwa awali na Mungu, si umbile lililojeruhiwa na kuanguka, jinsi lilivyo sasa kutokana na dhambi asili na dhambi zetu binafsi. Dhana hizo hazichelewi kuonyesha matokeo yake: “kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake” (Lk 6:44). Hao mitume wa aina mpya, wakitaka kupendeza ulimwengu wanaufuata badala ya kuuongoa; wanapuuzia matokeo ya dhambi asili na uovu mkuu wa dhambi ya mauti iliyo chukizo kwa Mungu, si tu dhara kwa binadamu. Wanapuuzia hasa uzito wa dhambi za roho: kutosadiki, kujiamini, kiburi. Wanaona kosa kubwa zaidi ni kutojihusisha na shughuli za jamii, hivyo maisha ya sala tu kwao ni ya bure. Mungu alijibu mwenyewe fikra hizo za Umarekani kwa utakatifu wa Teresa wa Mtoto Yesu na uenezi wa uangavu wake. Hao wanapuuzia tena ukuu usiopimika wa lengo letu, yaani Mungu asili ya neema. Hivyo badala ya kusema juu ya uzima wa milele, wanazungumzia maadili yanayohusika kidogo tu na dini, na hawaonyeshi upinzani wa moja kwa moja kati ya mbingu na moto. Hatimaye wanasahau kuwa msalaba ndio chombo kilichochaguliwa na Bwana ili kuuokoa ulimwengu. Matokeo ya fikra hizo yanaonyesha kuwa asili yake ni ubinadamu tu, unaokanusha walau kimatendo mambo yanayopita maumbile, na hivyo hauoni ufishaji umo katika kiini cha Ukristo, ni kitu kimoja na toba ambayo ni ya lazima kwa wote. Kwa namna nyingine fikra hizo ziliwahi kujitokeza kati ya Watulivu, hasa M. Molinos aliyedai kwamba “kutaka kutenda kunamchukiza Mungu, anayetaka kutenda peke yake ndani mwetu”. Tusipotenda tena, eti! Tunajiangamiza ili Mungu tu aishi na kutawala ndani yetu. Kwa msingi huo alidai tusimfikirie wala kumpenda, tusifikirie mbingu wala moto, tusizingatie matendo yetu wala kasoro zetu, tusitamani ukamilifu wala wokovu, tusimuombe Mungu chochote ila tujiachilie kwake atekeleze matakwa yake ndani yetu pasipo mchango wetu. Hatimaye alisema, “Mtu hahitaji tena kupinga vishawishi, ila asivijali; msalaba wa hiari wa kujifisha ni mzigo unaolemea na wa bure ambao tuutupe”. Eti! Vishawishi vinafaa daima, hata vinaposababisha maovu: vikitujia si lazima tutekeleze maadili yaliyo kinyume chake, bali tuvikubali tu, na hivyo tujitambue si kitu. Fikra hizo zinatumbukia uzembe tu.
  3. Kinyume cha fikra za kidunia mara mojamoja unapatikana ugumu wa maisha unaotokana na kiburi, kama ule wa Wajanseni, waliosahau kuwa roho ya ufishaji wa Kikristo ni upendo wa Mungu. Mafundisho yao yalizidisha matokeo ya dhambi asili hata wakasema, “mtu anatakiwa kufanya malipizi maisha yake yote kwa dhambi asili”. Walizuia watu wasikomunike wakisema hawastahili muungano huo na Bwana, isipokuwa wenye kumpenda Mungu kitakatifu. Walisahau kuwa huo upendo safi ni tunda la ekaristi, mradi mtu aipokee kwa bidii. Misimamo mikali kama huo haileti kamwe ukombozi wala amani.
  4. According to the Catechism of the Catholic Church, "[t]he way of perfection passes by way of the Cross. There is no holiness without renunciation and spiritual battle. Spiritual progress entails the ascesis and mortification that gradually lead to living in the peace and joy of the Beatitudes: ‘He who climbs never stops going from beginning to beginning, through beginnings that have no end. He never stops desiring what he already knows.’". "Catechism of the Catholic Church - Point 2015". www.vatican.va. Iliwekwa mnamo 2017-04-05.  "Jesus' call to conversion and penance, like that of the prophets before him, does not aim first at outward works, "sackcloth and ashes," fasting and mortification, but at the conversion of the heart, interior conversion. Without this, such penances remain sterile and false; however, interior conversion urges expression in visible signs, gestures and works of penance." (CCC 1430) CCC 1430
  5. Kumfuasa Yesu Kristo III,54

Marejeo[hariri | hariri chanzo]